7
Baada ya haya niliona malaika wanne wamesimama kwenye kona nne za dunia, wamezuia pepo nne za nchi kwa nguvu ili kwamba pasiwe na upepo unaovuma katika nchi, juu ya bahari au dhidi ya mti wowote. Nikaona malaika mwingine akija kutoka mashariki, aliyekuwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Akalia kwa sauti kuu kwa malaika wanne ambao walipewa ruhusa ya kudhuru nchi na bahari: “Msiidhuru nchi, bahari, au miti mpaka tutakapokuwa tumekwishaweka muhuri katika paji za vichwa vya watumishi wa Mungu wetu.” Nikasikia idadi ya wale waliotiwa muhuri: 144, 000, ambao walitiwa muhuri kutoka kila kabila ya watu wa Israel: 12, 000 kutoka katika kabila ya Yuda walitiwa muhuri, 12, 000 kutoka katika kabila ya Rubeni, 12, 000 kutoka katika kabila ya Gadi. 12, 000 kutoka katika kabila ya Asheri, 12, 000 kutoka katika kabila ya Naftali, 12, 000 kutoka katika kabila ya Manase. 12, 000 kutoka kabila ya Simioni, 12, 000 kutoka kabila ya Lawi, 12, 000 kutoka kabila ya Isakari, 12, 000 kutoka kabila ya Zebuloni, 12, 000 kutoka kabila ya Yusufu, na 12, 000 kutoka kabila ya Benyamini walitiwa muhuri. Baada ya mambo haya nilitazama, na kulikuwa na umati mkubwa ambao hapana mtu angeweza kuuhesabu - kutoka kila taifa, kabila, jamaa, na lugha - wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo. Walikuwa wamevaa kanzu nyeupe na wana matawi ya mitende mikononi mwao, 10 na walikuwa wakiita kwa sauti ya juu: “Wokovu ni kwa Mungu ambaye ameketi katika kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo!” 11 Malaika wote waliokuwa wamesimama kuzunguka kiti cha enzi na kuwazunguka wale wazee pamoja na wenye uhai wanne, wakainama chini ardhini na wakaweka nyuso zao juu ya ardhi mbele ya kiti cha enzi na wakamwabudu Mungu, 12 wakisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukurani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu milele na milele! Amina!” 13 Kisha mmoja wa wale wazee akaniuliza, “hawa ni akina nani waliovaa kanzu nyeupe, na wametoka wapi? 14 Nikamwambia, “Bwana mkubwa, unajua wewe,” na akaniambia, “Hawa ni wale waliotoka katika dhiki kuu. Wamezifua kanzu zao na kuzifanya nyeupe kwa damu ya Mwanakondoo. 15 Kwa sababu hii, wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, na wanamwabudu yeye usiku na mchana katika hekalu lake. Yeye aliye keti juu ya kiti cha enzi atasambaza hema yake juu yao. 16 Hawataona njaa tena, wala kiu tena. Jua halitawachoma, wala joto la kuunguza. 17 Kwa kuwa Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, na atawaongoza katika chemchemi ya maji ya uzima, na Mungu atafuta kila chozi katika macho yao.”