7
Haki Na Rehema, Sio Kufunga
Katika mwaka wa nne wa utawala wa Mfalme Dario, neno la Bwana lilimjia Zekaria siku ya nne ya mwezi wa tisa, mwezi wa Kisleu. Watu wa Betheli walikuwa wamemtuma Shareza na Regem-Meleki pamoja na watu wao, kumsihi Bwana kwa kuwauliza makuhani wa nyumba ya Bwana Mwenye Nguvu Zote na manabii, “Je, imempasa kuomboleza na kufunga katika mwezi wa tano, kama ambavyo nimekuwa nikifanya kwa miaka mingi?”
Kisha neno la Bwana Mwenye Nguvu Zote likanijia kusema: “Waulize watu wote wa nchi na makuhani, ‘Je, mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba kwa miaka sabini iliyopita, mlifunga kweli kwa ajili yangu? Na mlipokuwa mkila na kunywa, je, hamkuwa mnasherehekea kwa ajili ya nafsi zenu? Je, haya sio maneno ya Bwana aliyosema kupitia manabii waliotangulia, wakati Yerusalemu pamoja na miji inayoizunguka ilipokuwa katika hali ya utulivu na ya mafanikio, wakati Negebu na Shefala zikiwa zimekaliwa na watu?’ ”
Neno la Bwana likamjia tena Zekaria: “Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. 10 Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’
11 “Lakini wakakataa kusikiliza, wakanipa kisogo kwa ukaidi na kuziba masikio yao. 12 Wakaifanya mioyo yao migumu kama jiwe gumu na hawakuisikiliza sheria au maneno ambayo Bwana Mwenye Nguvu Zote aliyatuma kwa njia ya Roho wake kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo Bwana Mwenye Nguvu Zote alikasirika sana.
13 “ ‘Wakati nilipoita, hawakusikiliza, kwa hiyo walipoita, sikusikiliza,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. 14 ‘Niliwatawanya kwa upepo wa kisulisuli miongoni mwa mataifa yote, mahali ambapo walikuwa wageni. Nchi ikaachwa ukiwa nyuma yao kiasi kwamba hakuna aliyeweza kuingia au kutoka. Hivi ndivyo walivyoifanya ile nchi iliyokuwa imependeza kuwa ukiwa.’ ”