18
1 Baada ya mambo hayo, Paulo aliondoka Athene kwenda Korintho.
2 Huko akampata Myahudi aitwaye Akwila mtu wa kabila la Ponto, yeye na mke wake aitwaye Prisila walikuja kutoka huko Italia, kwa sababu Klaudia aliamuru Wayahudi wote waondoke Roma; Paulo akaja kwao;
3 Paulo akaishi na kufanya kazi nao kwani yeye anafanya kazi inayofanana na yao. Wao walikuwa ni watengeneza mahema.
4 Paulo akajadiliana nao katika sinagogi kila siku ya Sabato. Aliwashawishi Wayahudi pamoja na Wagiriki.
5 Lakini Sila na Timotheo walipokuja kutoka Makedonia, Paulo alisukumwa na Roho kuwashuhudia Wayahudi kuwa Yesu ndiye Kristo.
6 Wakati Wayahudi walipompinga na kumdhihaki, hivyo Paulo akakung'uta vazi lake mbele yao, na kuwaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu wenyewe; Mimi sina hatia. Kutoka sasa na kuendelea, nawaendea Mataifa”.
7 Hivyo akaondoka kutoka pale akaenda kwenye nyumba ya Tito Yusto, Mtu anayemwabudu Mungu. Nyumba yake iko karibu na sinagogi.
8 Krispo, kiongozi wa sinagogi pamoja na watu wa nyumbani mwake wakamwamini Bwana. Watu wengi wa Korintho waliomsikia Paulo akiongea waliamini na kubatizwa.
9 Bwana akamwambia Paulo usiku kwa njia ya maono, “Usiogope, lakini ongea na usinyamaze.
10 Kwani Mimi niko pamoja nawe, na hakuna atakayejaribu kukudhuru, maana nina watu wengi katika mji huu”.
11 Paulo akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha neno la Mungu miongoni mwao.
12 Lakini Galio alipofanywa mtawala wa Akaya, Wayahudi walisimama pamoja kinyume na Paulo na kumpeleka mbele ya kiti cha hukumu,
13 wakisema, “Mtu huyu huwashawishi watu wamwabudu Mungu kinyume cha sheria”.
14 Wakati Paulo alipokuwa akitaka kusema, Galio akawaambia Wayahudi, “Ninyi Wayahudi, kama ingelikuwa ni kosa au uhalifu, ingekuwa halali kuwashughulikia.
15 Lakini kwa sababu ni maswali, yanayohusu maneno na majina, na sheria zenu, basi hukumuni ninyi wenyewe. Mimi sitamani kuwa hakimu kwa habari ya mambo hayo.”
16 Galio akawaamuru waondoke mbele ya kiti cha hukumu,
17 Hivyo, wakamkamata Sosthene, kiongozi wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Lakini Galio hakujali walichokifanya.
18 Paulo, baada ya kukaa pale kwa muda mrefu, aliwaacha ndugu na kwenda kwa meli Siria pamoja na Prisila na Akwila. Kabla ya kuondoka bandarini, alinyoa nywele zake kwani alikuwa ameapa kuwa Mnadhiri.
19 Walipofika Efeso, Paulo alimwacha Prisila na Akwila pale, lakini yeye mwenyewe akaingia kwenye sinagogi na kujadiliana na Wayahudi.
20 Walipomwambia Paulo akae nao kwa muda mrefu, yeye alikataa.
21 Lakini akaondoka kwao, akawaambia, “Nitarudi tena kwenu, ikiwa ni mapenzi ya Mungu”. Baada ya hapo, akaondoka kwa meli kutoka Efeso.
22 Paulo alipotua Kaisaria, alipanda kwenda kusalimia Kanisa la Yerusalemu, kisha akashuka chini kwa kanisa la Antiokia.
23 Baada ya kukaa kwa muda pale, Paulo aliondoka kupitia maeneo ya Galatia na Frigia na kuwatia moyo wanafunzi wote.
24 Myahudi mmoja aitwaye Apolo, aliyezaliwa huko Alexandria, alikuja Efeso. Alikuwa na ufasaha katika kuongea na hodari katika Maandiko.
25 Apollo alikuwa ameelekezwa katika mafundisho ya Bwana. Kwa jinsi alivyokuwa na bidii katika roho, aliongea na kufundisha kwa usahihi mambo yanayomuhusu Yesu, ila alijua tu ubatizo wa Yohana.
26 Apolo akaanza kuzungumza kwa ujasiri katika hekalu. Lakini Prisila na Akwila walipomsikia, walifanya urafiki naye na wakamwelezea juu ya njia za Mungu kwa usahihi.
27 Alipotamani kuondoka kwenda Akaya, ndugu walimtia moyo na kuwaandikia barua wanafunzi walioko Akaya ili wapate kumpokea. Alipowasili, kwa neema aliwasaidia sana wale waliomini.
28 Kwa nguvu zake na maarifa, Apolo aliwazidi Wayahudi hadharani akionesha kupitia maandiko ya kuwa Yesu ndiye Kristo.