36
Kwa kiongozi wa muziki. Zaburi ya Daudi ya mtumishi wa Yahwe.
1 Dhambi hunena kama unabii katika moyo wa mwovu; machoni mwake hamna hofu ya Mungu.
2 Kwa maana yeye hujifariji mwenyewe, akifikiria kuwa dhambi zake hazitagundulika na kuchukiwa.
3 Maneno yake ni yenye dhambi na udanganyifu; hataki kuwa mwenye hekima na kutenda mema.
4 Alalapo kitandani, hupanga namna ya kutenda dhambi; yeye hukaa nje kwenye nja ya uovu; yeye hakatai uovu.
5 Uaminifu wa agano lako, Yahwe, unafika mbinguni; uaminifu wako unafika mawinguni.
6 Haki yako ni kama milima ya Mungu; hukumu yako ni kama kina kirefu. Yahwe, wewe huwahifadhi wote wanadamu na wanyama.
7 Ni jinsi gani uaminifu wa aganao lako ni wa thamani, Mungu! Watu hukimbilia usalama chini ya uvuli wa mbawa zako.
8 Nao watatoshelezwa tele na utajiri wa chakula nyumbani mwako; utawafanya wanywe kutoka katika mto wa baraka zako za thamani.
9 Kwa kuwa mna chemichemi ya uzima; na katika mwanga wako tutaiona nuru.
10 Uupanue uaminifu wa agano lako kikamilifu kwa wale wanao kujua wewe, ulinzi wako uwe juu ya wanyoofu wa moyo.
11 Usiuache mguu wa mwenye kiburi unisogelee. Usiiache mkono wa mwovu unitoweshe.
12 Kule wafanyao maovu wameanguka; wameharibiwa hawawezi kuinuka.