10
1 Ndipo Samweli akachukua chupa ya mafuta, akayamimina juu ya kichwa cha Sauli, na akambusu. Akasema, “Je, Mungu hajakutia mafuta uwe mtawala juu ya urithi wake?
2 Utakapoondoka kwangu leo, utawaona wanaume wawili na kaburi la Raheli, katika nchi ya Benyamini hapo Selsa. Watu hao watakuambia, 'Wale punda mliokuwa mkiwatafuta wamepatikana. Sasa, Baba yako ameacha kuwatunza punda, na ana hofu juu yenu, anasema, “Nitafanya nini kuhusu mwanangu?”
3 Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na utafika katika mwaloni wa Tabori. Utakutana na watu watatu hapo wakienda kwa Mungu huko Betheli, mmoja akibeba wana-mbuzi watatu, mwingine akibeba mikate mitatu, na mwingine akibeba kiriba cha divai.
4 Watawasalimu na watawapatia mikate miwili, kutoka mikononi mwao.
5 Baada ya hayo, utafika katika mlima wa Mungu, mahali ilipo ngome ya Wafilisti. Utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakiteremka chini kutoka mahali pa juu wakiwa na kinanda, tari, kinubi na filimbi mbele yao; na watakuwa wakitabiri.
6 Roho ya BWANA itakujaza, nawe utatabiri pamoja nao, na utabadilishwa na kuwa mtu tofauti.
7 Basi, ishara hizi zikikufikia, fanya lolote ambalo mikono yako itaona ifanye, kwa sababu Mungu yu pamoja nawe.
8 Nenda ushuke mbele yangu hadi Gilgali. Kisha nitakufuata huko nitoe dhabihu za kuteketezwa na kutoa dhabihu za amani. Nisubiri kwa muda wa siku saba hadi nije kwako na nikuoneshe unachopaswa kufanya.”
9 Sauli alipotega mgongo amuache Samweli, Mungu akampa moyo mwingine. Ndipo ishara zote hizi zikatimia siku hiyo.
10 Walipofika mlimani, kundi la manabii lilikutana naye, na Roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu ili atabiri pamoja nao.
11 Kila mtu aliyemfahamu kabla hajamwona akitabiri pamoja na manabii, watu waliambizana wao kwa wao,:”Kitu gani kimempata mtoto wa Kishi? Hivi Sauli ni mmoja wa manabii siku hizi?”
12 Mtu mmoja kutoka eneo hilo akajibu, “Na ni nani baba yao?” Kwa sababu ya jambo hili, ukawapo msemo, “Hivi Sauli naye ni mmoja wa manabii?”
13 Alipomaliza kutabiri, akafika mahali pa juu.
14 Ndipo baba yake mdogo na akamuuliza Sauli na mtumishi wake, “Mlienda wapi?” Naye akamjibu, “Kuwatafuta punnda; tulipoona kwamba hatuwezi kuwapata, tukaenda kwa Samweli.”
15 Baba yake mdogo akasema, “Tafadhali niambie kile alichosema kwako Samweli,”
16 Sauli akamjibu baba yake mdogo, “Alituambia waziwazi kwamba punda wamepatikana.” Lakini kuhusu swala la ufalme alilosema Samweli hakumwambia.
17 Basi Samweli aliwaita watu pamoja huko Mispa.
18 Akwaambia watu wa Israeli, “Hivi ndivyo BWANA, Mungu wa Israeli asemavyo: 'Niliwatoa Israeli kutoka Misri, na niliwaokoa kutoka nchi ya Wamisri, na kutoka mkono wa falme zote zilizowaonea.'
19 Lakini leo mmemkataa Mungu wenu, awaokoaye kutoka kwenye majanga na mahangaiko; na mmemwambia, ' Tuwekee mfalme juu yetu,; Sasa jihudhurisheni wenyewe mbele za BWANA kwa kabila na jamaa zenu.”
20 Kisha Samweli akawaleta kabila zote za Isareli karibu, na kulichagua kabila la Benyamini.
21 Akawasogeza karibu kabila la Benyamini kwa kufuata jamaa zao; na jamaa ya Wamatri ikachaguliwa; na Sauli mwana wa Kishi akachaguliwa. Lakini walipokwenda kumtafuta, hakuweza kuonekana.
22 Kisha watu walitaka kumuuliza Mungu maswali zaidi, “Bado yupo mtu mwingine ajaye?” BWANA akajibu, “ Yeye mwenyewe kajificha kwenye mizigo.”
23 Wakaenda mbio na kumleta Sauli kutoka humo. Aliposimama kati yao, alikuwa mrefu kuliko watu wote kuanzia mabega yake kwenda juu.
24 Kisha Samweli akawaambia watu, “Je, mnamuona mtu ambaye BWANA amemchagua? Hakuna mtu kama yeye kati ya watu wote.” Watu wote wakapiga Kelele, “Mfalme na aishi”
25 Ndipo Samweli akawaambia watu desturi na sheria za ufalme, akaziandika katika kitabu, na kuziweke mbele za BWANA. Baadaye Samweli akawaruhusu watu waondoke kila mtu aende nyumbani kwake.
26 Sauli pia alienda nyumbani kwake huko Gibea, akiwa na baadhi ya watu wenye nguvu, wenye mioyo iliyoguswa na Mungu.
27 Lakini baadhi ya watu wasiofaa walisema, “Huyu mtu atatuokoaje?” Watu hawa walimdharau Sauli na hawakumletea zawadi zozote. Lakini Sauli alinyamaza kimya.