9
Kisha malaika wa tano alipiga tarumbeta yake. Niliona nyota kutoka mbinguni iliyokuwa imeanguka kwenye dunia. Nyota ilipewa ufunguo wa shimo linaloelekea kwenye shimo lisilo na mwisho. Alifungua shimo lisilo na kikomo, na moshi ukapanda juu kwa safu kutoka ndani ya shimo kama moshi kutoka katika tanuru kubwa. Jua na anga vilibadilika vikawa giza kwa sababu ya moshi uliotoka shimoni. Ndani ya moshi nzige walitoka kuja juu ya dunia, nao walipewa nguvu kama ile ya nge juu ya dunia. Waliambiwa kutokudhuru majani katika nchi au mmea wowote wa kijani au mti, isipokuwa tu watu ambao hawakuwa na muhuri wa Mungu katika paji za nyuso zao. Hawakupewa ruhusa ya kuwaua hao watu, bali kuwatesa tu kwa miezi mitano. Uchungu wao ulikuwa kama ule wa kuumwa na nge amwumapo mtu. Katika siku hizo watu watatafuta kifo, lakini hawatakipata. Watatamani kufa, lakini kifo kitawakimbia. Nzige walifanana na farasi walioandaliwa kwa vita. Kwenye vichwa vyao kulikuwa na kitu kama taji ya dhahabu na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu. Walikuwa na nywele kama za wanawake na meno yao yalikuwa kama ya simba. Walikuwa na vifua kama vifua vya chuma na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya magari mengi ya vita na farasi wakimbiao kwenda vitani. 10 Walikuwa na mikia inayouma kama nge; katika mikia yao walikuwa na nguvu ya kudhuru watu kwa miezi mitano. 11 Walikuwa naye kama mfalme juu yao malaika wa shimo lisilokuwa na mwisho. Jina lake katika Kiebrania ni Abadoni, na katika Kiyunani ana jina Apolioni. 12 Ole ya kwanza imepita. Angalia! Baada ya hili kuna maafa mawili yaja. 13 Malaika wa sita alipiga tarumbeta yake, na nikasikia sauti ikitoka katika pembe ya madhabahu ya dhahabu ambayo iko mbele za Mungu. 14 Sauti ilimwambia malaika wa sita aliyekuwa na tarumbeta, “Waachie malaika wanne ambao wamefungwa katika mto mkubwa Efrata.” 15 Malaika wale wanne waliokuwa wameandaliwa kwa saa hiyo maalumu, siku hiyo, mwezi huo, na mwaka huo, waliachiwa wawaue theluthi ya wanadamu. 16 Idadi ya maaskari waliokuwa juu ya farasi ilikuwa 200, 000, 000. Nilisikia idadi yao. 17 Hivi ndivyo nilivyoona farasi katika maono yangu na wale waliopanda juu yao: Vifua vyao vilikuwa vyekundu kama moto, bluu iliyoiva na njano isiyoiva. Vichwa vya farasi vilifanana na vichwa vya simba, na midomoni mwao ulitoka moto, moshi na salfa. 18 Theluthi ya wanadamu waliuawa na haya mapigo matatu: moto, moshi, na salfa iliyotoka katika midomo yao. 19 Kwa kuwa nguvu ya farasi ilikuwa katika midomo yao na katika mikia yao—kwa kuwa mikia yao ilikuwa kama nyoka, na walikuwa na vichwa ambavyo walitumia kuwatia majeraha wanadamu. 20 Watu waliobaki, wale ambao walikuwa hawajauawa na mapigo haya, hawakutubia matendo yao waliyokuwa wamefanya, wala hawakuacha kuabudu mapepo na miungu ya dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti—vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia au kutembea. 21 Wala hawakutubia uuaji wao, uchawi wao, uasherati wao au njia zao za wizi.