14
1 Utafuteni upendo na kutamani sana karama za rohoni, zaidi sana mpate kutoa unabii.
2 Maana yeye anenaye kwa lugha hasemi na watu bali husema na Mungu. Maana hakuna aelewaye kwa sababu anena mambo yaliyofichika katika Roho.
3 Lakini yeye atoaye unabii, asema na watu na kuwajenga, kuwatia moyo, na kuwafariji.
4 Yeye anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, lakini yeye atoaye unabii hulijenga kanisa.
5 Sasa natamani kwamba ninyi nyote mnene kwa lugha. Lakini zaidi ya hayo, natamani ya kwamba mtoe unabii. Yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha (labda awepo wa kutafasiri), ili kwamba kanisa lipate kujengwa.
6 Lakini sasa, kaka na dada zangu, nikija kwenu na kunena kwa lugha, nitawafaidia nini ninyi? Siwezi, isipokuwa nasema nanyi kwa njia ya ufunuo, au kwa njia ya maarifa, au unabii, au kwa njia ya fundisho.
7 Ikiwa vitu visivyo na uhai kama filimbi au kinubi visipotoa sauti zilizo na tofauti, itatambulikanaje ni chombo gani kinachezwa?
8 Kwa maana ikiwa baragumu itatoa sauti isiyojulikana, ni jinsi gani mtu atatambua ya kuwa ni muda wa kujiandaa kwa vita?
9 Vivyo hivyo na ninyi. Mkitoa kwa ulimi neno lisilo dhahiri, ni jinsi gani mtu ataelewa mnachosema? Mtakuwa mkiongea, na hakuna atakayewaelewa.
10 Hakuna shaka kwamba kuna lugha nyingi mbalimbali duniani, na hakuna hata moja isiyo na maana.
11 Lakini ikiwa sijui maana ya lugha, nitakuwa mgeni kwake yeye anenaye, naye anenaye atakuwa mgeni kwangu.
12 Vivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani sana kuona uthihirisho wa Roho, takeni kwamba mzidi sana kulijenga kanisa.
13 Hivyo, yeye anenaye kwa lugha na aombe apewe kutafasiri.
14 Kwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.
15 Nifanye nini? Nitaomba kwa roho yangu, lakini pia nitaomba kwa akili zangu. Nitaimba kwa roho yangu, na nitaimba kwa akili zangu pia.
16 Vinginevyo, ukimsifu Mungu kwa roho, yeye aliye mgeni ataitikaje “Amina” utoapo shukurani, akiwa hayajui usemayo?
17 Maana ni kweli wewe washukuru vema, lakini yule mwingine hajengwi.
18 Namshukuru Mungu kwa kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote.
19 Lakini katika kanisa ni heri ninene maneno matano kwa ufahamu wangu ili nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha.
20 Kaka na dada zangu, msiwe watoto katika kufikiri kwenu. Badala yake, kuhusiana na uovu, iweni kama watoto wachanga. Lakini katika kufikiri kwenu mkawe watu wazima.
21 Imeandikwa katika sheria, “Kwa watu wa lugha nyingine na kwa midomo ya wageni nitasema na watu hawa. Wala hata hivyo hawatanisikia,” asema Bwana.
22 Hivyo, ndimi ni ishara, sio kwa walioamini, bali kwa wasioamini. Lakini kutoa unabii ni ishara, sio kwa wasioamini, bali kwa ajili yao waaminio.
23 Haya, ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja na wote wanene kwa lugha, na wageni na wasioamini wameingia, je hawawezi kusema kwamba mna wazimu?
24 Lakini ikiwa wote mnatoa unabii na asiyeamini au mgeni akaingia, atashawishiwa na yote asikiayo. Atahukumiwa na yote yasemwayo.
25 Siri za moyo wake zingefunuliwa. Matokeo yake, angeanguka kifudifudi na kumwabudu Mungu. Angekiri ya kwamba Mungu yu kati yenu.
26 Nini kifuatacho basi, kaka na dada zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana Zaburi, mafundisho, mafunuo, lugha au tafsiri. Fanyeni kila kitu ili kwamba mlijenge kanisa.
27 Kama yeyote ananena kwa lugha, wawepo wawili au watatu, na kila mmoja katika zamu. Na mtu lazima atafasiri kilichosemwa.
28 Lakini kama hakuna mtu wa kutafasiri, basi kila mmoja wao akae kimya ndani ya kanisa. Basi kila mmoja aongee peke yake na kwa Mungu.
29 Na manabii wawili au watatu wanene, na wengine wasikilize kwa kupambanua kilichosemwa.
30 Lakini aliyeketi akifunuliwa jambo katika huduma, yule ambaye alikuwa ananena na anyamaze.
31 Kwa kuwa kila mmoja wenu anaweza kutoa unabii mmoja baada ya mwingine ili kwamba kila mmoja aweze kujifunza na wote waweze kutiwa moyo.
32 Kwa kuwa roho za manabii ziko chini ya uangalizi wa manabii.
33 Kwa kuwa Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani. Kama ilivyo katika makanisa yote ya waumini,
34 imewapasa wanawake wakae kimya katika kanisa. Kwa kuwa hawaruhusiwi kuzungumza. Badala yake, wanapaswa kuwa katika unyenyekevu, kama pia sheria inavyosema.
35 Kama kuna chochote wanatamani kujifunza, basi wawaulize waume zao nyumbani. Kwa kuwa ni aibu kwa mwanamke kuongea katika kanisa.
36 Je neno la Mungu lilitoka kwenu? Je limewafikia ninyi tu?
37 Kama mtu akijiona kuwa ni nabii au wa rohoni, inampasa ayatambue mambo ninayowaandikia ya kwamba ni maagizo ya Bwana.
38 Lakini asipotambua haya, mwacheni asitambuliwe.
39 Hivyo basi, kaka na dada zangu, takeni sana kutoa unabii, na msimzuie mtu yeyote kunena kwa lugha.
40 Lakini mambo yote yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu.