20
Kwa maana ufalme wa mbinguni unafanana na mmliki wa shamba, aliyeamka asubuhi na mapema ili kuajiri wafanyakazi katika shamba lake la mizabibu. Baada ya kuwa amekubaliana na wafanyakazi dinari moja kwa kutwa, aliwatuma kwenda katika shamba lake la mizabibu. Alienda tena baada ya masaa matatu hivi na aliona wafanyakazi wengine wakiwa wamesimama bila kazi katika eneo la soko. Akawaambia, 'Ninyi pia, nendeni katika shamba la mizabibu, na chochote kilicho halali nitawapa.' Hivyo wakaenda kufanya kazi. Akaenda tena baada ya masaa sita na tena katika saa ya tisa, na alifanya hivyo hivyo. Mara nyingine tena mnamo saa kumi na moja, alienda na kuwakuta watu wengine wamesimama bila kazi. Aliwaambia, 'kwanini mmesimama hapa bila kazi yoyote kwa siku nzima? Wakamwambia, kwasababu hakuna mtu yeyote aliyetuajiri. Akawaambia, 'Nanyi ninyi pia nendeni katika shamba la mizabibu.' Wakati wa jioni ulipofika, mwenye shamba la mizabibu alimwambia msimamizi wake, 'Waite wafanyakazi na uwalipe mishahara, kwa kuanza na wa mwisho hadi wa kwanza.' Walipokuja wale walioajiriwa saa kumi na moja, kila mmoja wao alipokea dinari. 10 Walipokuja wafanyakazi wa kwanza, walifikiri kuwa watapokea zaidi, lakini walipokea pia kila mmoja dinari moja kila mtu. 11 Baada ya kupokea malipo yao, walimlalamikia mmiliki wa shamba. 12 Wakasema, 'Hawa wafanyakazi wa mwisho wametumia saa moja tu katika kufanya kazi, lakini umewalinganisha na sisi, sisi tumebeba mzigo kwa siku nzima na kuungua na joto.' 13 Lakini mwenye shamba akajibu na kusema kwa mmoja wao, 'Rafiki, sikutenda jambo baya. Je! hatukukubaliana na mimi kwa dinari moja? 14 Pokea kile kilicho halali yako na uende zako. Ni furaha yangu kuwapa hawa wafanyakazi walioajiriwa mwisho sawa sawa na wewe. 15 Je! Si haki kwangu kufanya kile ninachotaka na mali zangu? Au jicho lako ni ovu kwa sababu mimi ni mwema? 16 Hivyo wa mwisho atakuwa kwanza na wa kwanza wa mwisho'' 17 Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalem, aliwachukuwa wanafunzi wake kumi na mbili pembeni, na njiani akawaambia, 18 ''Tazama tunaelekea Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa katika mikono ya wakuu wa makuhani na waandishi. Watamhukumu kifo 19 na watamtoa kwa watu wa mataifa ili kumdhihaki, kumchapa na kumsulibisha. Lakini katika siku ya tatu atafufuka.'' 20 Kisha mama wa wana wa Zebedayo alikuja kwa Yesu na wana wake. Alipiga magoti mbele yake na kumwomba kitu kutoka kwake. 21 Yesu akamwambia, “Unataka nini?” Akamwambia, ''Amuru kuwa hawa wanangu wawili wakae, mmoja mkono wako wa kulia na mmoja mkono wako wa kushoto katika ufalme wako.'' 22 Lakini Yesu akajibu na kusema, “Haujui kile unachoomba. Je! Unaweza kukinywea kikombe ambacho nitakinywea?” wakamwambia, “Tunaweza.” 23 Akawaambia, “Kikombe changu hakika mtakinywea. Lakini kukaa mkono wangu wa kulia na mkono wangu wa kushoto si jukumu langu kuwapa, lakini ni kwa wale ambao wamekwisha kuandaliwa na Baba yangu.” 24 Wanafunzi wengine kumi waliposikia hivyo, wakahuzunishwa sana na wale ndugu wawili. 25 Lakini Yesu aliwaita mwenyewe na kuwaambia, “Mnafahamu ya kuwa watawala wa mataifa huwatiisha, na wakuu wao hutekeleza mamlaka juu yao. 26 Lakini isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote atakayetaka kuwa mkubwa miongoni mwenu lazima awe mtumishi wenu. 27 Na atakaye kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima awe mtumishi wenu. 28 Kama vile Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa uhai wake kuwa ukombozi kwa wengi.” 29 Wakati wakitoka Yeriko, umati mkubwa ulimfuata. 30 Na waliwaona vipofu wawili wameketi kando ya barabara. Waliposikia kuwa Yesu alikuwa anapita, walipaza sauti na kusema, “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie.” 31 Lakini umati ukawakemea, na kuwaambia nyamazeni. Hata hivyo, wao wakapaza sauti zaidi na kusema, “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie.” 32 Kisha Yesu alisimama na aliwaita na kuwauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” 33 Wakamwambia, “Bwana kwamba macho yetu yafumbuliwe.” 34 Basi Yesu, akiwa amevutwa na huruma, akayagusa macho yao, mara hiyo, wakapokea uwezo wa kuona na wakamfuata.