19
Baada ya mambo haya nilisikia sauti kama ya mlio mkubwa wa kundi kubwa la watu mbinguni ikisema, “Haleluya. Wokovu, utukufu, na nguvu ni vya Mungu wetu. Hukumu zake ni kweli na za haki, kwa kuwa amemhukumu kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uzinzi wake. Amefanya kisasi kwa damu ya watumishi wake, ambayo aliimwaga yeye mwenyewe.” Kwa mara ya pili walisema, “Haleluya! Moshi hutoka kwake milele na milele.” Wale wazee ishirini na wanne na viumbe hai wanne wakasujudu na kumwabudu Mungu akaaye kwenye kiti cha enzi. Walikuwa wakisema, “Amina. Haleluya!” Ndipo sauti ilitoka kwenye kiti cha enzi, ikisema, “Msifuni Mungu wetu, enyi watumishi wake wote, ninyi mnaomcha yeye, wote wasio na umuhimu na wenye nguvu.” Ndipo nilisikia sauti kama sauti ya kundi kubwa la watu, kama sauti ya ngurumo ya maji mengi, na kama ngurumo ya radi, ikisema, “Haleluya! Bwana ni Mungu wetu, mtawala juu ya wote, hutawala. Na tushangilie na kufurahi na kumpa utukufu kwa sababu harusi na sherehe ya Mwana Kondoo imekuja, na bibi harusi yuko tayari.” Aliruhusiwa kuvalishwa kitani safi na yenye kung'aa (kitani safi ni matendo ya haki ya waumini). Malaika akasema nami, “Yaandike haya: Wamebarikiwa walioalikwa kwenye sherehe ya harusi ya Mwana kondoo.” Vilevile akaniambia, “Haya ni maneno ya kweli ya Mungu.” 10 Nilisujudu mbele ya miguu yake nikamwabudu, lakini akaniambia, “Usifanye hivi! Mimi ni mtumishi mwenzako na wa ndugu zako mwenye kuushika ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu, kwa kuwa ushuhuda wa Yesu ni roho ya unabii.” 11 Kisha niliona mbingu zimefunguka, na tazama kulikuwa na farasi mweupe! Na yule aliyekuwa amempanda anaitwa Mwaminifu na wa Kweli. Huhukumu kwa haki na kufanya vita. 12 Macho yake ni kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake ana taji nyingi. Ana jina lililoandikwa juu yake asilolifahamu mtu yeyote isipokuwa yeye mwenyewe. 13 Amevaa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aliitwa Neno la Mungu. 14 Majeshi ya mbinguni yalikuwa yakimfuata juu ya farasi weupe, walivalishwa kitani nzuri, nyeupe na safi. 15 Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao huyaangamiza mataifa, naye atawatawala kwa fimbo ya chuma. Naye hukanyaga vyombo vya mvinyo kwa hasira kali ya Mungu, hutawala juu ya wote. 16 Naye ameandikwa juu ya vazi lake na katika paja lake jina, MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA. 17 Niliona malaika amesimama katika jua. Aliwaita kwa sauti kuu ndege wote warukao juu, “Njoni, kusanyikeni pamoja kwenye chakula kikuu cha Mungu. 18 Njoni mle nyama ya wafalme, nyama ya majemedari, nyama ya watu wakubwa, nyama ya farasi na wapanda farasi, na nyama ya watu wote, walio huru na watumwa, wasio na umuhimu na wenye nguvu.” 19 Nilimwona mnyama na wafalme wa nchi pamoja na majeshi yao. Walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kufanya vita na mmoja aliyepanda farasi na jeshi lake. 20 Mnyama alikamatwa na nabii wake wa uongo aliyezifanya ishara katika uwepo wake. Kwa ishara hizi aliwadanganya wale walioipokea chapa ya mnyama na walioisujudia sanamu yake. Wote wawili walitupwa wangali hai katika ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti. 21 Wale waliobaki waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa mmoja aliyepanda juu ya farasi. Ndege wote walikula mizoga ya miili yao.