7
Ezra Awasili Yerusalemu
Baada ya mambo haya, wakati wa utawala wa Artashasta mfalme wa Uajemi, Ezra mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia, mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu, mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi, mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki, mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani mkuu Aroni. Huyu Ezra alipanda kutoka Babeli. Alikuwa mwalimu mwenye ujuzi mzuri katika sheria ya Mose, ambayo Bwana, Mungu wa Israeli, alikuwa ametoa. Mfalme alikuwa amempa Ezra kila kitu alichoomba, kwa maana Bwana Mungu wake alikuwa pamoja naye. Pia baadhi ya Waisraeli, wakiwemo makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu na watumishi wa Hekalu,* nao walikuja Yerusalemu mwaka wa saba wa utawala wa Mfalme Artashasta.
Ezra aliwasili Yerusalemu mwezi wa tano wa mwaka wa saba wa utawala wa Mfalme Artashasta. Ezra alianza safari yake kutoka Babeli tangu siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akawasili Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kwa maana mkono wa neema wa Mungu wake ulikuwa juu yake. 10 Kwa maana Ezra alikuwa amejitoa kwa moyo wote kujifunza na kushika sheria ya Bwana na kuwafundisha watu wa Israeli amri na sheria zake.
Barua Ya Ezra Kutoka Kwa Mfalme Artashasta
11 Hii ni nakala ya barua ambayo Mfalme Artashasta alikuwa amempa Ezra aliyekuwa kuhani na mwalimu, mtu aliyeelimika katika mambo yahusuyo maagizo na amri za Bwana kwa Israeli.
12 Artashasta, mfalme wa wafalme,
Kwa Ezra kuhani, mwalimu wa Sheria ya Mungu wa mbinguni:
Salamu.
 
13 Sasa naamuru kwamba mtu yeyote Mwisraeli katika ufalme wangu, pamoja na makuhani na Walawi, ambaye anataka kwenda Yerusalemu pamoja nawe aweza kwenda. 14 Unatumwa na mfalme na washauri wake saba kuchunguza kuhusu Yuda na Yerusalemu kulingana na Sheria ya Mungu wako, iliyoko mkononi mwako. 15 Zaidi ya hayo, uchukue pamoja nawe fedha na dhahabu ambazo mfalme na washauri wake wamempa Mungu wa Israeli kwa hiari, Mungu ambaye maskani yake yako Yerusalemu, 16 pia fedha na dhahabu zote unazoweza kupata kutoka jimbo la Babeli, pamoja na sadaka za hiari watakazotoa watu na makuhani kwa ajili ya Hekalu la Mungu wao katika Yerusalemu. 17 Hakikisha kwamba fedha hizi zimetumika kununua mafahali, kondoo dume na wana-kondoo pamoja na sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji, uvitoe dhabihu juu ya madhabahu ya Hekalu la Mungu wenu katika Yerusalemu.
18 Kisha wewe na Wayahudi ndugu zako mnaweza kufanya lolote linaloonekana jema sana kwa fedha na dhahabu zilizosalia, kulingana na mapenzi ya Mungu wenu. 19 Uvitoe kwa Mungu wa Yerusalemu vyombo vyote ulivyokabidhiwa kwa ajili ya ibada katika Hekalu la Mungu wako. 20 Kitu kingine chochote kinachohitajika kwa ajili ya Hekalu la Mungu wenu ambacho unatakiwa kukitoa, waweza kukitoa kutoka hazina ya mfalme.
21 Mimi, Mfalme Artashasta, sasa naagiza watunza hazina wote wa Ngʼambo ya Mto Frati kutoa kwa bidii chochote kwa Ezra kuhani na mwalimu wa Sheria ya Mungu wa mbinguni atakachohitaji kwenu, 22 talanta 100 za fedha, ngano kori 100, divai bathi 100,§ mafuta ya zeituni bathi 100, na chumvi kiasi chochote. 23 Chochote ambacho Mungu wa mbinguni ameagiza, kifanyike kwa ukamilifu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wa mbinguni. Kwa nini pawepo ghadhabu dhidi ya utawala wa mfalme na wanawe? 24 Pia ninyi fahamuni kuwa hamna mamlaka ya kuwatoza kodi, ushuru au ada makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu, watumishi wa Hekalu au wafanyakazi wengine kwenye nyumba ya Mungu.
25 Nawe Ezra, kufuatana na hekima ya Mungu wenu uliyo nayo, weka mahakimu na waamuzi wote wanaozifahamu sheria za Mungu wenu ili watoe haki kwa watu wote wa Ngʼambo ya Mto Frati. Nawe inakupasa umfundishe yeyote ambaye hazifahamu. 26 Yeyote ambaye hataitii sheria ya Mungu wenu pia sheria ya mfalme, hakika lazima aadhibiwe kwa kuuawa, kuhamishwa, kunyangʼanywa mali au kufungwa gerezani.
27 Sifa ziwe kwa Bwana, Mungu wa baba zetu, Mungu ambaye kwa njia hii ameweka ndani ya moyo wa mfalme kuipa heshima nyumba ya Bwana iliyoko Yerusalemu, kwa namna hii 28 ambaye ameniongezea kibali chake mbele ya mfalme, washauri wake na maafisa wote wa mfalme wenye uwezo. Kwa kuwa mkono wa Bwana Mungu wangu ulikuwa pamoja nami, nilijipa moyo nikakusanya watu walio viongozi kutoka Israeli wakwee pamoja nami.
* 7:7 Yaani Wanethini (pia 7:24). 7:22 Talanta 100 za fedha ni sawa na kilo 3,400. 7:22 Kori 100 za ngano ni sawa na kilo 10,000. § 7:22 Bathi 100 za divai ni sawa na lita 2,000.