27
Muda wa asubuhi ulipofika, wakuu wote wa makuhani na wazee wa watu walikula njama dhidi ya Yesu wapate kumuua. Walimfunga, walimwongoza, na kumfikisha kwa Liwali Pilato. Kisha wakati Yuda, ambaye alikuwa amemsaliti, aliona kwamba Yesu amekwisha kuhukumiwa, alijuta na kurudisha vipande thelathini vya fedha kwa mkuu wa makuhani na wazee, na akasema, “Nimefanya dhambi kwa kuisaliti damu isiyo na hatia.” Lakini wakajibu, “Inatuhusu nini sisi? Yaangalie hayo mwenyewe.” Kisha alivirusha chini vile vipande vya fedha katika hekalu, na kuondoka zake na kujinyonga mwenyewe. Mkuu wa makuhani alivichukua vile vipande vya fedha na kusema, “Si halali kuiweka fedha hii katika hazina, kwa sababu ni gharama ya damu.” Walijadiliana kwa pamoja na fedha ikatumika kununulia shamba la mfinyazi la kuzika wageni. Kwa sababu hii shamba hilo limekuwa likiitwa, “Shamba la damu” hadi leo hii. Kisha lile neno lililokuwa limenenwa na nabii Yeremia lilitimia, kusema, “Walitwaa vipande thelathini vya fedha, gharama iliyopangwa na watu wa Israel kwa ajili yake, 10 na waliitumia kwa shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyokuwa amenielekeza.” 11 Sasa Yesu alisimama mbele ya liwali, na liwali akamwuliza, “Je! Wewe ni mfalme wa Wayahudi?” Yesu alimjibu, “Wewe wasema hivyo.” 12 Lakini wakati aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu chochote. 13 Kisha Pilato alimwambia, “Hujayasikia mashitaka yote dhidi yako?” 14 Lakini hakumjibu hata neno moja, hivyo liwali alijawa na mshangao. 15 Sasa katika sikukuu ilikuwa desturi ya liwali kumfungua mfungwa mmoja anayechaguliwa na umati. 16 Wakati huo walikuwa na mfungwa sugu jina lake Baraba. 17 Hivyo wakati walipokuwa wamekusanyika pamoja, Pilato aliwauliza, “Ni nani mnataka tumfungue kwa ajili yenu?” Baraba au Yesu anayeitwa Kristo?” 18 Kwa sababu alijua kwamba wamekwisha kumkamata kwa sababu ya chuki. 19 Wakati alipokuwa akiketi kwenye kiti chake cha hukumu, mke wake alimtumia neno na kusema, “Usitende jambo lolote kwa mtu huyo asiye na hatia. Kwani nimeteswa mno hata leo katika ndoto kwa sababu yake.” 20 Ndipo wakuu wa makuhani na wazee waliwashawishi makutano wamwombe Baraba, na Yesu auawe. 21 Liwali aliwauliza, “Ni yupi kati ya wawili mnataka mimi nimwachie kwenu?” Walisema, “Baraba.” 22 Pilato akawaambia, “Nimtendee nini Yesu anayeitwa Kristo?” Wote wakajibu, “Msulibishe” 23 Naye akasema, “Kwa nini, ni kosa gani ametenda?” Lakini walizidi kupaza sauti hata juu mno, “Msulibishe.” 24 Hivyo wakati Pilato alipoona hawezi kufanya lolote, lakini badala yake vurugu zilikuwa zimeanza, alitwaa maji akanawa mikono yake mbele ya umati, na kusema, “Mimi sina hatia juu ya damu ya mtu huyu asiye na hatia. Yaangalieni haya wenyewe.” 25 Watu wote wakasema, “Damu yake iwe juu yetu na watoto wetu.” 26 Kisha akamfungulia Baraba kwao, lakini alimpiga mijeredi Yesu na kumkabidhi kwao kwenda kusulibiwa. 27 Kisha askari wa liwali wakamchukua Yesu mpaka Praitorio na kundi kubwa la maaskari wote wakamkusanyika. 28 Wakamvua nguo zake na kumvika kanzu ya rangi nyekundu. 29 Kisha wakatengeneza taji ya miiba na kuiweka juu ya kichwa chake, na walimwekea mwanzi katika mkono wake wa kuume. Walipiga magoti mbele yake na kumkejeri, wakisema, “Salamu, Mfalme wa Wayahudi?” 30 Na walimtemea mate, na walitwaa mwanzi na kumpiga kichwani. 31 Wakati walipokuwa wakimkejeri, walimvua ile kanzu na kumvika nguo zake, na kumwongoza kwenda kumsulibisha. 32 Walipotoka nje, walimwona mtu kutoka Krene jina lake Simeoni, ambaye walimlazimisha kwenda nao ili apate kuubeba msalaba wake. 33 Walipofika mahali paitwapo Galigotha, maana yake, “Eneo la fuvu la Kichwa.” 34 Walimpa siki iliyochanganywa na nyongo anywe. Lakini alipoionja, hakuweza kuinywa. 35 Wakati walipokuwa wamemsulibisha, waligawana mavazi yake kwa kupiga kura. 36 Na waliketi na kumwangalia. 37 Juu ya kichwa chake waliweka mashitaka dhidi yake yakisomeka, “Huyu ni Yesu, mfalme wa Wayahudi.” 38 Wanyang'anyi wawili walisulibiwa pamoja naye, mmoja upande wa kulia wake na mwingine wa kushoto. 39 Wale waliokuwa wakipita walimdhihaki, wakitikisa vichwa vyao 40 na kusema, “Wewe uliyekuwa unataka kuliharibu hekalu na kulijenga katika siku tatu, jiokoe mwenyewe! Kama ni Mwana wa Mungu, shuka chini utoke msalabani!” 41 Katika hali ile ile wakuu wa makuhani walikuwa wakimkashifu, pamoja na waandishi na wazee, na kusema, 42 “Aliokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni Mfalme wa Wayahudi. Na ashuke chini toka msalabani, ndipo tutakapomwamini. 43 Alimtumaini Mungu. Acha Mungu amwokoe sasa kama anataka, kwa sababu alisema, 'Mimi ni Mwana wa Mungu.'” 44 Na wale wanyang'anyi waliokuwa wamesulibiwa pamoja naye pia walisema maneno ya kumdhihaki. 45 Sasa kutoka saa sita kulikuwa na giza katika nchi yote hadi saa tisa. 46 Ilipofika saa tisa, Yesu akalia kwa sauti kuu, “Eloi, Eloi, lama thabakithan?” akimaanisha, “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?” 47 Wakati huo baadhi yao waliokuwa wamesimama pale walisikia, wakasema, “Anamwita Eliya.” 48 Mara moja mmoja wao alikimbia kuchukua sifongo na kuijaza kinywaji kichungu, akaiweka juu ya mti na kumpa apate kunywa. 49 Nao waliosalia wakasema, “Mwacheni peke yake, acheni tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.” 50 Kisha Yesu akalia tena kwa sauti kuu na akaitoa roho yake. 51 Tazama, Pazia la hekalu lilipasuka sehemu mbili kutokea juu hadi chini. Na ardhi ikatetemeka na miamba ikapasuka vipande. 52 Makaburi yalifunguka, na miili ya watakatifu wengi waliokuwa wamelala usingizi walifufuliwa. 53 Walitoka kwenye makaburi baada ya ufufuo wake, waliingia mji mtakatifu, na wakaonekana na wengi. 54 Basi yule akida na wale ambao walikuwa wakimtazama Yesu waliona tetemeko na mambo yaliyokuwa yakitokea, walijawa na woga sana na kusema, “Kweli huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” 55 Wanawake wengi waliokuwa wakimfuata Yesu kutoka Galilaya ili kumhudumia walikuwa pale wakitazama kutoka kwa mbali. 56 Miongini mwao walikuwa Mariamu Magdarena, Mariamu mama yake Yakobo na Joseph, na mama wa watoto wa Zebedayo 57 Ilipofika jioni, alikuja mtu tajiri kutoka Arimathayo, aliyeitwa Yusufu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. 58 Alimwendea Pilato na kuuomba mwili wa Yesu. Kisha Pilato aliagiza apate kupewa. 59 Yusufu aliuchukua mwili akaufunga na nguo ya sufi safi, 60 na akaulaza katika kaburi jipya lake alilokuwa amelichonga mwambani. Kisha akavingirisha jiwe kubwa likafunika mlango wa kaburi na akaenda zake. 61 Mariamu Magdalena na Mariamu mwingine walikuwa pale, wamekaa kuelekea kaburi. 62 Siku iliyofuata ambayo ilikuwa siku baada ya maandalio, wakuu wa makuhani na Mafarisayo walikusanyika pamoja kwa Pilato. 63 Wakamwambia, “Bwana, tunakumbuka kuwa wakati yule mdanganyifu alipokuwa hai, alisema, 'Baada ya siku tatu atafufuka tena.' 64 Kwahiyo, agiza kwamba kaburi lilindwe salama mpaka siku ya tatu. Vinginevyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kumwiba na kusema kwa watu, 'Amefufuka kutoka wafu.' Na udanganyifu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.” 65 Pilato akawaambia, “Chukueni walinzi. Nendeni mkafanye hali ya usalama kama muwezavyo.” 66 Hivyo walikwenda na kufanya kaburi kuwa salama, jiwe liligongwa mhuri na kuweka walinzi.