37
1 Hakika, moyo wangu hutetemeka kwa hili; umeondolewa kutoka katika sehemu yake.
2 Sikia, Ee, Sikia kelele za sauti yake, sauti inayotoka katika mdomo wake.
3 Huiagiza sauti chini ya mbingu yote, na huutuma mwanga wake katika mipaka ya dunia.
4 Sauti huunguruma baada yake; yeye huunguruma kwa sauti ya ukuu wake; hauzuii mshindo wa mwanga wakati sauti yake inaposikika.
5 Mungu huunguruma kwa sauti yake kwa namna ya ajabu; yeye hufanya mambo makubwa ambayo sisi hatuwezi kuyafahamu.
6 Kwa kuwa huiambia theluji, 'Angukeni juu ya dunia'; hali kadhalika kwa manyunyu ya mvua, 'Iweni manyunyu makubwa ya mvua.'
7 Huuzuia mkono wa kila mtu usifanye kazi, ili kwamba watu wote aliowaumba wataona matendo yake.
8 Kisha hayawani huenda na kujificha na kukaa katika mapango yake.
9 Dhoruba hutoka katika chumba chake upande wa kusini na baridi kutoka katika pepo zilizotawanyika katika upande wa Kaskazini.
10 Barafu imetolewa kwa pumzi ya Mungu; upana wa maji umeganda kama chuma.
11 Hakika, huyapima mawingu manene yenye unyevu; yeye huusambaza mwanga wake katika mawingu.
12 Yeye huyazungusha mawingu kwa uongozi wake, ili yafanye chochote anayoyaagiza juu ya uso wote wa ulimwengu.
13 Huyafanya haya yote yatokee; wakati mwingine hutokea kwa ajili ya kusahihisha, wakati mwingine kwa ajili ya nchi yake, na wakati mwingine ni kwa matendo ya agano la uaminifu.
14 Yasikilize haya, Ayubu; acha na ufikiri juu matendo ya ajabu ya Mungu.
15 Je unajua ni kwa namna gani Mungu hushurutisha mawingu na kuufanya mwanga wa radi ung'ae ndani yake?
16 Je unafahamu kuelea kwa mawingu, matendo ya ajabu ya Mungu, Je ni nani aliyemkamilifu katika maarifa?
17 Je unafahamu ni kwa jinsi gani mavazi yako huwa ya moto wakati nchi ikiwa imetulia kwasababu ya upepo unaotoka upande wa kusini?
18 Je unaweza kulitandaza anga kama anavyofanya - anga ambalo lina nguvu kama kioo cha chuma kigumu?
19 Tufundishe sisi kile tunachopaswa kumwambia yeye, kwa kuwa hatuwezi kutoa hoja zetu katika mpangilio kwasababu ya kiza katika akili zetu.
20 Je anapaswa kuambiwa kwamba ninapenda kuongea naye? Je mtu angependa kumezwa?
21 Sasa, watu hawawezi kulitazama jua wakati linang'aa katika anga baada ya upepo kupita katikati yake na umelisafisha kwa mawingu yake.
22 Kutoka upande wa kaskazini hutokea fahari ya dhahabu - juu ya Mungu kuna ukuu wa kutisha.
23 Na kuhusu Mwenye nguvu, hatuwezi kumpata; yeye ni mkuu katika nguvu na haki. Yeye hatesi watu.
24 Hivyo basi, watu humwogopa. Yeye huwa hawajali wale ambao ni wenye hekima katika akili zao wenyewe.”