8
1 Yahweh akazungumza na Musa, akisema,
2 “Walete Aroni na wanawe pamoja naye, mavazi na mafuta ya upako, fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo dume wawili, na kikapu cha mkate usio na hamira.
3 Ita kusanyiko lote kwenye ingilio la hema la kukutania.”
4 Kwa hiyo Musa akafanya kama Yahweh alivyomwamru, nalo kusanyiko lilikuja pamoja mbele ya ingilio la hema la kukutania. Kisha Musa akaliambia kusanyiko,
5 “Hivi ndivyo alivyotuamru Yahweh tutende.”
6 Musa akamleta Aroni na wanawe na kuwaosha kwa maji.
7 Akamvika Aroni kanzu ya ndani yenye urefu wa kufika magotini na kumfunga ukumbuu kiunoni mwake, akamvika joho la nje lenye mikono mirefu na kumvika kile kizibao chenye vipande viwili tumboni na mgongoni na kukifunga kuzunguka kiunoni mwake kwa mshipi uliosokotwa kwa ustadi na kukikaza mwilini mwake.
8 Kisha Musa akaweka kifuko kifuani mwa Aroni, na ndani ya kifuko hicho akaweka Urimu na Thumimu.
9 Na kisha akamfunga kiremba kichwani, na juu ya kiremba kwa mbele, akaweka bamba la dhahabu; liwe taji takatifu, kama Yahweh alivyomwamru yeye.
10 Musa akayatwaa hayo mafuta ya upako, akalipaka lile hema la kukutania na kila kitu kilichokuwamo ndani yake na kuvitenga kwa ajili ya Yahweh.
11 Akayanyunyiza hayo mafuta juu ya madhabahu mara saba, na kisha akaipaka mafuta hiyo madhabahu na vyombo vyake vyote, na sinia la kunawia na kitako chake ili kuvitenga wa ajili ya Yahweh.
12 Akamimina sehemu ya mafuta ya upako juu ya kichwa cha Aroni na kisha akampaka mafuta ili kumtenga.
13 Musa akawaleta wana wa Aroni na kuwavika kila mmoja kanzu ya ndani yenye urefu wa kufika magotini. Kila mmoja wao akamfunga kwa ukumbuu kiunoni mwake na kuwafunga vitambaa vya kitani kichwani pao, kama vile Yahweh alivyokuwa amemru Musa.
14 Musa akamleta huyo fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, naye Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha fahali ambaye wamemelete kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
15 Musa akamchinja, na kisha akachukua sehemu ya damu yake kwa kidole chake na kuiweka juu ya mpembe za madhabahu, akaitakasa hiyo madhabahu, na kuitenga kwa Mungu, ambapo kwa kufanya hivyo, aliisababisha madhabahu kuwa sehemu ya kufaa kwa kufanyia upatanisho.
16 Akachukua mafuta yote yaliyokuwa sehemu za ndani, kile kiwambo cha ini, zile figo mbili pamoja na mafuta yake, Musa akaichoma hiyo nyama yote juu ya madhabahu.
17 Lakini yule fahali, ngozi yake, nyama yake na kinyesi chake, akavichoma nje ya kambi, kama vile Yehweh alivyokuwa amemwamru yeye.
18 Musa akamleta yule konndoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, naye Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo kondoo.
19 Musa akamchinja kondoo na kuinyunyizia damu yake kila upande wa madhabahu.
20 Naye akamkatakata kondoo vipande vipande na akakiteketeza kichwa chake pamoja na vile vipande na mafuta.
21 Akaziosha kwa maji zile sehemu za ndani pamoja na miguu na akamteketeza kandoo mzima juu ya madhabahu. Ilikuwa ni dhabihu ya kuteketezwa na ilitoa harufu ya kupendeza, sadaka iliyofanywa kwa Yahweh kwa moto kama vile Yahweh alivyokuwa amemwamru Musa.
22 Kisha Musa akamleta yule kondoo dume mwingine, kondoo wa kuwekwa wakfu, naye Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha kondoo.
23 Aroni akamchinja, naye Musa akachukua sehemu ya damu na kuiweka kwenye ncha ya sikio la Aroni la kulia, juu ya dole gumba la mkono wake wa kulia, na kwenye kidole kikumbwa cha mguu wake wa kulia.
24 Akawaleta wana wa Aroni, naye akaweka sehemu ya damu ya kondoo yule kwenye ncha ya sikio lao la kulia, kwenye dole gumba lao cha mkono wa kulia na kwenye kidole chao kikubwa cha mguu wa kulia. Kisha Musa akainyunyiza damu ya huyo kila upande wa madhabahu
25 Naye akayatwaa yale mafuta, mafuta ya mkiani, mafuta liyolikuwa sehemu za ndani, na mafuta yafunikayo ini, zile figo mbili pamoja na mafuta yake na paja la kulia.
26 Akachukua mkate mmoja kutoka kwenye kikapu cha mikate isiyo na hamira ambayoo ilikuwa mbele za Yahweh, akatwaa mkate moja usio na hamira, na mkate mmoja ulioandaliwa kwa mafuta, na mkate mwemba wa kaki na akaiweka juu ya mafuta na juu ya paja la kulia la kondoo.
27 Akaiweka yote mikoni mwa Aroni na katika mikono ya wanawe na kuitikisa mbele za Yahweh kuwa sadaka ya kutikiswa
28 Kisha Musa akaichukua mikate hiyo kutoka mikononi mwao na kuiteketeza juu ya madhabahu kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Zilikuwa ni sadaka ya kuwekwa wakfu na ilitoa harufu ya kupendeza. Ilikuwa sadaka iliyofanywa kwa Yahweh kwa moto.
29 Musa akakichukua kidari na kukitikisa kuwa sadaka ya kutikiswa kwa Yahweh. Ilikuwa ni mgao wa Musa wa kondoo wa kuwekewa mikono kwa makuhani, Kama vile Yahweh alivyokuwa amemwamuru yeye.
30 Musa akatwaa sehemu ya mafuta ya upako na damu iliyokuwa juu ya madhabahu; naye akayanyunyiza haya juu ya nguo za Aroni, juu ya nguo zake mwenyewe na juu ya nguo za wana wa Aruni waliokua pamoja naye. Kwa njia hii alimtenga Aroni na nguo zake, na wanawe na nguo zao kwa ajili ya Yahweh.
31 Kwa hiyo Musa akawambia Aruni na wanawe, “Ipikeni nyama mbele ya ingilio la hema la kukutania, na hapo mtaila pamoja na mkate ulio kwenye kikapu cha kuwekwa wakfu, kama ilivyoamriwa, kusema, 'Aroni na wanawe wataila.'
32 Masalio yoyote ya nyama na mikate utayateketeza kwa moto.
33 Na hamtatoka kwenye ingilio la hema la kukutania kwa muda wa siku saba, hata zitakapotimia siku za kuwekwa mikono kwenu. Kwa kuwa kwa muda wa siku saba, Yahweh atawaweka wakfu.
34 Kilichotendeka siku hii— Yahweh ndiye amekiamru kitendekeke ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
35 Mtakaa kwenye ingilio la hema la kukutania mchana na usiku siku saba, nanyi ishikeni amri ya Yahweh ili msije mkafa, kwa sababu hivi ndivyo ilivyoamriwa.
36 Kwa hiyo Aroni na wanawe wakafanya mambo yote ambayo Yahweh alikuwa amewaamru kwa kinywa cha Musa.