Mwanzo
1
1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na nchi.
2 Nayo nchi haikuwa na umbo na ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji. Roho wa Mungu alikuwa akielea juu ya uso wa maji.
3 Mungu akasema, “na kuwe nuru,” na kulikuwa na nuru.
4 Mungu akaona nuru kuwa ni njema. Akaigawa nuru na giza.
5 Mungu akaiita nuru “ mchana” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni na asubuhi, siku ya kwanza.
6 Mungu akasema, “ na kuwe na anga kati ya maji, na ligawe maji na maji.”
7 Mungu akafanya anga na kugawanya maji yaliyo kuwa chini ya anga na maji ambayo yalikuwa juu ya anga. Ikawa hivyo.
8 Mungu akaita anga “mbingu.” Ikawa jioni na asubuhi siku ya pili.
9 Mungu akasema, “maji yaliyo chini ya mbingu yakusanyike pamoja mahali pamoja, na ardhi kavu ionekane.” Ikawa hivyo.
10 Mungu aliita ardhi kavu “nchi,” na maji yaliyo kusanyika akayaita “bahari.” Akaona kuwa ni vyema.
11 Mungu akasema, nchi ichipushe mimea: miche itoayo mbegu na miti ya matunda itoayo matunda ambayo mbegu yake imo ndani ya tunda, kila kitu kwa namna yake.” Ikawa hivyo.
12 Nchi ikatoa mimea, miche itoayo mbegu ya aina yake, na miti itoayo tunda ambalo mbegu yake imo ndani yake, kwa aina yake. Mungu akaona kuwa ni vyema.
13 Ikawa jioni na asubuhi, siku ya tatu.
14 Mungu akasema, “kuwe na mianga katika anga kutenganisha mchana na usiku. Na ziwe kama ishara, kwa majira, kwa siku na miaka.
15 Ziwe mianga katika anga ili kutoa mwanga juu ya nchi.” Ikawa hivyo.
16 Mungu akafanya mianga mikuu miwili, mwanga mkuu zaidi kutawala mchana, na mwanga mdogo kutawala usiku. Akafanya nyota pia.
17 Mungu akazipanga katika anga kutoa mwanga juu nchi,
18 kutawala mchana na usiku, na kugawanya mwanga kutoka kwenye giza. Mungu akaona kuwa ni vyema.
19 Ikawa jioni na asubuhi, siku ya nne.
20 Mungu akasema, “maji yajae idadi kubwa ya viumbe hai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu.”
21 Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini, pamoja na kila kiumbe hai cha aina yake, viumbe waendao na wanaojaa kila mahali majini, na kila ndege mwenye mabawa kwa aina yake. Mungu akaona kuwa ni vyema.
22 Mungu akavibariki, akisema, “zaeni na muongezeke, na mjae majini katika bahari. Ndege waongezeke juu nchi.”
23 Ikawa jioni na asubuhi, siku ya tano.
24 Mungu akasema, “ nchi na itoe viumbe hai, kila kiumbe kwa aina yake, mnyama wa kufugwa, vitu vitambaavyo, na wanyama wa nchi, kila kitu kwa jinsi yake.” Ikawa hivyo.
25 Mungu akafanya wanyama wa nchi kwa aina yake, wanyama wa kufugwa kwa aina yake, na kila kitambaaho juu ya ardhi kwa aina yake. Akaona kuwani vyema.
26 Mung akasema, “na tumfanye mtu katika mfano wetu, wa kufanana na sisi. Wawe na mamlaka juu ya samaki wa bahari, juu ya ndege wa angani, juu ya wanyama wa kufuga, juu ya nchi yote, na juu ya kila kitu kitambaacho kinacho tambaa juu ya nchi.”
27 Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake. Katika mfano wake alimuumba. Mwanaume na mwanamke aliwaumba.
28 Mungu akawabariki na akawaambia, “zaeni na kuongezeka. Jazeni nchi, na muitawale. Muwe na mamlaka juu ya samaki wa baharini, juu ya ndege wa angani, na juu ya kila kiumbe hai kiendacho juu ya nchi,”
29 Mungu akasema, “tazama, nimewapeni kila mmea uzaao mbegu ambao uko juu ya nchi, na kila mti wenye tunda ambalo lina mbegu ndani yake. Vitakuwa ni chakula kwenu.
30 Kwa kila mnyama wa nchi, kwa kila ndege wa angani, na kila kitambaacho juu ya nchi, na kila kiumbe ambacho kina pumzi ya uhai ni metoa kila mmea kwa ajili ya chakula.” ikawa hivyo.
31 Mungu akaona kila kitu alichokiumba. Tazama, kikawa chema sana. Ikawa jioni na asubuhi siku ya sita.