16
1 BWANA akamwambia Samweli, “Utamlilia Sauli kwa muda gani, ikiwa nimemkataa asiwe mfalme juu ya Israeli? Ijaze pembe yako mafuta na uende. Nitakutuma kwa Yese akaaye Bethlehemu, maana nimejichagulia mfalme katika wanawe.
2 Samweli akasema, “Jinsi gani nitaenda? Kama Sauli akisikia jambo hili, ataniua.” BWANA akasema, “chukua mtamba na useme, 'Nimekuja kutoa dhabihu kwa BWANA.'
3 Umwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonesha kile utakachofanya. Utamtia mafuta kwa ajili yangu yule nitakaye kuambia.”
4 Samweli akafanya kama BWANA alivyosema na akaenda Bethlehemu. Wazee wa mji walikuwa wakitetemeka walipokuja kuonana naye na wakasema, “Je, umekuja kwa amani?”
5 Naye akasema, “kwa amani; Nimekuja kutoa dhabihu kwa BWANA. Jitoeni wenyewe kwa BWANA kwa ajili ya dhabihu na muandamane nami,” Na akamweka wakfu Yese na watoto wake kwa BWANA, na baadaye aliwaita wote kwenye dhabihu.
6 Walipofika, akamwangalia Eliabu na akajisemea mwenyewe kwamba mtiwa mafuta wa BWANA hakika amesimama mbele yake.
7 Lakini BWANA akamwambia Samweli, “Usimwangalie sura yake ya nje, au kimo cha umbo lake; kwa sababu nimemkataa. Maana BWANA haangalii kama mtu aangaliavyo; mtu hutazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo.”
8 Kisha Yese akamwita Abinadabu akamwambia apite mbele ya Samweli. Na Samweli akasema, “Hata huyu BWANA hakumchagua.”
9 Kisha Yese akmwambia Shama apite karibu. Na Samweli akasema, “Hata huyu BWANA hakumchagua.”
10 Yese akawaleta watoto wake saba wakapita mbele ya Samweli. Na Samweli akamwambia Yese, “Hakuna hata mmoja aliyechaguliwa na BWANA kati ya hawa.”
11 Kisha Samweli akamuulia Yese, “Je, watoto wako wote wako hapa?” Naye akajibu, “Yupo mdogo kabisa lakini anachunga kondoo.” Samweli akamwambia Yese, “Tuma watu wakamwite; maana hatutakaa chini hadi atakapofika hapa.”
12 Yese akawatuma watu wakamleta. Naye kijana huyu alikuwa mwekundu na mwenye macho mazuri na mwenye muonekano mzuri. BWANA akasema, “Amka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.”
13 Ndipo Samweli akachukua pembe yenye mafuta na kumtia mafuta katikati ya kaka zake. Roho wa BWANA akamwijia Daudi kwa nguvu tangu siku hiyo na kuendelea. Kisha Samweli akanyanyuka na kwenda Rama.
14 Basi Roho wa BWANA akamwacha Sauli, badala yake roho ya ubaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua.
15 Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Tazama, roho ya ubaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.
16 Haya bwana wetu hebu sasa amuru watumishi wako walio mbele yako wamtafute mtu mwenye ujuzi wa kupiga kinubi. Basi ikwa roho wa ubaya kutoka kwa Mungu yuko juu yako, atakipiga kinubi nawe utajisikia vizuri.”
17 Sauli akawaambia watumishi wake, “Mnitafutie mtu anayeweza kupiga vizuri na mmlete kwangu.”
18 Ndipo kijana mmoja kati yao akajibu, na kusema, “Nimemuona mtoto wa Yese Mbethtelehemu, aliye mjuzi katika kupiga, ni mwenye nguvu, mtu jasiri, mtu wa vita, mwenye busara aongeapo, mtu mzuri kwa uso; na BWANA yuko pamoja naye.”
19 Hivyo Sauli akawatuma wajumbe kwa Yese, na kusema, “Nitumie mtoto wako Daudi, anayewatunza kondoo.” 1 Samweli! 6: 20-21
20 Yese akamchukua punda aliyebeba mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, na akamtuma kwa Sauli pamoja na vitu hivyo.
21 Ndipo Daudi akafika kwa Sauli na kuanza kazi yake. Sauli alimpenda sana Daudi, na akawa mbeba silaha wake.
22 Sauli akawatuma wajumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi awe mbele yangu, maana amepata kibali machoni pangu.”
23 Wakati wowote roho ya usumbufu kutoka kwa Mungu ikiwapo juu ya Sauli, Daudi alichukuwa kinubi na kukipiga. Hivyo Sauli angeburudishwa na kupona, na huyo roho wa usumbufu angemtoka.