44
1 Yusufu akamwamru msimamizi wa nyumba yake, akisema, “Jaza magunia ya watu hawa kwa chakula, kiasi wawezacho kubeba, na uweke pesa ya kila mtu katika mdomo wa gunia lake.
2 Uweke kikombe changu, cha fedha, katika mdomo wa gunia la mdogo, na pesa yake ya chakula pia.” Msimamizi akafanya kama Yusufu alivyosema.
3 Kukapambazuka asubuhi, na wale watu wakaruhusiwa kuondoka, wao na punda zao.
4 Walipokuwa wametoka mjini lakini hawajafika mbali, Yusufu akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Inuka, uwafuatie wale watu, na utakapowapata, wambie, 'Kwa nini mmelipa uovu badala ya mema?
5 Je hiki siyo kikombe ambacho bwana wangu hukinywea, na kikombe akitumiacho kwa uaguzi? Mmefanya vibaya, kwa jambo hili mlilolifanya.”
6 Msimamizi wa nyumba akawapata na kuwambia maneno haya.
7 Wakasema, “Kwa nini bwana wetu anasema maneno kama haya? Na iwe mbali na watumishi wako kwamba wanaweza kufanya jambo hili.
8 Tazama, pesa tulizozikuta katika midomo ya magunia yetu, tulizileta kwako kutoka katika nchi ya Kanaani. Ni kwa jinsi gani basi tunaweza kuiba katika nyumba ya bwana wako fedha au dhahabu?
9 Yeyote kitakayeonekana kwake miongoni mwa watumishi wako, atakufa, nasi sote tutakuwa watumwa wa bwana wangu.”
10 Msimamizi akasema, “Basi na iwe kwa kadili ya maneno yenu. Yeye ambaye kikombe kitaonekana kwake atakuwa mtumwa wangu, nanyi wengine mtakuwa bila hatia.”
11 Kisha kila mtu akaharakisha na kulishusha gunia lake chini. na kila mtu akalifungua gunia lake.
12 Msimamizi akatafuta. akaanza na mkubwa wa wote na kumaliza kwa mdogo wa wote, na kikombe kikaonekana katika gunia la Benjamini.
13 Wakararua mavazi yao. Kila mtu akapakia juu ya punda wake nao wakarudi mjini.
14 Yuda na ndugu zake wakaja katika nyumba ya Yusufu. Bado alikuwepo pale, nao wakainama mbele zake hata chini.
15 Yusufu akawambia, “Je ni nini hili mlilolifanya? Je hamjui kwamba mtu kama mimi anafanya uaguzi.
16 Yuda akasema, “Je tunaweza kumwambia nini bwana wangu? Tuseme nini? au ni jinsi gani twaweza kujithibitisha wenyewe? Mungu ameona uovu wa watumishi wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, wote sisi na yule ambaye kikombe kimeonekana mkononi mwake.”
17 Yusufu akasema, “Na iwe mbali nami kwamba naweza kufanya hivyo. Mtu ambaye kikombe kimeonekana mkononi mwake, huyu ndiye atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine, nendeni kwa amani kwa baba yenu.”
18 Ndipo Yuda alipomkaribia na kusema, “Bwana wangu, tafadhari mwache mtumishi wako aseme neno katika masikio ya bwana wangu, na usiziache hasira zako kuwaka dhidi ya mtumishi wako, kwani wewe ni kama Farao.
19 Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, kusema, Je mnaye baba au ndugu?'
20 Nasi tukamwambia bwana wangu, 'Tunaye baba, ni mzee, na mwana wa uzee wake, ni mdogo. Na ndugu yake alishakufa, na yeye peke yake ndiye amebaki kwa mama yake, na baba yake anampenda.'
21 Nawe ukawambia matumishi wako, 'Mleteni ili nimwone.'
22 Nasi tukamwambia bwana wangu, 'Kijana hawezi kumwacha babaye. Kwani akimwacha babaye baba yake angekufa.'
23 Na ukawambia watumishi wako, 'Mdogo wenu asipokuja pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.'
24 Na ikawa tulipokwenda kwa mtumishi wako baba yangu, tulimwambia maneno ya bwana wangu.
25 Na baba yetu akasema, Nendeni tena, mkatununulie chakula.'
26 Nasi tukasema, “Hatuwezi kushuka. Ikiwa mdogo wetu atakuwa nasi, ndipo tutakaposhuka, kwani hatuwezi kuuona uso wa mtu yule mdogo wetu asipokuwa pamoja nasi.'
27 Mtumishi wako baba yetu akatwambia, 'Mnajua kwamba mke wangu alinizalia wana wawili.
28 Na mmoja akatoka kwangu nami nikasema, “Bila shaka ameraruliwa vipande, na tangu hapo sijamwona.”
29 Nanyi mkimchukua huyu naye kutoka kwangu mabaya yanaweza kumpata, mtashusha mvi zangu kwa kaburini kwa huzuni.
30 Kwa hiyo, basi, nitapokuja kwa mtumishi wako baba yangu, na kijana hayupo nasi, kwa kuwa uhai wake umefungamanishwa katika uhai wa kijana,
31 itakuwa, atakapoona kwamba kijana hayupo nasi atakufa. Na watumishi wako watazishusha mvi za mtumishi wako baba yetu kaburini kwa masikitiko.
32 Kwani mtumishi wako alikuwa mdhamini wa kijana kwa baba yangu na alisema, 'Ikiwa sitamleta kwako, ndipo nitakapokuwa mwenye hatia kwa baba yangu daima.”
33 Kwa hiyo sasa, tafadhari mwache mtumishi wake akae kama mtumwa kwa bwana wangu badala ya kijana, na umwache kijana aende na ndugu zake.
34 Kwa maana nitakwenda jinsi gani kwa baba yangu ikiwa kijana hayupo nami? Ninaogopa kuona mabaya yatakayompata baba yangu.”