10
1 Yesu aliondoka eneo hilo na akaenda katika mkoa wa Uyahudi na eneo la mbele ya Mto Yorodani, na makutano walimfuata tena. Aliwafundisha tena, kama ilivyokuwa kawaida yake kufanya.
2 Na Mafarisayo walikuja kumjaribu na wakamuuliza, “Ni halali kwa mwanamume kuachana na mke wake?”
3 Yesu akawajibu, “Musa aliwaamuru nini?”
4 Wakasema, “Musa aliruhusu kuandika cheti cha kuachana na kisha kumfukuza mwanamke.”
5 “Ni kwa sababu ya mioyo yenu migumu ndiyo maana aliwaandikia sheria hii,” Yesu aliwaambia.
6 “Lakini kutoka mwanzo wa uumbaji, 'Mungu aliwaumba mwanamume na mwanamke.'
7 Kwa sababu hii mwanamume atamwacha baba yake na mama yake na ataungana na mke wake,
8 na hao wawili watakuwa mwili mmoja; Kwa kuwa si wawili tena, bali mwili mmoja.
9 Kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”
10 Walipokuwa ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza tena kuhusu hili.
11 Akawaambia, “Yeyote amwachaye mke wake na kumwoa mwanamke mwingine, anafanya uzinzi dhidi yake.
12 Mwanamke naye akimwacha mme wake na kuolewa na mwanamme mwingine, anafanya uzinzi.”
13 Nao walimletea watoto wao wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea.
14 Lakini Yesu alipotambua hilo, hakufurahishwa nalo kabisa akawaambia, “Waruhusuni watoto wadogo waje kwangu, na msiwazuie, kwa sababu walio kama hawa ufalme wa Mungu ni wao.
15 Ukweli nawaambia, yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hakika hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu.
16 Kisha akawachukua watoto mikononi mwake na akawabariki akiwawekea mikono yake juu yao.
17 Na alipoanza safari yake mtu mmoja alimkimbilia na akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu Mwema, nifanye nini ili niweze kurithi uzima ya milele?”
18 Na Yesu akasema, “Kwa nini unaniita mwema? Hakuna aliye mwema, isipokuwa Mungu peke yake.
19 Unazijua amri: 'Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, mheshimu baba na mama yako'.”
20 Mtu yule akasema, “Mwalimu, haya yote nimeyatii tangu nikiwa kijana.”
21 Yesu alimwangalia na kumpenda. Akawambia, “Unapungukiwa kitu kimoja. Unapaswa kuuza vyote ulivyo navyo na uwape masikini, na utakuwa na hazina mbinguni. Ndipo uje unifuate.”
22 Lakini alikata tamaa kwa sababu ya maelezo haya; aliondoka akiwa mwenye huzuni, kwa kuwa alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu akatazama pande zote na kuwaambia wanafunzi wake, “Ni jinsi gani ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu!
24 Wanafunzi walishangazwa kwa maneno haya. Lakini Yesu akawaambia tena, “Watoto, ni jinsi gani ilivyo vigumu kuingia katika ufalme wa Mungu!
25 Ni rahisi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano, kuliko mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
26 Walishangazwa sana na wakasemezana, “Hivyo nani ataokoka”
27 Yesu akawaangalia na kusema, “ Kwa binadamu haiwezekani, lakini sio kwa Mungu. Kwa kuwa katika Mungu yote yanawezekana.”
28 “Petro akaanza kuzungumza naye, “Angalia tumeacha vyote na tumekufuata.”
29 Yesu akasema, “Ukweli nawaambia ninyi, hakuna aliyeacha nyumba, au kaka, au dada, au mama, au baba, au watoto, au ardhi, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili,
30 ambaye hatapokea mara mia zaidi ya sasa hapa duniani: nyumba, kaka, dada, mama, watoto, na ardhi, kwa mateso, na ulimwengu ujao, uzima wa milele.
31 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.”
32 Walipokuwa njiani, kwenda Yerusalemu, Yesu alikuwa amewatangulia mbele yao. Wanafunzi walishangaa, na wale waliokuwa wanafuata nyuma waliogopa. Ndipo Yesu akawatoa pembeni tena wale kumi na wawili na akaanza kuwaambia ambacho kitamtokea hivi karibuni:
33 “Tazama, tunakwenda mpaka Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atafikishwa kwa makuhani wakuu na waandishi. Watamhukumu afe na watamtoa kwa watu wa Mataifa.
34 Watamdhihaki, watamtemea mate, watampiga fimbo, na watamwua. Lakini baada ya siku tatu atafufuka.”
35 Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walikuja kwake na kusema, “Mwalimu, tunakuhitaji utufanyie chochote tukuombacho.”
36 Aliwaambia, “Mnataka niwatendee nini?”
37 Wakasema, “Turuhusu tukae nawe katika utukufu wako, mmoja katika mkono wako wa kuume na mwingine mkono wako wa kushoto.”
38 Lakini Yesu aliwajibu, “Hamjui mnachoomba. Mnaweza kukinywea kikombe ambacho nitakiywea au kustahimili ubatizo ambao nitabatizwa?”
39 Wakamwambia, “Tunaweza” Yesu akawaambia, “Kikombe nitakachokinywea, mtakinywea. Na ubatizo ambao kwao nimebatizwa, mtaustahimili.
40 Lakini atakayekaa mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto sio mimi wa kutoa, lakini ni kwa wale ambao kwao imekwisha andaliwa.”
41 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana.
42 Yesu akawaita kwake na kusema, “Mnajua kuwa wale wanaodhaniwa kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala, na watu wao mashuhuri huwaonyesha mamlaka juu yao.”
43 Lakini haipaswi kuwa hivi kati yenu. Yeyote atakaye kuwa mkubwa kati yenu lazima awatumikie,
44 na yeyote atakaye kuwa wa kwanza kati yenu ni lazima awe mtumwa wa wote.
45 Kwa kuwa Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa bali kutumika, na kuyatoa maisha yake kuwa fidia kwa wengi.”
46 Wakaja Yeriko. Alipokuwa akiondoka Yeriko na wanafunzi wake na kundi kubwa, mwana wa Timayo, Batimayo, kipofu mwombaji, alikaa kando ya barabara.
47 Aliposikia kuwa ni Yesu Mnazareti, alianza kupiga kelele na kusema, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”
48 Wengi walimkemea yule kipofu, wakimwambia anyamaze. Lakini alilia kwa sauti zaidi, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”
49 Yesu alisimama na kuamuru aitwe. Walimwita yule kipofu, wakisema, “Kuwa shujaa! Inuka! Yesu anakuita.”
50 Akalitupa pembeni koti lake, akakimbia zaidi, na kuja kwa Yesu.
51 Yesu akamjibu na kusema, “Unataka nikufanyie nini?” Yule mwanaume kipofu akamjibu, “Mwalimu, ninataka kuona.”
52 Yesu akamwambia, “Nenda. Imani yako imekuponya.” Hapo hapo macho yake yakaona; na akamfuata Yesu barabarani.