6
Wale wote walio chini ya nira kama watumwa wawachukulie mabwana zao kama wenye heshima zote, wanatakiwa kufanya hivyo ili jina la Mungu na mafundisho yasitukanwe. Watumwa wenye mabwana waaminio wasiwadharau kwa sababu wao ni ndugu. Badala yake, wawatumikie zaidi. Kwa sababu mabwana wanaosaidiwa kazi zao ni waamini na wanapendwa. Fundisha na kuyatangaza mambo haya. Iwapo mtu fulani anafundisha kwa upotovu na hayapokei maelekezo yetu yenye kuaminika, ambayo ni maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo, iwapo hawalikubali fundisho liongozalo kwenye utauwa. Mtu huyo anajivuna na hajui chochote. Badala yake, ana vurugu na mabishano juu ya maneno. Maneno haya huzaa wivu, ugomvi, matukano, shuku mbaya, na vurugu za mara kwa mara kati ya watu wenye akili zilizoharibika. Wanaiacha kweli. Wanafikiri kwamba utauwa ni njia ya kuwa matajiri” Sasa utauwa na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na chochote duniani. Wala hatuwezi kuchukua chochote kutoka duniani. Badala yake, tutosheke na chakula na mavazi. Sasa hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu, katika mtego. Huanguka katika upumbavu mwingi na tamaa mbaya, na katika kitu chochote kinachowafanya watu wazame katika maangamizi na uharibifu. 10 Kwa kuwa kupenda fedha ni chanzo cha aina zote za uovu. Watu ambao hutamani hiyo, wamepotoshwa mbali na imani na wamejichoma wenyewe kwa huzuni nyingi. 11 Lakini wewe mtu wa Mungu, yakimbie mambo hayo. Fuata haki, utauwa, uaminifu, upendo, usitahimilivu, na upole. 12 Piga vita vizuri vya imani. Shikilia uzima wa milele ulioitiwa. Ilikuwa ni kwa sababu hii kwamba ulitoa ushuhuda mbele ya mashahidi wengi kwa kile kilicho chema. 13 Nakupa amri hii mbele za Mungu, anayesababisha vitu vyote kuishi, na mbele ya Yesu Kristo, aliyenena iliyo kweli kwa Pontio Pilato: 14 itunze amri kwa ukamilifu, pasipo mashaka, hadi ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo. 15 Mungu atadhihirisha ujio wake kwa wakati sahihi- Mungu, Mbarikiwa, nguvu pekee, Mfalme anayetawala, Bwana anayeongoza. 16 Peke yake anaishi milele na akaaye katika mwanga usiokaribiriwa. Hakuna mtu awezaye kumwona wala awezaye kumtazama. Kwake iwe heshima na uweza wa milele. Amina. 17 Waambie matajiri katika ulimwengu huu wasijivune, na wasitumaini katika utajiri, ambao siyo wa uhakika. Badala yake, wanapaswa kumtumaini Mungu. Ambaye hutupatia utajiri wote wa kweli ili tufurahie. 18 Waambie watende mema, watajirike katika kazi njema, wawe wakarimu, na utayari wa kutoa. 19 Katika njia hiyo watajiwekea msingi mzuri kwa mambo yajayo, ili kwamba waweze kushika maisha halisi. 20 Timotheo, linda kile ulichopewa. Jiepushe na majadiliano ya kipumbavu na mabishano yenye kujipinga ambayo kwa kwa uongo huitwamaarifa. 21 Baadhi ya watu huyatangaza mambo haya, na hivyo wameikosa imani. Neema na iwe pamoja nawe.