3
1 Basi kulikuwa na Farisayo ambaye jina lake Nikodemo, mmoja wa wajumbe wa baraza la Wayahudi.
2 Mtu huyu alimwendea Bwana Yesu usiku na akamwambia, “Rabi, tunajua ya kuwa u mwalimu kutoka kwa Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kutenda ishara hizi zote Mungu asipokuwa pamoja naye.”
3 Yesu akamjibu, “Amini, amini, mtu hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu asipozaliwa mara ya pili.”
4 Nikodemo akasema,” Mtu anawezaje kuzaliwa akiwa mzee? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake mara ya pili na kuzaliwa, je anaweza?”
5 Yesu akajibu, “Amini, amini mtu sipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu.
6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili, na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
7 Usishangae kwa sababu nilikuwambia, 'ni lazima kuzaliwa mara ya pili.'
8 Upepo huvuma popote upendapo na sauti yake mwaisikia, lakini hamjui utokako wala uendako. Ndivyo ilivyo hali ya kila aliyezaliwa na roho.
9 Nikodemo akajibu, kwa kusema, “Mambo haya yawezekanaje?”
10 Yesu akamjibu, “Wewe u mwalimu wa Israeli, hata hauyajui mambo haya?
11 Amini, amini, nakuambia, kile tunachokifahamu twakishuhudia kwa kile tulichokiona. Lakini hampokei ushuhuda wetu.
12 Kama nimewambia mambo ya hapa duniani na hamuamini, mtawezaje kuamini kama nikiwambia mambo ya mbinguni?
13 Maana hakuna aliyepanda juu kutoka mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka, Mwana wa Adamu.
14 Kama vile Musa alivyomwinua nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu lazima ainuliwe,
15 ili kwamba wote watakaomwamini wapate uzima wa milele.
16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, kwamba akamtoa mwanae wa pekee, ili kwamba mtu yeyote amwaminiye asiangamie bali awe na uzima wa milele.
17 Kwa sababu Mungu hakumtuma mwanae duniani ili auhukumu ulimwengu, bali kwamba ulimwengu uokolewe katika yeye.
18 Amwaminiye Yeye hatahukumiwa. Yeye asiyemwamini tayari ameshahukumiwa kwa sababu hajaliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
19 Hii ndiyo sababu ya hukumu, ya kwamba nuru imekuja ulimwenguni, lakini wanadamu wakapenda giza zaidi ya nuru kwa sababu matendo yao yalikuwa maovu.
20 kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru wala haji nuruni ili matendo yake yasije yakawekwa wazi.
21 Lakini, yeye atendaye kweli huja kwenye nuru ili matendo yake yaonekane kwamba yametendwa kwa utiifu wa Mungu.
22 Baada ya haya, Yesu pamoja na wanafunzi walienda katika nchi ya Yudea. Huko alitumia muda pamoja nao na alikuwa akibatiza.
23 Sasa Yohana pia alikuwa akibatiza huko Ainea karibu na Salim maana kulikuwa na maji mengi pale. Watu walikuwa wakija kwake na kubatizwa,
24 kwa kuwa Yohana alikuwa hajatupwa gerezani.
25 Kisha palitokea mabishano kati ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi kuhusu sikukuuu za utakaso.
26 Wakaenda kwa Yohana wakamwambia, “Rabi, yeye uliyekuwa naye ng'ambo ya Mto Yorodani, yeye uliyeshuhudia habari zake, tazama, anabatiza na wote wanaenda wanamfuata.”
27 Yohana akajibu mtu hawezi kupokea kitu chochote isipokuwa kama amepewa kutoka mbinguni.
28 Ninyi wenyewe mwashuhudia kuwa nalisema kuwa, 'mimi sio Kristo', badala yake nilisema, 'nimetumwa mbele yake.'
29 Yeye aliye na bibi arusi ni bwana harusi. Sasa rafiki wa bwana arusi, asimamaye na kusikiliza hufurahia sana kwa sababu ya sauti ya bwana arusi. Hii sasa ni furaha yangu iliyotimilika.
30 Anapaswa kuzidi, nami napaswa kupungua.
31 Yeye atokaye juu, yu juu ya yote. Yeye aliye wa ulimwengu anatoka ulimwenguni na huongea mambo ya ki ulimwengu. Yeye atokaye mbinguni yuko juu ya yote.
32 Yeye hushuhudia yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna apokeaye ushuhuda wake.
33 Yeye aliye pokea ushuhuda wake amehakikisha kuwa Mungu ni mkweli.
34 Kwa sababu yeye aliyetumwa na Mungu huongea maneno ya Mungu. Kwa kuwa hampi Roho kwa kipimo.
35 Baba humpenda Mwana na amempa vitu vyote mikononi mwake.
36 Yeye amwaminiye Mwana anao uzima wa milele, lakini kwa yeye asiye mtii Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu hushikamana juu yake.