103
Zaburi ya Daudi.
1 Nitamsifu Yahwe maisha yangu yote, na vyote vilivyomo ndani yangu, nitalisifu jina lake takatifu.
2 Maishani mwangu mwote nitamsifu Yahwe, na kukumbuka matendo yake yote mazuri.
3 Yeye husamehe dhambi zako zote; huponya magonjwa yako yote.
4 Huukomboa uhai wako dhidi ya uharubifu; hukuvika taji kwa uaminifu wa agano lake na hutenda kwa rehema.
5 Huyatosheleza maisha yako kwa mambo mema ili kwamba ujana wako ufanywe upya kama tai.
6 Yahwe hutenda yaliyo haki naye hutenda hukumu ya haki kwa ajili ya wote walio onewa.
7 Alimjulisha Musa njia zake, matendo yake kwa uzao wa Israeli.
8 Yahwe ni wa huruma na neema; ni mvumilivu; ana agano kuu la uaminifu.
9 Hataadhibu siku zote; hakasiriki siku zote.
10 Hatushughulikii sisi kama dhambi zetu zinavyostahili au kutulipa kulingana na uhitaji wa dhambi zetu.
11 Kama mbingu zilivyo juu zaidi ya nchi, ndivyo ulivyo ukuu wa uaminifu wa agano lake kwao wale wanaomcha yeye.
12 Kama vile mashariki ilivyo mbali na magharibi, hivi ndivyo ameondoa hatia zetu za dhambi zetu mbali nasi.
13 Kama vile baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo Yahwe alivyo na huruma kwao wamchao.
14 Maana anajua tulivyo umbwa; anajua kuwa tu mavumbi.
15 Kama ilivyo kwa mwanadamu, siku zake ni kama majani; hustawi kama ua katika shamba.
16 Upepo hulipiga, nalo hutoweka, na hakuna hata mmoja awezaye kuelezea mahali lilipokua.
17 Lakini agano la uaminifu wa Yahwe uko kwa wale wamchao yeye milele hata milele. Haki yake ni endelevu kwa uzao wao.
18 Wanashika agano lake na kukumbuka kutii maagizo yake.
19 Yahwe ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, na ufalme wake watawala juu ya kila mtu.
20 Msifuni Yahwe, enyi malaika zake, ninyi hodari wenye nguvu na mtendao neno lake, na kutii sauti ya neno lake.
21 Msifuni Yahwe, enyi jeshi la malaika wote, ninyi ni watumishi mfanyao mapenzi yake.
22 Msifuni Yahwe, viumbe wake wote, mahali popote atawalapo. Nitamsifu Yahwe maisha yangu yote.