54
Kwa kiongozi wa muziki; kwenye vyombo vya nyuzi. Maschil ya Daudi; wakati Ziphites alipokuja na kumwambia Sauli, “Hivi Daudi hakujificha pamoja nasi?”
1 Uniokoe, Mungu, kwa jina lako, na kwa nguvu zako unihukumu.
2 Usikie maombi yangu, Mungu; uyategee sikio maneno ya mdomo wangu.
3 Kwa maana wageni wameinuka dhidi yangu, na watu wasio na huruma wanaitafuta roho yangu; nao hawakumuweka Mungu mbele yao. Selah
4 Tazama, Mungu ni msaidizi wangu; Bwana ndiye anisaidiaye.
5 Naye atawalipizia uovu maadui zangu; katika uaminifu wako, uwaharibu!
6 Nitakutolea dhabihu kwa moyo mkunjufu; nitalishukuru jina lako, Yahwe, kwa maana ni jema.
7 Kwa kuwa yeye ameniokoa katika kila shida; macho yangu yamewatazama adui zangu yakiwa na ushindi.