21
1 Basi ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu kule Yezreeli, karibu na ikulu ya Ahabu, mfalme wa Samaria.
2 Ahabu akamwambia Nabothi, akisema, “Nipe shamba lako, ili nilifanye kuwa bustani ya mboga, kwa sababu iko karibu na nyumba yangu. Badala yake nitakupa shamba zuri la mizabibu, au, kama ukipenda nitakulipa thamani yake kwa fedha.”
3 Nabothi akamjibu Ahabu, “BWANA na alizuie hilo nisije nikatoa urithi wa mababu zangu kwako.”
4 Ahabu akaingia kwenye ikulu yake akiwa mchovu na mwenye hasira kwa sababu ya jibu ambalo Nabothi Myezreeli alimpa aliposema, “Sitakupa urithi wa mababu zangu.” Akalala kitandani kwake, akiwa amegeuza uso wake upande ule, na akagoma kula chakula chochote.
5 Yezebeli mke wake akaiingia kwake, akamwambia “Kwa nini moyo wako una huzuni, kiasi kwamba hutaki kula?”
6 Naye akamjibu,” Niliongea na Nabothi Myezreeli nikamwambia, 'Nipe shamba lako nami nitakupa pesa, au kama inakupendeza, nitakupa shamba jingine ili liwe lako.' Naye akanijibu, 'Sitakupa shamba langu.'”
7 Naye Yezebeli mkewe akamjibu, “Je, wewe si mtawala wa ufalme wa Israeli? Inuka ule; na moyo wako uwe na amani. Nitalichukua hilo shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli kwa ajili yako.
8 Kwa hiyo Yezebeli akaandika barua kwa jina la Ahabu, akaitia muhuri wake, akazituma kwa wazee na kwa watu tajiri alioketi nao kwenye vikao, na ambao pia waliishi karibu na Nabothi.
9 Katika ile barua aliyoandika, ilisema hivi, “Pigeni mbiu ya kufunga mkamkalishe Nabothi juu mbele ya watu.
10 Pia mwaweke watu wawili wasiokuwa waaminifu pamoja naye na wale watu watoe ushahidi kinyume naye, waseme, 'Ulimlaani Mungu na mfalme.”Halafu mchukueni nje mkampige kwa mawe mpaka afe.
11 Kwa hiyo watu wa mji wake, wazee na watu tajiri waishio kwenye huo mji, wakafanya kama Yezebeli alivyowaeleza, kama ilivyoandikwa kwenye zile baraua ambazo alikuwa amewatumia.
12 Wakapiga mbiu ya kufunga wakamkalisha Nabothi juu mbele ya watu.
13 Na wale watu wawili wasiokuwa waaminifu wakaja wakakaa mbele ya Nabothi; nao wakatoa ushuhuda wao dhidi ya Nabothi kuwa amemlaani Mungu na mfalme.” Kisha wakamchukua nje ya mji wakampiga kwa mawe mpaka akafa.
14 Kisha wazee wakatuma neno kwa Yezebeli, wakisema, “Nabothi ameshapigwa mawe na amekufa.”
15 Naye Yezebeli aliposikia kuwa Nabothi ameshapigwa mawe na alikuwa amekufa, akamwabia Ahabu, “Inuka na ukamiliki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia, kwa sababu Nabothi hayuko hai, bali amekufa.”
16 Ahabu aliposikia kuwa Nabothi amekufa, akainuka ili aende kwenye lile shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli na kulimiliki.
17 Ndipo neno la BWANA likamjia Eliya Mtishibi, likisema,
18 “Inuka uende ukakutane na Ahabu mfalme wa Israeli, ambaye anaishi Samaria. Yumo kwenye shamba la Nabothi, ambako ameenda kuchukua umiliki wa shamba hilo.
19 Ukaongee naye umwambie kwamba BWANA anasema, 'Je, umeua na kujimilikisha?' na utamwambia kwamba BWANA anasema, 'Mahali pale ambapo mbwa wameramba damu ya Nabothi, ndipo mbwa watakaporamba damu yako, ndiyo, damu yako.'”
20 Ahabu akamwambia Eliya, “Je, umenipatia, adui yangu?” Eliya akamjibu, “Nimekupata wewe kwa sababu, umejiuza mwenyewe kufanya yaliyo maovu mbele ya macho ya BWANA.
21 BWANA anakwambia hivi: 'Tazama, Nitaleta janga kwako na litakuangamiza kabisa na kufutilia mbali kila mtoto mume na mtumwa na mtu huru katika Israeli.
22 Nitaifanya familia yako kama familia ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama familia ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umenighadhabisha na umewasababisha Israeli kufanya dhambi.
23 Pia BWANA ameongea kuhusu Yezebeli, amesema, “mbwa watamla Yezebeli pembeni mwa ukuta wa Yezreeli.'
24 Yeyote ambaye ni mtu wa familia ya Ahabu ambaye atafia mjini - mbwa watamla. Na yeyote ambaye atafia shambani - ataliwa na ndege wa angani.”
25 Hapakuwepo na mtu kama Ahabu, ambaye alijiuza mwenyewe kufanya maovu mbele ya macho ya BWANA, ambaye mke wake Yezebeli alimchochea kufanya dhambi.
26 Ahabu alifanya matendo yachukizayo kwa ajili ya sanamu alizofanya, kama vile yale yote ambayo Waamori walifanya, BWANA akawafukuza mbele ya watu wa Israeli.
27 Ahabu aliposikis maneno haya, Akachana mavazi yake na akavaa magunia kwenye mwili wake na akfaunga, na akalala kwenye magunia na akahuzunika sana.
28 Kisha neno la BWANA likamjia Eliya Mtishibi likisema,
29 “Je, unamwona jinsi Ahabu anavyojinyenyekeza mbele yangu? Kwa sababu anajinyeyenyekeza mwenyewe mbele yangu, Sitaleta lile janga katika siku zake; Ni katika siku za mwanae, nitakpolileta hilo janga katika familia yake.”