17
Siku sita baadaye Yesu aliwachukua pamoja naye Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, na akawachukua mpaka juu ya mlima mrefu wao wenyewe. Alibadilishwa mbele yao. Uso wake ukang'aa kama jua, na nguo zake zilionekana zenye kung'aa kama nuru. Tazama, pale walitokea Musa na Eliya wakiongea naye. Petro akajibu na kumwambia Yesu, “Bwana, ni vema kwetu sisi kuwepo mahali hapa. Kama ukitamani, nitajenga hapa vibanda vitatu - kimoja chako, na kimoja kwa ajili ya Musa, na kimoja kwa ajili ya Eliya.” Wakati anaongea, tazama wingu jeupe likawatia kivuli, na tazama, ikatokea sauti toka kwenye wingu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa ninayependezwa naye. Msikilizeni yeye.” Wanafunzi waliposikia hayo, wakaanguka kifudifudi na wakaogopa sana. Kisha Yesu akaja akawagusa na kusema, “Inukeni wala msiogope.” Nao wakainua nyuso zao juu lakini hawakumwona mtu isipokuwa Yesu pekee. Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu akawaagiza, akasema, “Msitoe habari ya maono hayo mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuka kutoka katika wafu.” 10 Wanafunzi wake wakamwuliza, wakisema, “ Ni kwanini waandishi wanasema kuwa Eliya atakuja kwanza? 11 Yesu akawajibu na kusema, “Eliya atakuja kweli na atarudisha mambo yote. 12 Lakini naawaambieni ninyi, Eliya amekwisha kuja, lakini hawakumtambua. Badala yake, walimfanyia mambo watakayo wao. Na hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyoteswa katika mikono yao.” 13 Ndipo wanafunzi wakatambua kuwa alikuwa akiongea habari za Yohana Mbatizaji. 14 Walipofika katika umati wa watu, mtu mmoja alimwendea, akapiga magoti mbele zake, na kumwambia, 15 “Bwana, umhurumie mwanangu, maana amekuwa na kifafa na kuteseka sana. Kwa kuwa mara nyingi huanguka motoni au kwenye maji. 16 Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya. 17 Yesu akajibu akisema, “Enyi Kizazi kisichoamini na kilichoharibika, nitakaa pamoja nanyi mpaka lini? Nitavumiliana nanyi hata lini? Mlete hapa kwangu.” 18 Yesu alimkemea, na pepo akamtoka. Kijana aliponywa tangu saa ile. 19 Kisha wanafunzi wakamjia Yesu kwa siri na kumwuliza, “Kwanini hatukuweza kumfukuza?” 20 Yesu akawaambia, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Kweli nawaambieni, kama mtakuwa na imani hata ndogo kama punje ya mbegu ya haradali, mtaweza kuuambia mlima huu, hama kutoka hapa uende kule, nao utahama na hakutakuwa na kitu chochote cha kushindikana kwenu. 21 (Zingatia: Maneno ya msitari wa 21 “Lakini, aina hii ya pepo haiwezekani kutoka, ila kwa maombi na Kufunga” hayaonekani katika nakala bora za kale). 22 Wakati wakiwa bado Galilaya, Yesu akawaambia Wanafunzi wake, “Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa watu. 23 Na watamwua, na siku ya tatu atafufuka.” Wanafunzi walihuzunika sana. 24 Nao walipofika Kapenaumu, watu wakusanyao kodi ya nusu shekeli wakamwendea Petro na kusema, “Je mwalimu wenu hulipa kodi ya nusu shekeli?” 25 Akasema, “Ndiyo” Lakini Petro alipoingia ndani ya nyumba, Yesu akaongea na Petro kwanza na kusema, “ Unafikiria nini Simon? Wafalme wa dunia, hupokea kodi au ushuru kutoka nani? Kwa wale wanaowatawa kutoka kwa wageni? 26 Na wakati Petro aliposema, “Kutoka kwa wageni” Yesu akamwambia, hivyo watawaliwa wameondolewa katika ulipaji. 27 Lakini tusije tukawafanya watoza ushuru wakatenda dhambi, nenda baharini, tupa ndoano, na umtwae yule samaki ajaye kwanza. Baada ya kuufungua mdomo wake, utakuta mle shekeli moja. Ichukue na uwape watoza ushuru kwa ajili yangu na wewe.