2
1 Sasa kuhusu kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa pamoja ili tuwe naye: tunawaomba ninyi ndugu zetu,
2 kwamba msisumbuliwe wala kutabishwa kwa urahisi, kwa roho, au kwa ujumbe au kwa barua inayoonkana kuwa imetoka kwetu, ikisema ya kuwa siku ya Bwana tayari imekuja.
3 Mtu na asiwadanganye kwa namna yoyote. Kwa kuwa haitakuja mpaka lile anguko litokee kwanza na mtu wa uasi afunuliwe, yule mwana wa uharibifu.
4 Huyu ndiye apingaye naye hujiinua mwenyewe akimpinga Mungu na chochote kinachoabudiwa. Na matokeo yake, hukaa kwenye hekalu la Mungu na kujionyesha yeye kuwa kama Mungu.
5 Je, hamkumbuki kuwa nilipokuwa nanyi niliwaambia juu ya mambo haya?
6 Sasa mnajua kile kinachomzuia, ili kwamba aweze kufunuliwa kwa wakati sahihi utakapowadia.
7 Kwa kuwa siri ya yule mtu mwenye kuasi inafanya kazi mpaka sasa, ila tu kuna anaye mzuia sasa mpaka atakapotolewa njiani.
8 Ndipo yule mwenye kuasi atakapofunuliwa, amabaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake. Bwana atamfanya kuwa si chochote kwa ufunuo wa ujio wake.
9 Ujio wa yule mwenye kuasi utakuwa kwa sababu ya kazi ya shetani kwa nguvu zote, ishara na maajabu ya uongo,
10 na uongo wote wenye udhalimu. Mambo haya yatakuwepo kwa wale wanaopotea, kwa sababu hawakuupokea upendo wa kweli kwa ajili ya kuokolewa kwao.
11 Kwa sababu hiyo Mungu anawatumia kazi yenye uovu ili waamini uongo.
12 Matokeo yake ni kwamba wote watahukumiwa, wale ambao hawakuamini ukweli bali wao hujifurahisha katika udhalimu.
13 Lakini inatupasa tumshukuru Mungu kila mara kwa ajili yenu ndugu mpendwao na Bwana. Kwa sababu Bwana aliwachagua ninyi kama malimbuko ya wokovu kwa utakaso wa Roho na imani katika ile kweli.
14 Hiki ndicho alichowaitieni ninyi, kwamba kupitia injili muweza kuupata utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.
15 Kwa hiyo, ndugu, simameni imara. Ueleweni ule utamaduni mliofundishwa, kwa neno au kwa barua yetu.
16 Sasa, Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu aliyetupenda na kutupa faraja ya milele na ujasiri mwema kwa ajili ya maisha yajayo kupitia neema,
17 awafariji na kuifanya imara mioyo yenu katika kila neno na kazi njema.