3
1 Sasa nyoka alikuwa mwerevu kuliko myama mwingine yeyote wa kondeni ambaye Yahwe Mungu alikuwa amemuumba. Akamwambia mwanamke, “Je ni kweli Mungu amesema, 'Msile matunda kutoka kwenye mti wowote bustanini'?”
2 Mwanamke akamwambia nyoka, “Twaweza kula tunda kutoka kwenye miti ya bustani,
3 lakini kuhusu tunda la mti ambao uko katikati ya bustani, Mungu alisema, 'msile, wala msiuguse, vinginevyo mtakufa.'”
4 Nyoka akamwambia mwanamke, “hakika hamtakufa.
5 Kwasababu Mungu anajua kwamba siku mkila macho yenu yatafumbuliwa, na mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
6 Na mwanamke alipoona kuwa mti ni mzuri kwa chakula, na kuwa unapendeza macho, na kwamba mti ulitamanika kwa kumfanya mtu awe mwerevu, alichukua sehemu ya tunda na akala. Na sehemu yake pia akampatia mumewe aliyekuwa naye, naye akala.
7 Macho ya wote wawili yalifumbuliwa, na wakajua kuwa wako uchi. Wakashona majani ya miti pamoja na wakatengeneza vya kujifunika wao wenyewe.
8 Wakasikia sauti ya Yahwe Mungu akitembea bustanini majira ya kupoa kwa jua, kwa hiyo mwanaume na mke wake wakajificha wao wenyewe kwenye miti ya bustani kuepuka uwepo wa Yahwe Mungu.
9 Yahwe Mungu akamuita mwanaume na kumwambia, “ uko wapi?”
10 Mwanaume akasema, “nilikusikia bustanini, na nkaogopa, kwa sababu nilikuwa uchi. kwa hiyo nikajificha.”
11 Mungu akasema, “Ni nani alikwambia kuwa ulikuwa uchi? Je umekula kutoka mti ambao nilikuagiza usile matunda yake?”
12 Mwanaume akasema, “ Mwanamke uliyenipa kuwa na mimi, alinipatia tunda kutoka kwenye mti, na nikala.”
13 Yahwe Mungu akamwambia mwanamke, “ Nini hiki ulichofanya?” mwanamke akasema, “nyoka alinidanganya, na nikala.”
14 Yahwe Mungu akamwambia nyoka, “ kwa sababu umefanya jambo hili, umelaaniwa wewe mwenyewe miongoni mwa wanyama wote wa kufugwa na wanyama wote wa mwituni. Itakuwa kwa tumbo lako utakwenda, na mavumbi utakula kwa siku zote za maisha yako.
15 Nitaweka uadui kati yako na mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake. Atakujeruhi kichwa chako na utamjeruhi kisigino chake.”
16 Kwa mwanamke akasema, nitaongeza uchungu wakati wa kuzaa watoto; itakuwa katika maumivu utazaa watoto. Tamaa yako itakua kwa mume wako, lakini atakutawala.”
17 Kwa Adam akasema, “kwa sababu umesikiliza sauti ya mke wako, na umekula kutoka katika mti, ambao nilikuagiza, nikisema, “ usile matunda yake', ardhi imelaaniwa kwa sababu yako; kupitia kazi yenye maumivu utakula matunda ya ardhi kwa siku zote za maisha yako.
18 Ardhi itazaa miiba na mbigili kwa ajili yako, na utakula mimea ya shambani.
19 Kwa jasho la uso wako utakula mkate, mpaka utakapo irudia ardhi, ambayo kwayo ulitwaliwa. kwa kuwa wewe ni mavumbi na kwenye mavumbi utarudi.”
20 Mwanaume akaita mke wake jina Hawa kwa sababu alikuwa mama wa wote wenye uhai.
21 Yahwe Mungu akatengeneza mavazi ya ngozi kwa ajili ya Adam na mke wake na akawavalisha.
22 Yahwe Mungu akasema, “ sasa mtu huyu amekuwa kama mmoja wetu, ajuaye mema na mabaya. Kwa hiyo sasa hataruhusiwa kugusa kwa mkono wake, na kuchukua tunda la mti wa uzima, na kula akaishi tena milele.”
23 Kwa hiyo Yahwe Mungu akamuondoa kutoka kwenye bustani ya Edeni, kwenda kulima ardhi ambayo kwahiyo alikuwa ametwaliwa.
24 Kwa hiyo Mungu akamfukuza mtu huyu nje ya bustani, na akaweka kerubi mashariki mwa bustani ya Edeni, na upanga wa moto ulio geuka geuka kila upande, ili kulinda njia ya kwenda kwenye mti wa uzima.