3
1 Uwakumbushe kuwanyenyekea viongozi na mamlaka, kuwatii na kuwa tayari katika kila kazi njema.
2 Wakumbushe kutokumtendea mtu yeyote ubaya, waepuke majibizano, wawape nafasi watu wengine katika kufanya maamuzi, na kuonesha unyenyekevu kwa watu wote.
3 Kwa kuwa sisi pia tulikuwa na mawazo potofu na wakaidi. Tulikuwa upotevuni na tulifanywa watumwa kwa tamaa nyingi na starehe. Tuliishi katika wivu na uovu. Tulichukiza na kuchukiana.
4 Lakini wakati huruma ya Mungu mwokozi wetu na upendo wake kwa wanadamu ulipoonekana,
5 haikuwa kwa matendo yetu ya haki tuliyofanya, bali alituokoa kwa neema yake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa upya na katika kufanywa upya kwa Roho Mtakatifu.
6 Mungu alimwaga Roho Mtakatifu kwa wingi juu yetu kupitia Yesu Kristo mwokozi wetu.
7 Alifanya hivi ili kwamba, tukiwa tumehesabiwa haki kwa neema yake, tuwe washirika katika uhakika wa maisha ya milele.
8 Huu ni ujumbe wa kuaminika. Ninawataka myanene kwa ujasiri mambo haya, ili kwamba wale wanaomwamini Mungu wawe na dhamira juu ya kazi nzuri ambayo aliiweka mbele yao. Mambo haya ni mazuri na yanafaida kwa ajili ya watu wote.
9 Lakini jiepusheni na mijadala ya kipumbavu, nasaba, mashindano, na migongano kuhusu sheria. Mambo hayo hayana maana wala faida.
10 Mkataeni yeyote anayesababisha migawanyiko kati yenu. Baada ya onyo moja ama mawili,
11 jueni kwamba mtu wa jinsi hiyo ameiacha njia iliyo sahihi na anatenda dhambi na kujihukumu mwenyewe.
12 Nitakapomtuma kwako Artemi au Tikiko, harakisha uje kwangu huku Nikopoli ambapo nimeamua kukaa kipindi cha baridi.
13 Harakisha na umtume Zena mtaalamu katika sheria, na Apolo, pasipo kupungukiwa na kitu.
14 Watu wetu lazima wajifunze kujishughulisha katika kazi nzuri ambazo zinagusa mahitaji muhimu ili kwamba wasije wakawa wasiozaa matunda.
15 Wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu wale watupendao katika imani. Neema iwe nanyi nyote.