8
Orodha Ya Viongozi Wa Jamaa Waliorudi Na Ezra
1 Hawa ndio viongozi wa jamaa pamoja na wale walioandikwa ambao walikuja pamoja nami kutoka Babeli wakati wa utawala wa Mfalme Artashasta:
2 wa wazao wa Finehasi, alikuwa Gershoni;
wa wazao wa Ithamari, alikuwa Danieli;
wa wazao wa Daudi, alikuwa Hatushi
3 wa wazao wa Shekania;
wa wazao wa Paroshi, alikuwa Zekaria, na watu 150 walioandikishwa pamoja naye;
4 wa wazao wa Pahath-Moabu, alikuwa Eliehoenai mwana wa Zerahia na wanaume 200 pamoja naye;
5 wa wazao wa Zatu, alikuwa Shekania mwana wa Yahazieli na wanaume 300 pamoja naye;
6 wa wazao wa Adini, alikuwa Ebedi mwana wa Yonathani na wanaume 50 pamoja naye;
7 wa wazao wa Elamu, alikuwa Yeshaya mwana wa Athalia, na wanaume 70 pamoja naye;
8 wa wazao wa Shefatia, alikuwa Zebadia mwana wa Mikaeli na wanaume 80 pamoja naye;
9 wa wazao wa Yoabu, alikuwa Obadia mwana wa Yehieli na wanaume 218 pamoja naye;
10 wa wazao wa Bani, alikuwa Shelomithi mwana wa Yosifia na wanaume 160 pamoja naye;
11 wa wazao wa Bebai, alikuwa Zekaria mwana wa Bebai na wanaume 28 pamoja naye;
12 wa wazao wa Azgadi, alikuwa Yohanani mwana wa Hakatani na wanaume 110 pamoja naye;
13 wa wazao wa Adonikamu, hawa walikuwa wa mwisho ambao majina yao ni Elifeleti, Yeueli, Shemaya na wanaume 60 pamoja nao;
14 wa wazao wa Bigwai, walikuwa Uthai na Zakuri na wanaume 70 pamoja nao.
Kurudi Yerusalemu
15 Niliwakusanya kwenye mto utiririkao kuelekea Ahava, nasi tukapiga kambi pale siku tatu. Wakati nilipokagua kati ya watu na makuhani, sikuwapata Walawi.
16 Basi niliwaita Eliezeri, Arieli, Shemaya, Elnathani, Yaribu, Elnathani, Nathani, Zekaria na Meshulamu waliokuwa viongozi na Yoyaribu na Elnathani waliokuwa wasomi,
17 nikawatuma kwa Ido kiongozi huko Kasifia. Niliwaambia watakayomwambia Ido na ndugu zake, watumishi wa Hekalu huko Kasifia, ili waweze kutuletea wahudumu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu.
18 Kwa sababu mkono wa neema wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, walituletea Sherebia, mtu mwenye uwezo kutoka wazao wa Mahli mwana wa Lawi, mwana wa Israeli, na wana wa Sherebia pamoja na ndugu zao wanaume kumi na wanane.
19 Naye Hashabia, pamoja na Yeshaya kutoka wazao wa Merari na ndugu zake na wapwa wake wanaume ishirini.
20 Vilevile walileta watumishi wa Hekalu 220, kikundi ambacho Daudi na maafisa walikuwa wamekiweka kusaidia Walawi. Wote walikuwa wameorodheshwa kwa majina.
21 Kando ya Mto Ahava, hapo nilitangaza kufunga, ili tujinyenyekeshe mbele za Mungu wetu na kumwomba kwa ajili ya kutujalia safari ya amani sisi na watoto wetu, pamoja na mali zetu zote.
22 Niliona aibu kumwomba mfalme askari na wapanda farasi wa kutulinda njiani kutokana na adui zetu, kwa sababu tulikwisha kumwambia mfalme, “Mkono wa neema wa Mungu wetu uko juu ya kila mmoja anayemtafuta, lakini hasira yake kubwa ni dhidi ya wote wamwachao.”
23 Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu wetu kuhusu jambo hili, naye akajibu maombi yetu.
24 Kisha niliwatenga viongozi wa makuhani kumi na wawili, pamoja na Sherebia, Hashabia na ndugu zao kumi,
25 nami nikawapimia fedha, dhahabu na vifaa ambavyo mfalme, washauri wake, maafisa wake na Israeli wote waliokuwepo walikuwa wamevitoa sadaka kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu.
26 Niliwapimia talanta 650 za fedha, vifaa vingine vya fedha vya uzito wa talanta mia moja, talanta mia moja za dhahabu,
27 mabakuli ishirini ya dhahabu ya thamani ya darkoni elfu moja, na vyombo viwili vya shaba iliyosuguliwa, ya thamani kama dhahabu.
28 Niliwaambia, “Ninyi pamoja na vyombo hivi ni wakfu kwa Bwana. Fedha na dhahabu ni sadaka ya hiari kwa Bwana, Mungu wa baba zenu.
29 Vilindeni kwa uangalifu mpaka mtakapovipima ndani ya vyumba vya nyumba ya Bwana katika Yerusalemu mbele ya makuhani, viongozi na Walawi pamoja na wakuu wa jamaa za Israeli.”
30 Ndipo makuhani na Walawi wakapokea fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu ambavyo vilipimwa na kupelekwa katika nyumba ya Mungu wetu mjini Yerusalemu.
31 Tulianza safari kutoka Mto Ahava kwenda Yerusalemu kwenye siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza. Mkono wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, naye njiani alitulinda dhidi ya adui na wanyangʼanyi.
32 Kwa hiyo tuliwasili Yerusalemu ambapo tulipumzika kwa siku tatu.
33 Katika siku ya nne, ndani ya nyumba ya Mungu wetu, tulipima fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu, tukakabidhi mikononi mwa kuhani Meremothi mwana wa Uria. Eleazari mwana wa Finehasi alikuwa pamoja naye, pia walikuwako Walawi wawili, Yozabadi mwana wa Yeshua na Noadia mwana wa Binui.
34 Kila kitu kilihesabiwa kwa idadi na kupimwa kwa uzito, nao uzito wote uliandikwa wakati ule.
35 Kisha mateka waliokuwa wamerudi kutoka utumwani wakatoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mungu wa Israeli: mafahali kumi na wawili kwa ajili ya Israeli wote, kondoo dume tisini na sita, wana-kondoo sabini na saba na mbuzi dume kumi na wawili kuwa sadaka ya dhambi. Hii yote ilikuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Bwana.
36 Pia walikabidhi manaibu wa mfalme na watawala wa Ngʼambo ya Mto Frati maagizo ya mfalme, ambao baadaye walitoa msaada kwa watu na kwa nyumba ya Mungu.