2
“Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika: 'Haya ni maneno ya yule anayeshikilia zile nyota saba katika mkono wake wa kuume. Yeye atembeaye kati ya vinara vya dhahabu vya taa saba asema hivi, “ '“Najua ambacho umetenda na bidii yako ya kazi na uvumilivu wako thabiti, na kwamba huwezi kuhusiana nao walio waovu, na umewajaribu wote wanaojiita kuwa mitume na kumbe siyo, na wameonekana kuwa waongo. Najua una subira na uvumilivu, na umepitia mengi kwa sababu ya jina langu, na haujachoka bado. Lakini hili ndilo nililonalo dhidi yako, umeuacha upendo wako wa kwanza. Kwa hiyo kumbuka ulipoanguka, ukatubu na kufanya matendo uliyofanya tangu mwanzo. Usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako kutoka mahali pake. Lakini wewe una hili, unachukia yale ambayo Wanikolai wameyatenda, ambayo hata mimi nayachukia. Kama una sikio, sikiliza yale ambayo Roho anayaambia makanisa. Na kwa yeye ashindaye nitampa kibali cha kula kutoka katika mti wa uzima ulio katika paradiso ya Mungu.' “Kwa malaika wa kanisa la Smirna andika: 'Haya ni maneno ya yule ambaye ni mwanzo na mwisho ambaye alikufa na kuwa hai tena: '“Nayajua mateso yako na umasikini wako (lakini wewe ni tajiri), na uongo wa wale wanaojiita ni wayahudi (lakini siyo - wao ni sinagogi la Shetani). 10 Usiogope mateso yatakayokupata. Tazama! Ibilisi anataka kuwatupa baadhi yenu gerezani ili mpate kujaribiwa, na mtateseka kwa siku kumi. Iweni waaminifu hadi kufa, na nitawapa taji ya uzima. 11 Kama una sikio, sikiliza Roho anavyoyaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapata madhara ya mauti ya pili.' 12 “Kwa malaika wa kanisa la Pergamo andika: 'Haya ndiyo anenayo yeye aliye nao huo upanga mkali, wenye makali kuwili. 13 '“Najua mahali unapoishi -mahali kilipo kiti cha enzi cha shetani. Hata hivyo wewe walishika sana jina langu, na hukuikana imani yako iliyo kwangu, hata siku zile za Antipasi shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa miongoni mwenu, hapo ndipo Shetani anaishi. 14 Lakini nina mambo machache dhidi yako: unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki kuweka vikwazo mbele ya wana wa Israel, ili wale vyakula vilivyotolewa sadaka kwa miungu na kuzini. 15 Katika hali iyo hiyo, hata wewe unao baadhi yao wanaoshika mafundisho ya Wanikolai. 16 Basi tubu! Na usipofanya hivyo, naja upesi, na nitafanya vita dhidi yao kwa upanga utokao katika kinywa changu. 17 Kama una sikio, sikiliza Roho anachowaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, pia nitampa jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya juu ya jiwe, jina ambalo hakuna alijuaye isipokuwa yeye alipokeaye.' 18 “Kwa malaika wa kanisa la Thiatira andika: “Haya ndiyo maneno ya Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na nyayo kama shaba iliyosuguliwa sana: 19 '“Najua ambacho umefanya - upendo wako na imani na huduma na uvumilivu wako thabiti, na kwamba kile ulichofanya hivi karibuni ni zaidi ya kile ulichofanya mwanzo. 20 Lakini ninalo hili dhidi yako: unamvumilia mwanamke Yezebeli anayejiita mwenyewe nabii mke. Kwa mafundisho yake, anawapotosha watumishi wangu kuzini na kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu. 21 Nilimpa muda wa kutubu, lakini hayuko tayari kuutubia uovu wake. 22 Angalia! Nitamtupa kwenye kitanda cha maradhi, na wale watendao uasherati naye kwenye mateso makali, vinginevyo watubu kwa alichofanya. 23 Nitawapiga wanawe wafe na makanisa yote watajua kwamba mimi ndiye niyachunguzaye mawazo na tamaa. Nitampa kila mmoja wenu kadiri ya matendo yake. 24 Lakini kwa baadhi yenu mliosalia katika Thiatira, kwa wale wote msioshika fundisho hili, na msiojua kile ambacho baadhi huita mafumbo ya Shetani, nasema kwenu, 'sitaweka juu yenu mzigo wowote.' 25 Kwa jambo lolote, lazima muwe imara mpaka nitakapokuja. 26 Yeyote ashindaye na kufanya kile nilichofanya hadi mwisho, kwake yeye nitampa mamlaka juu ya mataifa. 27 'Atawatawala kwa fimbo ya chuma, kama mabakuli ya udongo, atawavunja vipande vipande.' 28 Kama nilivyopokea kutoka kwa Baba yangu, nitampa pia nyota ya asubuhi. 29 Ukiwa na sikio, sikiliza kile ambacho Roho anayaambia makanisa.'