24
Yesu alitoka hekaluni na kwenda zake. Wanafunzi wake walimwendea na kumuonesha majengo ya hekalu. Laikni aliwajibu na kuwaambia, “Je, hamuyaoni mambo haya yote? Kweli nawaambia, hakuna jiwe litalobaki juu ya lingine bila kubomolewa.” Na alipokaa katika Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake walimwendea kwa faragha na kusema, “Tuambie, mambo haya yatatokea lini? Kitu gani kitakuwa dalili ya kuja kwako na mwisho wa ulimwengu?” Yesu aliwajibu na kuwaambia, “Iweni makini kwamba asije mtu akawapotosha. Kwa kuwa wengi watakuja kwa jina langu. Watasema, 'Mimi ndiye Kristo', na watawapotosha wengi. Mtasikia vita na taarifa za vita. Angalieni msije mkawa na wasiwasi, kwa kuwa mambo haya hayabudi kutokea; lakini ule mwisho utakuwa bado. Kwa kuwa taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na matetemeko ya ardhi katika sehemu mbalimbali. Lakini mambo haya yote ni mwanzo tu wa uchungu wa kujifungua. Ndipo watawatoa kwa ajili ya mateso na kuwaua. Mtachukiwa na mataifa yote kwa sababu ya jina langu. 10 Ndipo wengi watajikwaa na kusalitiana na watachukiana wenyewe kwa wenyewe. 11 Manabii wengi wa uongo watatokea na kuwadanganya wengi. 12 Kwa sababu uovu utaongezeka, upendo wa wengi utapoa. 13 Lakini atakaye vumilia mpaka mwisho, ataokolewa. 14 Hii Injili ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu mzima kama ushuhuda kwa mataifa yote. Na ndipo ule mwisho utafika. 15 Kwa hiyo, mtakapoona chukizo la uharibifu, lililosemwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu [asomaye na afahamu], 16 ndipo walioko Yuda wakimbilie milimani. 17 Na yule aliyeko juu ya paa la nyumba asiweze kuteremka chini kuchukua kitu chochote kutoka ndani ya nyumba yake, 18 naye aliyeko shambani asirudi kuchukua vazi lake. 19 Lakini ole wao ambao wana mtoto na wale ambao wananyonyesha katika siku hizo! 20 Ombeni kwamba kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. 21 Kwa kuwa kutakuwa na dhiki kuu, ambayo haijawahi kuwapo tangu kuumbwa kwa ulimwengu hadi sasa, na wala haitakuwapo tena. 22 Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna ambaye angeokoka. Lakini kwa sababu ya wateule, siku hizo zitafupishwa. 23 Kisha ikiwa mtu yeyote atawaambia 'Tazama, Kristo yuko hapa! au, 'Kristo yuko kule' msiamini maneno hayo. 24 Kwa kuwa Makristo wa uongo na manabii wa uongo watakuja na kuonesha ishara kubwa na maajabu, kwa kusudi la kupotosha, kama ingewezekana hata na wateule. 25 Tazameni, nimewatahadharisha kabla ya mambo hayo kutokea. 26 Kwa hiyo, ikiwa watawaambia, ''Kristo yuko jangwani,' msiende huko jangwani. Au, 'Tazameni, yuko ndani ya nyumba,' msiamini maneno hayo. 27 Kama vile radi inavyomulika kutokea mashariki na kuangaza hadi magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwa Mwana wa Adamu. 28 Popote ulipo mzoga, huko ndiko tai wakusanyikapo. 29 Lakini mara baada ya dhiki kuu ya siku zile, Jua litatiwa giza, mwezi hautatoa mwanga wake, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbinguni zitatikisika. 30 Ndipo ishara ya Mwana wa Adamu itaonekana angani, na makabila yote ya dunia wataomboleza. Watamwona Mwana wa Adamu akija katika mawingu ya angani kwa nguvu na utukufu mkuu. 31 Atawatuma malaika wake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya pamoja wateule wake kutoka pande nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine. 32 Jifunzeni somo kutokana na mti mtini. Mara tu tawi linapochipuka na kutoa majani, mnajua kwamba kiangazi kinakaribia. 33 Hivyo pia, mtakapoona mambo haya yote, mnapaswa kujua kwamba amekaribia, karibu na malango. 34 Kweli nawaambia, kizazi hiki hakitapita, hadi mambo yote haya yatakuwa yametokea. 35 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. 36 Lakini kuhusu siku ile na saa hakuna mtu ajuaye, hata malaika wa mbinguni, wala Mwana, bali Baba peke yake. 37 Kama vile ilivyokuwa katika siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa kuja kwa Mwana wa Adamu. 38 Kwa kuwa katika siku hizo kabla ya gharika watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa hadi siku ile ambayo Nuhu aliingia katika safina, 39 na hawakujua kitu chochote hadi gharika ilipokuja na kuwasomba wote - ndivyo itakavyokuwa kuja kwa Mwana wa Adamu. 40 Ndipo watu wawili watakuwa shambani- mmoja atachukuliwa, na mmoja ataachwa nyuma. 41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja - mmoja atachukuliwa, na mmoja atabaki. 42 Kwa hiyo, kuweni macho kwa sababu hamjui ni siku gani ambayo atakuja Bwana wenu. 43 Lakini mjue kwamba, ikiwa bwana mwenye nyumba angejua ni saa ipi ambayo mwizi angekuja, angekesha na asingeruhusu nyumba yake kuvamiwa. 44 Kwa hiyo, pia mnapaswa kuwa tayari, kwa kuwa Mwana wa Adamu atakuja katika saa msiyoitarajia. 45 Hivyo ni nani aliye mwaminifu, mtumwa mwenye akili, ambaye bwana wake amempa madaraka juu ya walio katika nyumba yake, ili awape chakula kwa wakati unaofaa? 46 Amebarikiwa mtumishi huyo, ambaye bwana wake atamkuta akifanya hivyo wakati ajapo. 47 Kweli nawaambia kwamba bwana atamweka juu ya kila kitu kilicho chake. 48 Lakini kama mtumwa mwovu akisema moyoni mwake, 'Bwana wangu amekawia,' 49 na akaanza kuwapiga watumishi wake, na akala na kulewa vileo, 50 Bwana wa mtumwa huyo atakuja katika siku ambayo haitarajii, na katika saa ambayo haijui. 51 Bwana wake atamkata vipande viwili na kumweka katika nafasi moja sawa na wanafiki, ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.