4
1 Hivi ndivyo mtu atuhesabu sisi, kama watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za kweli za Mungu.
2 Katika hili, kinachotakiwa kwa uwakili ni kwamba wawe wa kutumainiwa.
3 Lakini kwangu mimi ni kitu kidogo sana kuwa ninahukumiwa na ninyi au hukumu ya kibinadamu. Kwa kuwa sijihukumu hata mimi mwenyewe.
4 Sijihukumu mimi mwenyewe, hii haina maana kuwa mimi ni mwenye haki. Ni Bwana anihukumuye.
5 Kwa hiyo, msitamke hukumu juu ya lolote kabla ya wakati, kabla ya kuja kwa Bwana. Atayaleta nuruni mambo yaliyofichika gizani na kufunua makusudi ya mioyo. Ndipo kila mmoja atapokea sifa yake kutoka kwa Mungu.
6 Sasa, kaka na dada zangu, mimi mwenyewe na Apolo nimetumia kanuni hizi kwa ajili yenu. Ili kwamba kutoka kwetu mnaweza kujifunza maana ya usemi, “Usiende zaidi ya kilivyoandikwa.” Hii ni kwamba hakuna mmoja wenu ajivunaye juu ya mwingine.
7 Maana ni nani aonaye tofauti kati yenu na mwingine? Ni nini ulicho nacho hukukipokea bure? Kama umekwisha kupokea bure, kwa nini mnajivuna kama hamkufanya hivyo?
8 Tayari mnavyo vyote ambavyo mngetaka! Tayari mmekuwa na utajiri! Mmeanza kutawala-na kwamba mnamiliki zaidi yetu sisi! Kweli, nawatakia umililki mwema ili kwamba tumiliki pamoja nanyi.
9 Kwa hiyo ninadhani Mungu ametuweka sisi mitume kama kutuonyesha wa mwisho katika mustari wa maandamano na kama watu waliohukumiwa kuuawa. Tumekuwa kama tamasha kwa ulimwengu, kwa malaika na kwa wanadamu.
10 Sisi ni wajinga kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye hekima katika Kristo. Tu wanyonge, lakini ninyi mna nguvu. Mnaheshimiwa, lakina sisi tunadharauliwa.
11 Hata saa hii tuna njaa na kiu, hatuna nguo, tuna mapigo, na tena hatuna makazi.
12 Tunafanya kazi kwa bidii, kwa mikono yetu wenyewe. Tunapodharauliwa, twabariki. Wakati tunapoteswa, twavumilia.
13 Tunapotukanwa, twarudisha kwa upole. Tumekuwa, na tu bado tunahesabiwa kuwa kama kukataliwa na dunia na takataka kwa mambo yote.
14 Siandiki mambo haya kuwaaibisha ninyi, lakini kuwarudi ninyi kama watoto wangu niwapendao.
15 Hata kama mna waalimu makumi elfu katika Kristo, hamna baba wengi. Kwa kuwa nimekuwa baba yenu katika Yesu Kristo kupitia injili.
16 Hivyo ninawasihi mniige mimi.
17 Hiyo ndiyo sababu nilimtuma kwenu Timotheo, mpendwa wangu na mtoto mwaminifu katika Bwana. Atawakumbusheni njia zangu katika Kristo, kama ninavyofundisha kila mahali na kila kanisa.
18 Sasa baadhi yenu wanajisifu, wakitenda kana kwamba sitakuja kwenu.
19 Lakini nitakuja kwenu kitambo, kama Bwana akipenda. Ndipo nitajua si maneno yao tu wanaojisifu, lakini nitaona nguvu zao.
20 Kwa kuwa ufalme wa Mungu hauwi katika maneno bali katika nguvu.
21 Mnataka nini? Nije kwenu na fimbo au kwa upendo na katika roho ya upole?