26
1 Wakati Yesu alipomaliza kusema maneno yote hayo, aliwaambia wanafunzi wake,
2 “Mnajua kwamba baada ya siku mbili kutakuwa na sikukuu ya pasaka, na mwana wa Adamu atatolewa ili asulibiwe.”
3 Baadaye wakuu wa makuhani na wazee wa watu walikutana pamoja katika makao ya Kuhani Mkuu, aliye kuwa anaitwa Kayafa.
4 Kwa pamoja walipanga njama ya kumkamata Yesu kwa siri na kumuua.
5 Kwa kuwa walisema, “Isifanyike wakati wa sikukuu, kusudi isije ikazuka ghasia miongoni mwa watu.”
6 Wakati Yesu alipokuwa Bethania katika nyumba ya Simoni mkoma,
7 alipokuwa amejinyoosha mezani, mwanamke mmoja alikuja kwake akiwa amebeba mkebe wa alabasta iliyokuwa na mafuta yenye thamani kubwa, na aliyamimina juu ya kichwa chake.
8 Lakini wanafunzi wake walipoona jambo hilo, walichukia na kusema, “Nini sababu ya hasara hii?
9 Haya yangeweza kuuzwa kwa kiasi kikubwa na kupewa maskini.”
10 Lakini Yesu, akiwa anajua hili, aliwaambia, “Kwa nini mnamsumbua mwanamke huyu? Kwa kuwa amefanya kitu kizuri kwangu.
11 Masikini mnao siku zote, lakini hamtakuwa pamoja nami daima.
12 Kwa sababu alipomimina mafuta haya juu ya mwili wangu, alifanya hivyo kwa ajili ya maziko yangu.
13 Kweli nawaambieni, popote Injili hii itakapohubiriwa katika ulimwengu mzima, kitendo alichofanya huyu mwanamke, pia kitakuwa kinasemwa kwa ajili ya kumkumbuka.”
14 Ndipo mmoja wa wale Kumi na wawili, aliyeitwa Yuda Iskariote, alienda kwa wakuu wa makuhani
15 na kusema, “Mtanipatia nini nikimsaliti?” Wakampimia Yuda vipande thelathini vya fedha.
16 Tangu muda huo alitafuta nafasi ya kumsaliti.
17 Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi walimwendea Yesu na kusema, “Wapi unataka tukuandalie ule chakula cha Pasaka?”
18 Akawaambia, “Nendeni mjini kwa mtu fulani na mwambieni, Mwalimu anasema, “Muda wangu umekaribia. Nitaitimiza Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.””
19 Wanafunzi walifanya kama Yesu alivyowaagiza, na waliandaa chakula cha Pasaka.
20 Ilipofika jioni, aliketi kula chakula pamoja na wale wanafunzi Kumi na Wawili.
21 Walipokuwa wanakula chakula, alisema, “Kweli nawaambia kwamba mmoja wenu atanisaliti.”
22 Walihuzunika sana, na kila mmoja alianza kumuuliza, “Je, hakika siyo mimi, Bwana?”
23 Akawajibu, “Yule ambaye anachovya mkono wake pamoja nami katika bakuli ndiye atakaye nisaliti.
24 Mwana wa Adamu ataondoka, kama alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu ambaye atamsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa vizuri kwa mtu huyo kama asingezaliwa.”
25 Yuda, ambaye angemsaliti alisema, “Je!, Ni mimi Rabi?” Yesu akamwambia, “Umesema jambo hilo wewe mwenyewe.”
26 Walipokuwa wakila chakula, Yesu aliutwaa mkate, akaubariki, na kuumega. Akawapa wanafunzi wake akisema, “Chukueni, mle. Huu ni mwili wangu.”
27 Akatwaa kikombe na kushukuru, akawapa na kusema, “Kunyweni wote katika hiki.
28 Kwa kuwa hii ni damu ya agano langu, inayomwagwa kwa ajili ya wengi kwa msamaha wa dhambi.
29 Lakini nawaambieni, sitakunywa tena matunda ya mzabibu huu, hadi siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”
30 Walipokuwa wamemaliza kuimba wimbo, walitoka kwenda Mlima wa Mizeituni.
31 Kisha Yesu aliwaambia, “Usiku huu ninyi nyote mtajikwaa kwa sababu yangu, kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji na kondoo wa kundi watatawanyika.
32 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”
33 Lakini Petro alimwambia, “Hata kama wote watakukataa kwa sababu ya mambo yatakayokupata, mimi sitakukataa.”
34 Yesu akamjibu, “kweli nakuambia, usiku huu kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”
35 Petro akamwambia, “hata kama ingenipasa kufa na wewe, sitakukana.” Na wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo.
36 Baadaye Yesu alienda nao mahali panapoitwa Gethsemane na aliwaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati nikienda huko na kuomba.”
37 Akamchukua Petro na wana wawili wa Zebedayo na akaanza kuhuzunika na kusononeka.
38 Kisha aliwaambia, “Roho yangu ina huzuni kubwa sana, hata kiasi cha kufa. Bakini hapa na mkeshe pamoja nami.”
39 Akenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, na kuomba. Akasema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki kiniepuke. Isiwe kama ninavyotaka mimi, bali kama utakavyo wewe.”
40 Akawaendea wanafunzi na akawakuta wamelala usingizi, na akamwambia Petro, “Kwa nini hamkuweza kukesha nami kwa saa moja?
41 Kesheni na kuomba kusudi msiingie majaribuni. Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”
42 Akaenda zake mara ya pili na kuomba, akasema, “Baba yangu, kama jambo hili haliwezi kuepukika na ni lazima nikinywee kikombe hiki, mapenzi yako yatimizwe.”
43 Akarudi tena na kuwakuta wamelala usingizi, kwa kuwa macho yao yalikuwa mazito.
44 Kisha akawaacha tena akaenda zake. Akaomba mara ya tatu akisema maneno yaleyale.
45 Baadaye Yesu aliwaendea wanafunzi wake na kuwaambia, “Bado mmelala tu na kujipumzisha? Tazameni, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anasalitiwa mikononi mwa wenye dhambi.
46 Amkeni, tuondoke. Tazama, yule anaye nisaliti amekaribia.”
47 Wakati alipokuwa bado anaongea, Yuda mmoja wa wale Kumi na Wawili, akafika. Kundi kubwa lilifika pamoja naye likitokea kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu. Walikuja na mapanga na marungu.
48 Tena mtu aliyekusudia kumsaliti Yesu alikuwa amewapa ishara, akisema, “Yule nitakayembusu, ndiye yeye. Mkamateni.”
49 Mara hiyo alikuja kwa Yesu na kusema, “Salamu, Mwalimu!” Na akambusu.
50 Yesu akamwambia, “Rafiki, lifanye lile ambalo limekuleta.” Ndipo wakaja, na kumnyooshea mikono Yesu, na kumkamata.
51 Tazama, mtu mmoja aliyekuwa pamoja na Yesu, alinyosha mkono wake, akachomoa upanga wake, na akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, na kumkata sikio lake.
52 Ndipo Yesu akamwambia, rudisha upanga wako pale ulipoutoa, kwa kuwa wote watumiao upanga wataangamizwa kwa upanga.
53 Mnadhani kuwa siwezi kumwita Baba yangu, naye akanitumia majeshi zaidi ya kumi na mawili ya malaika?
54 Lakini basi jinsi gani maandiko yangeweza kutimizwa, hivi ndivyo inapasa kutokea?”
55 Wakati huo Yesu akauambia umati, “Je! Mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kama mnyang'anyi? Kila siku nilikaa hekaluni nikifundisha, na hamkunishika!
56 Lakini yote haya yametendeka ili Maandiko ya manabii yatimie.” Ndipo wanafunzi wake wakamwacha na kukimbia.
57 Wale waliomkamata Yesu alimpeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, mahali ambapo waandishi na wazee walikuwa wamekusanyika pamoja.
58 Lakini Petro alimfuata nyuma kwa mbali hadi katika ukumbi wa Kuhani Mkuu. Aliingia ndani na kukaa pamoja na walinzi aone kitakachotokea.
59 Basi wakuu wa makuhani na Baraza lote walikuwa wakitafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu, kusudi wapate kumuua.
60 Ingawa walijitokeza mashahidi wengi, Lakini hawakupata sababu yoyote. Lakini baadaye mashahidi wawili walijitokeza mbele
61 na kusema, “ Mtu huyu alisema, ''Naweza kulivunja hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.”'
62 Kuhani Mkuu alisimama na kumwuliza, “Hauwezi kujibu? Hawa wanakushuhudia nini dhidi yako?”
63 Lakini Yesu alikaa kimya. Kuhani Mkuu akamwambia, “Kama Mungu aishivyo, nakuamuru utwambie, kama wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu.”
64 Yesu akamjibu, “Wewe mwenyewe umesema jambo hilo. Lakini nakuambia, toka sasa na kuendelea utamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kulia wenye Nguvu, na akija katika mawingu ya mbinguni.”
65 Ndipo Kuhani Mkuu alirarua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Je, twahitaji tena ushahidi wa nini? Angalia, tayari mmesikia akikufuru.
66 Je! Mnawaza nini? Wakajibu na kusema, “Anastahili kifo.”
67 Kisha walimtemea mate usoni na kumpiga ngumi, na kumchapa makofi kwa mikono yao,
68 na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo. Ni nani amekuchapa?”
69 Wakati huo Petro alikuwa amekaa nje katika ukumbi, na mtumishi wa kike alimwendea na kusema, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.”
70 Lakini alikana mbele yao wote, akisema, Sijui kitu unachosema.”
71 Alipoenda nje ya lango, mtumishi mwingine wa kike alimwona na kuwaambia waliokuwepo hapo, “Mtu huyu pia alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.”
72 Akakana tena kwa kiapo, “Mimi simjui mtu huyu.”
73 Muda mfupi baadaye, wale waliokuwa wamesimama karibu, walimwendea na kusema na Petro, “Kwa hakika wewe pia ni mmoja wao, kwa kuwa hata lafudhi yako inaonesha.”
74 Ndipo alianza kulaani na kuapa, “Mimi simfahamu mtu huyu,” na mara hiyo jogoo akawika.
75 Petro alikumbuka maneno aliyoambiwa na Yesu, “Kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu.”