4
1 Tutasema nini tena kwamba Abrahamu, baba yetu kwa jinsi ya mwili, amepatikana?
2 Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, angekuwa na sababu ya kujisifu, lakini si mbele za Mungu.
3 Kwani maandiko yanasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”
4 Sasa kwa mtu afanyaye kazi, malipo yake hayahesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni.
5 Lakini kwa mtu asiyefanya kazi bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtaua, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki.
6 Daudi pia hunena baraka juu ya mtu ambaye Mungu amhesabia haki pasipo matendo.
7 Alisema, “Wamebarikiwa wale ambao maovu yao yamesamehewa na ambao dhambi zao zimefunikwa.
8 Amebarikiwa mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.”
9 Basi je baraka hizi ni kwa wale waliotahiriwa tu, au pia kwa wale wasiotahiriwa? Kwa maana twasema, “kwa Abrahamu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki.”
10 Hivyo ilihesabiwaje basi? Wakati Abrahamu alikuwa katika tohara, au kabla hajatahiriwa? Haikuwa katika kutahiriwa, bali katika kutotahiriwa.
11 Abrahamu alipokea alama ya kutahiriwa. Huu ulikuwa muhuri wa ile haki ya imani aliyokuwa nayo tayari kabla hajatahiriwa. Matokeo ya ishara hii ni kwamba alifanyika kuwa baba wa wote waaminio, hata kama wapo katika kutotahiriwa. Hii ina maana kwamba haki itahesabiwa kwao.
12 Hii pia ilimaanisha kuwa Abrahamu alifanyika baba wa tohara si tu kwa wale wanaotokana na tohara, bali pia wale wanaozifuata nyayo za baba yetu Abrahamu. Na hii ndiyo imani aliyokuwa nayo kwa wasiotahiriwa.
13 Kwa maana haikuwa kwa sheria kwamba ahadi ilitolewa kwa Abrahamu na uzao wake, ahadi hii ya kwamba watakuwa warithi wa dunia. isipokuwa, ilikuwa kupitia haki ya imani.
14 Kwa maana kama wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika.
15 Kwa sababu sheria huleta ghadhabu, lakini pale ambapo hakuna sheria, pia hakuna kutotii.
16 Kwa sababu hii hili hutokea kwa imani, ili iwe kwa neema. Matokeo yake, ahadi ni dhahiri kwa uzao wote. Na wazawa hawa si tu wale wanaojua sheria, bali pia wale ambao ni wa imani ya Abrahamu. Kwa maana yeye ni baba yetu sisi sote,
17 kama ilivyoandikwa, “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Abrahamu alikuwa katika uwepo wa yule aliyemwamini, yaani, Mungu ambaye huwapa wafu uzima na kuyaita mambo ambayo hayapo ili yaweze kuwepo.
18 Licha ya hali zote za nje, Abrahamu kwa ujasiri alimuamini Mungu kwa siku zijazo. Hivyo akawa baba wa mataifa mengi, kulingana na kile kilichonenwa,”... Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”
19 Yeye hakuwa dhaifu katika imani. Abrahamu alikiri kwamba mwili wake mwenyewe ulikwisha kufa - alikuwa na umri wa karibu miaka mia moja. Pia alikubaliana na hali ya kufa ya tumbo la Sara.
20 Lakini kwa sababu ya ahadi ya Mungu, Abrahamu hakusita katika kutokuamini. Bali, alitiwa nguvu katika imani na alimsifu Mungu.
21 Alikuwa akijua hakika ya kuwa kile ambacho Mungu ameahidi, alikuwa pia na uwezo wa kukikamilisha.
22 Kwa hiyo hii pia ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.
23 Sasa haikuandikwa tu kwa faida yake, kwamba ilihesabiwa kwake.
24 Iliandikwa kwa ajili yetu pia, kwa waliowekewa kuhesabiwa, sisi ambao tunaamini katika yeye aliyemfufua Bwana wetu Yesu kutoka wafu.
25 Huyu ni yule ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu na kufufuliwa ili tupate kuhesabiwa haki.