14
1 Siku moja, Yonathani mwana wa Sauli alimwambia mbeba silaha wake aliye mdogo, “Njoo, hebu twende hadi upande mwingine kwenye ngome ya Wafilisti.” Lakini hakumjulisha baba yake.
2 Sauli alikuwa akikaa nje ya mji wa Gibea chini ya mti wa mkomamanga ulio katika Migroni. Takribani watu mia sita walikwa pamoja naye,
3 akiwemo Ahiya mwana wa Ahitubu (nduguye Ikabodi) mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo, aliyevaa naivera. Watu hao hawakujua kwamba Yonathani ameondoka.
4 Katikati ya vichochoro, ambavyo Yonathani alinuia kuvipita hadi ngome ya Wafilisti, kulikuwa na mwamba wenye mteremko mkali upande mmoja, na mteremko mkali upande mwingine. Jabali moja liliitwa Bosesi, na jingine liliitwa Sene.
5 Lile jabali lenye mteremko mkali zaidi liliinuka upande wa kaskazini mbele ya Mikmashi, na jingine upande wa kusini mbele ya Geba.
6 Yonathani akamwambia kijana mbeba silaha, “Njoo, na tuvuke hadi ngome ya hawa wasiotahiriwa. Pengine BWANA atatenda kwa niaba yetu, kwa maana hakuna kitu kiwezacho kumzuia BWANA asiokoe kwa wengi au kwa watu wachache.”
7 Mbeba silaha wake akajibu, “Fanya kila kitu kilicho ndani ya moyo wako. Songa mbele, tazama, niko pamoja nawe, nitatii maagizo yako yote.”
8 Ndipo Yonathani akasema, “Tutavuka twende kwa watu hao, na tutajionesha wenyewe kwao.
9 Kama watatuambia, 'Subirini hapo hadi tutakapokuja kwenu' - basi tutabaki katika sehemu yetu na hatutavuka kwenda kwao.
10 Lakini kama watajibu, 'Njoni kwetu,' ndipo tutavuka; kwa sababu BWANA amewaweka mkononi mwetu. Hii ndiyo itakuwa ishara yetu.”
11 Kwa hiyo wote wawili wakajifunua mbele ya ngome ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Angalia, Webrania wanakuja kutokea kwenye mashimo walimojificha.”
12 Ndipo watu wa ile ngome wakamwita Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njoni huku kwetu, tutawaonesha jambo fulani.” Na Yonathani akamwambia mbeba silaha wake; “Nifuate nyuma yangu, kwa sababu BWANA amewaweka katika mkono wa Israeli.”
13 Yonathani alipanda juu kwa mikono na miguu yake, na mbeba silaha akimfuata nyuma yake. Wafilisti waliuwawa mbele ya Yonathani, na mbeba silaha wake akiwaua baadhi nyuma yake.
14 Hilo shambulio la kwanza walilofanya Yonathani na mbeba silaha wake, waliua watu wapatao ishirini katika urefu wa nusu handaki kwenye eka moja ya ardhi.
15 Kukawa na hofu kubwa katika kambi, uwandani, na katika watu. Hata ngome ya jeshi na watekaji nyara nao wakawa na hofu kubwa
16 Ndipo walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona kundi la askari wa Wafilisti likitawanyika, wakienda kule na huku.
17 Kisha Sauli akawaambia watu aliokuwa nao, “Mjihesabu ili muone nani hayupo hapa.”Walipokuwa wamehesabu, wakagundua kuwa Yonathani na mbebaji wa silaha zake hawapo.
18 Sauli akamwambia Ahiya, “Lete hapa naivera ya Mungu”- kwa maana siku hiyo Ahiya alivaa naivera akiwa pamoja na askari wa Israeli.
19 Wakati Sauli akiongea na kuhani, kelele na ghasia kubwa iliendelea na kuongezeka katika kambi ya Wafilisti. dipo sauli akamwambia kuhani, “Acha kazi unayofanya.”
20 Sauli na watu wote aliokuwa nao wakajipanga na kwenda kwenye mapigano. Upanga wa kila Mfilisti ulikwa juu ya Mfilisti mwenzake, na kulikuwa na ghasia kubwa.
21 Basi Waebrania ambao mwanzoni walijiunga na Wafilisti, na kwenda kwenye kambi yao, wao pia waliungana na Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani.
22 Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika milima karibu na Efraimu waliposikia kwamba Wafilisti wamekimbia, nao pia wakawafuata Wafilisti nakuwafukuza kwenye hiyo vita.
23 Hivyo siku hiyo BWANA aliwaokoa Israeli, na mapigano yalivuka kupitiliza Beth aveni.
24 Siku hiyo watu wa Israeli walifadhaika kwa sababu Sauli aliwaweka watu chini ya kiapo akasema, “Na alaaniwe mtu atakaye kula chakula kabla ya jioni na kabla sijalipiza kisasi kwa maadui zangu.” Hivyo hakuna hata mmoja kati ya watu wote aliyeonja chakula.
25 Ndipo watu wote wakaingia msituni na kuona asali ikiwa juu ya ardhi.
26 Watu walipoingia humo msituni, asali ilitiririka, lakini hakuna aliyeweka mkono wake kinywani kwa maana watu waliogopa kiapo.
27 Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kwamba baba yake amewaagiza watu kwa kiapo. Akanyoosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya kwenye sega la asali. Kisha akanyoosha mkono wake hadi kinywani mwake, na macho yake yakaangaziwa.
28 Ndipo mmoja wa watu hao, akamwambia, “Baba yako aliwaagiza watu kwa mkazo na kwa kiapo, kwa kusema, 'Alaaniwe mtu atakaye kula chakula kwa siku ya leo,' ingawa watu wamedhoofika kwa ajili ya njaa.”
29 Baadaye Yonathani alisema, “Baba yangu amefanya matatizo katika nchi. Angalia jinsi macho yangu alivyotiwa nuru kwa sababu nilionja asali hii kidogo.
30 Je, siyo vivuri sana kama leo watu wangekula bila kizuizi nyara walizopata kutoka kwa maadui zao? Kwa sababu sasa mauaji hayakuwa makubwa katikati ya Wafilisti.”
31 Siku hiyo waliwashambulia Wafilisti kutoka Mikmashi hadi Aiyaloni. Na watu walikuwa wamechoka sana.
32 Hivyo watu wakazivamia nyara na kuchukua kondoo, ng'ombe na ndama na kuwachinja hapo chini. Watu walikula nyama zao pamoja na damu.
33 KIsha wakamwambia Sauli, “Tazama, watu wanamtenda BWANA dhambi kwa kula pamoja na damu.” Sauli akasema, “Mmetenda isivyo haki. Sasa, viringisheni jiwe kubwa kwangu.” Sauli akasema,
34 “Nendeni kati watu, na muwaambie, 'Kila mtu alete ng'ombe na kondoo wake, wawachinje hapa, na kuwala. Msimtende BWANA dhambi kwa kula na damu.”' Kwa hiyo watu wote wakaleta kila mtu na ng'ombe wake usiku huo na kuwachinja mahali hapo.
35 Sauli akamjengea BWANA madhabahu, ambayo ilikuwa ya kwanza kwake kumjengea BWANA.
36 Ndipo Sauli akasema, “Haya tuwafukuze Wafilisti usiku na kuwateka nyara hadi asubuhi; tusimwache hata mtu mmoja akiwa hai.” Nao wakamjibu, “Fanya unaloona linakupendeza.” Lakini kuhani akasema, “Hebu na tumkaribie Mungu mahali hapa.”
37 Sauli alitaka kumuuliza Mungu maswali zaidi, “Je, inanipasa kuwafukuza Wafilisti? Je, utawaweka katika mkono wa Israeli?” Lakini siku hiyo BWANA hakumjibu kitu.
38 Ndipo Sauli akasema, “Njoni hapa, viongozi wote wa watu; mjue na kuona jinsi dhambi hii ilivyotokea leo.
39 Kwa maana, kama BWANA aishivyo, aliyewaokoa Israeli, hata kama angekuwa mwanangu Yonathani, atapaswa kufa.” Lakini hakuna hata mtu mmoja miongoni mwa watu aliye mjibu neno.
40 Basi akawaambia Waisraeli wote, “Simameni upande mmoja, na mimi na Yonathani tutasimama upande mwingine.” Kisha watu wakamwambia Sauli, “Fanya lile unaloona jema kwako.”
41 Kwa hiyo, Sauli akamwambia BWANA, Mungu wa Israeli, “Tuoneshe Thumimu.” Yonathani na Sauli wakatwaliwa, lakini watu walinusurika kuchaguliwa.
42 Basi Sauli akasema, “Tupa mawe ya bahati nasibu tuone kati yangu na mwanangu Yonathani.” Ndipo Yonathani akatwaliwa.
43 Kisha Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie umefanya nini.” Yonathani akamwambia baba yake, “Nilionja asali kidogo kwa kutumia ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwangu. Niko hapa; Nitakufa.”
44 Sauli akasema, “Mungu afanye hivyo na kuzidi hata kwangu, kama Yonathani hautakufa.”
45 Basi watu wakamuuliza Sauli, “Je, inampasa Sauli afe, ni nani aliyetekeleza ushindi huu mkubwa kwa ajili ya Israeli? Mbali na hayo! Kama BWANA aishivyo, hata unywele mmoja wa kichwa chake hautaanguka chini, kwa maana leo amefanya kazi pamoja na Mungu.” Hivyo hao watu walimuokoa Yonathani ili asife.
46 Basi Sauli akasita kuwafuatia Wafilisti, nao wakarudi katika makao yao.
47 Sauli alipoanza kutawala juu ya Israeli, alipigana na adui zake wote kila upande. Alipigana dhidi ya Moabu, dhidi ya watu wa Amoni, Edomu, wafalme wa Zoba, na Wafilisti. Popote alipogeukia aliwapiga kwa adhabu adui zake.
48 Alitenda kwa ushujaa mkubwa na kuwashinda Waamaleki. Aliwaokoa Israeli kutoka mikono ya watu ambao waliwateka nyara.
49 Basi wana wa Sauli walikuwa ni hawa Yonathani, Ishvi, na Malkishua. Na majina ya binti zake wawili yalikuwa ni haya, Merabu mzaliwa wa kwanza, na mdogo aliitwa Mikali.
50 Jina la mke wa Sauli aliitwa Ahinoamu; naye alikuwa binti Ahimaasi. Na jina la Jemedari wa jeshi lake aliitwa Abneri mwana wa Neri, baba mdogo wa Sauli.
51 Kishi alikuwa baba yake Sauli; na Neri alikuwa baba yake na Abneri, wote walikuwa wana wa Abieli.
52 Kulikuwa na mapigano makali dhidi ya Wafilisti katika siku zote za Sauli. Naye alipomwona mtu yeyote mwenye nguvu, au mtu yeyote jasiri, alimuunganisha kwake.