22
Yesu alisema nao tena katika mifano, akisema, “Ufalme wa mbinguni unafanana na mfalme aliyeandaa sherehe ya harusi ya mwanawe. Akawatuma watumishi wake kuwakaribisha waliokuwa wamealikwa kuja katika sherehe ya harusi, lakini hawakufika. Mfalme aliwatuma tena watumishi wengine, akisema. “Waambieni wote walioalikwa, Angalieni, nimeandaa chakula. Fahali na ndama wangu wanono wamechinjwa, na mambo yote yako tayari, Njoni katika sherehe ya harusi.” Lakini watu hao hawakuzingatia kwa dhati mwaliko wake. Baadhi walirejea katika mashamba yao, na wengine walirudi katika sehemu zao za biashara. Wengine waliwainukia watumishi wa mfalme na kuwadharirisha na kuwaua. Lakini mfalme alikasirika. Alituma jeshi lake, akawaua wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto. Kisha aliwaambia watumishi wake, “Harusi iko tayari, lakini walioalikwa hawakustahili. Kwa hiyo nendeni kwenye makutano ya njia kuu, waalikeni watu wengi kadri iwezekanavyo waje kwenye sherehe ya harusi.” 10 Watumishi walienda njia kuu na kuwakaribisha watu wowote waliowaona, wema na wabaya. Hivyo ukumbi wa harusi ulijaa wageni. 11 Lakini mfalme alipoingia kuwatazama wageni, alimuona mtu mmoja ambaye hakuvaa vazi rasmi la harusi! 12 Mfalme alimwuliza, 'Rafiki, ulipataje kufika hapa ndani bila vazi la harusi?' Na mtu huyo hakujibu chochote. 13 Ndipo mfalme alipowaambia watumishi wake, “Mfungeni mtu huyu mikono na miguu na mtupeni nje katika giza, huko ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 14 Kwa kuwa watu wengi wanaitwa, lakini wateule ni wachache.” 15 Ndipo Mafarisayo waliondoka na kupanga jinsi ya kumkamata Yesu katika maneno yake mwenyewe. 16 Ndipo walipowatuma wanafunzi wao pamoja na Maherode. Na walimwambia Yesu, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mtu wa kweli, na kwamba unafundisha matakwa ya Mungu katika ukweli. Haujali maoni ya mtu mwingine na hauoneshi upendeleo kwa watu. 17 Kwa hiyo tuambie, unafikiri nini? Je, ni sahihi kisheria kulipa kodi kwa Kaisari au hapana?” 18 Yesu alifahamu uovu wao na akasema, “Kwa nini mnanijaribu, enyi wanafiki? 19 Nionesheni pesa itumikayo kulipia kodi.” Ndipo wakamletea dinari. 20 Yesu akawauliza, “Sura na jina hili ni vya nani?” 21 Wakamjibu, “Vya Kaisari.” Ndipo Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari vitu vilivyo vyake na vya Mungu mpeni Mungu.” 22 Waliposikia hivyo walishangaa. Kisha walimwacha na kwenda zao. 23 Siku hiyo baadhi ya Masadukayo walikuja kwa Yesu, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu. Wakamwuliza, 24 wakisema, “Mwalimu, Musa alisema, Ikiwa mtu amefariki bila kuzaa watoto, ndugu yake na amrithi huyo mwanamke na ampatie mtoto kwa ajili ya ndugu yake. 25 Walikuwapo ndugu saba. Wa kwanza alioa na kisha akafariki bila kuzaa watoto. Akamwachia mke nduguye. 26 Kisha ndugu yake wa pili naye akafanya vivyo hivyo, kisha yule wa tatu, ikawa hivyo hadi kwa yule wa saba. 27 Baada ya kufanya hivyo wote, yule mwanamke naye alifariki. 28 Sasa katika ufufuo huyo mwanamke atakuwa mke wa nani katika ndugu hao saba? Kwa sababu wote walimuoa.” 29 Lakina Yesu aliwajibu na kuwaambia, “Mnakosea, kwa sababu hamjui Maandiko wala nguvu za Mungu. 30 Kwa kuwa katika ufufuo, watu hawaoi wala kuolewa. Badala yake watu huwa kama malaika huko mbinguni. 31 Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjawahi kusoma kile ambacho Mungu alikisema kwenu, akisema, 32 Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” 33 Wakati kusanyiko waliposikia hili, waliyashangaa mafundisho yake. 34 Lakini Mafarisayo waliposikia kuwa Yesu amewanyamazisha Masadukayo, walijikusanya wao wenyewe kwa pamoja. 35 Mmoja wao, akiwa mwana sheria, alimwuliza swali kwa kumjaribu. 36 “Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu kuliko zote katika sheria?” 37 Yesu akamjibu, “Lazima umpende Bwana kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu na ya kwanza. 39 Na ya pili inafanana na hiyo- Ni lazima kumpenda jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. 40 Sheria zote na Manabii hutegemea amri hizi mbili.” 41 Na Mafarisayo walipokuwa bado wamejikusanya pamoja, Yesu aliwauliza swali. 42 Akisema, “J! e, Mwafikiri nini juu ya Kristo? Yeye ni Mwana wa nani?” Nao wakamjibu, “Ni mwana wa Daudi.” 43 Yesu akawajibu, “Ni kwa namna gani Daudi katika Roho anamwita Bwana, akisema, 44 'Bwana alimwambia Bwana wangu, “Kaa mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowafanya maadui zako wawekwe chini ya miguu yako.”'?” 45 Kama Daudi anamwita Kristo “Bwana,” jinsi gani atakuwa mtoto wake?” 46 Hakuna aliyeweza kumjibu neno tena, na hakuna aliyethubutu tena kumwuliza maswali zaidi tangu siku hiyo na kuendelea.