16
Hagari Na Ishmaeli
1 Basi Sarai, mkewe Abramu, alikuwa hajamzalia watoto. Lakini alikuwa na mtumishi wa kike Mmisri jina lake Hagari,
2 hivyo Sarai akamwambia Abramu, “Bwana amenizuilia kupata watoto. Nenda, ukakutane kimwili na mtumishi wangu wa kike, huenda nitaweza kupata watoto kupitia kwake.”
Abramu akakubaliana na lile Sarai alilosema.
3 Hivyo baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani miaka kumi, Sarai akamchukua mtumishi wake wa kike wa Kimisri, Hagari na kumpa mumewe awe mke wake.
4 Akakutana kimwili na Hagari, naye akapata mimba.
Hagari alipojua kuwa ana mimba, alianza kumdharau Sarai.
5 Ndipo Sarai akamwambia Abramu, “Unawajibika na manyanyaso ninayoyapata. Nilimweka mtumishi wangu mikononi mwako, sasa kwa vile anajua kwamba ana mimba, ananidharau mimi. Bwana na aamue kati yako na mimi.”
6 Abramu akamwambia, “Mtumishi wako yuko mikononi mwako. Mtendee lolote unalofikiri ni bora zaidi.” Ndipo Sarai akamtesa Hagari, hivyo akamtoroka.
7 Malaika wa Bwana akamkuta Hagari karibu na chemchemi huko jangwani; ilikuwa chemchemi ile iliyokuwa kando ya barabara iendayo Shuri.
8 Malaika akamwambia, “Hagari, mtumishi wa Sarai, umetokea wapi, na unakwenda wapi?”
Akamjibu, “Ninamkimbia bibi yangu Sarai.”
9 Ndipo malaika wa Bwana akamwambia, “Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.”
10 Malaika akaendelea akasema, “Nitazidisha wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi mno wasiohesabika.”
11 Pia malaika wa Bwana akamwambia:
“Wewe sasa una mimba
nawe utamzaa mwana.
Utamwita jina lake Ishmaeli,
kwa sababu Bwana amesikia juu ya huzuni yako.
12 Atakuwa punda-mwitu katikati ya wanadamu,
mkono wake utakuwa dhidi ya kila mtu
na mkono wa kila mtu dhidi yake,
naye ataishi kwa uhasama
na ndugu zake wote.”
13 Hagari akampa Bwana aliyezungumza naye jina hili: “Wewe ndiwe Mungu unionaye mimi,” kwa maana alisema, “Sasa nimemwona yeye anayeniona mimi.”
14 Ndiyo sababu kisima kile kikaitwa Beer-Lahai-Roi, ambacho bado kipo huko hata leo kati ya Kadeshi na Beredi.
15 Hivyo Hagari akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwana Hagari aliyemzalia, Ishmaeli.
16 Abramu alikuwa na umri wa miaka themanini na sita wakati Hagari alipomzalia Ishmaeli.