Mathayo
1
Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alikuwa baba wa Isaka, na Isaka baba wa Yakobo, na Yakobo baba wa Yuda na ndugu zake. Yuda alikuwa baba wa Peresi na Sera kwa Tamari, Peresi baba wa Hezeroni, na Hezeroni baba wa Ramu. Ramu alikuwa baba wa Aminadabu, Aminadabu baba wa Nashoni, na Nashoni baba wa Salimoni. Salimoni alikuwa baba wa Boazi kwa Rahabu, Boazi baba wa Obedi kwa Ruth, Obedi baba wa Yese, Yese alikuwa baba wa mfalme Daudi. Daudi alikuwa baba wa Sulemani kwa mke wa Uria. Sulemani alikuwa baba wa Rehoboamu, Rehoboamu baba wa Abiya, Abiya baba wa Asa. Asa alikuwa baba wa Yehoshafati, Yehoshafati baba wa Yoramu, na Yoramu baba wa Uzia. Uzia alikuwa baba wa Yothamu, Yothamu baba wa Ahazi, Ahazi baba wa Hezekia. 10 Hezekia alikuwa baba wa Manase, Manase baba wa Amoni na Amoni baba wa Yosia. 11 Yosia alikuwa baba wa Yekonia na kaka zake wakati wa kuchukuliwa kwenda Babeli. 12 Na baada ya kuchukuliwa kwenda Babeli, Yekonia alikuwa baba wa Shatieli, Shatieli alikuwa babu yake na Zerubabeli. 13 Zerubabeli alikuwa baba wa Abiudi, Abiudi baba wa Eliakimu, na Eliakimu baba wa Azori. 14 Azori alikuwa baba wa Zadoki, Zadoki baba wa Akimu, na Akimu baba wa Eliudi. 15 Eliudi alikuwa baba wa Elieza, Elieza baba wa Matani na Matani baba wa Yakobo. 16 Yakobo alikuwa baba wa Yusufu mume wa Mariamu, ambaye kwa yeye Yesu alizaliwa, aitwaye Kristo. 17 Vizazi vyote tangu Ibrahimu hadi Daudi vilikuwa vizazi kumi na vinne, kutoka Daudi hadi kuchukuliwa kwenda Babeli vizazi kumi na vinne, na kutoka kuchukuliwa kwenda Babeli hadi Kristo vizazi kumi na vinne. 18 Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulikuwa kwa namna hii. Mama yake, Mariamu, alichumbiwa na Yusufu, lakini kabla hawajakutana, alionekana kuwa na mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 19 Mume wake Yusufu, alikuwa mtu mwenye haki hakutaka kumwaibisha hadharani. Aliamua kusitisha uchumba wake naye kwa siri. 20 Alipokuwa akifikiri juu ya mambo haya, Malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema,'' Yusufu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Mariamu kama mkeo, kwa sababu mimba aliyonayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 Atajifungua mtoto wa kiume na utamwita jina lake Yesu, kwa maana atawaokoa watu wake na dhambi zao.'' 22 Yote haya yalitokea kutimizwa kile kilichonenwa na Bwana kwa njia ya nabii, akisema, 23 “Tazama, bikira atachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume, na watamwita jina lake Imanueli”— maana yake, “Mungu pamoja nasi.” 24 Yusufu aliamka kutoka usingizini na kufanya kama malaika wa Bwana alivyomwamuru na alimchukua kama mkewe. 25 Hata hivyo, hakulala naye mpaka alipojifungua mtoto wa kiume na alimwita jina lake Yesu.