5
Maono Ya Sita: Kitabu Kinachoruka
Nikatazama tena: na hapo mbele yangu kulikuwa na kitabu kilichoruka!
Akaniuliza, “Unaona nini?”
Nikamjibu, “Naona kitabu kinachoruka chenye, urefu wa dhiraa ishirini* na upana wa dhiraa kumi.”
Akaniambia, “Hii ni laana inayotoka kwenda juu ya nchi yote, kwa kuwa kufuatana na yale yaliyoandikwa katika upande mmoja, kila mwizi atafukuziwa mbali, pia kufuatana na yaliyo upande wa pili, kila aapaye kwa uongo atafukuziwa mbali. Bwana Mwenye Nguvu Zote asema, ‘Nitaituma hiyo laana, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi na nyumba ya huyo aapaye kwa uongo kwa Jina langu. Itabaki katika nyumba yake na kuiharibu, pamoja na mbao zake na mawe yake.’ ”
Maono Ya Saba: Mwanamke Ndani Ya Kikapu
Kisha yule malaika aliyekuwa akizungumza nami akanijia na kuniambia, “Tazama juu uone ni nini kile kinachojitokeza.”
Nikamuuliza, “Ni kitu gani?”
Akanijibu, “Ni kikapu cha kupimia.” Kisha akaongeza kusema, “Huu ni uovu wa watu katika nchi nzima.”
Kisha kifuniko kilichotengenezwa kwa madini ya risasi kilichokuwa kimefunika kile kikapu, kiliinuliwa na ndani ya kile kikapu alikuwako mwanamke ameketi! Akasema, “Huu ni uovu,” tena akamsukumia ndani ya kikapu na kushindilia kifuniko juu ya mdomo wa kikapu.
Kisha nikatazama juu: na pale mbele yangu, walikuwepo wanawake wawili, wakiwa na upepo katika mabawa yao! Walikuwa na mabawa kama ya korongo, nao wakainua kile kikapu na kuruka nacho kati ya mbingu na nchi.
10 Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Wanakipeleka wapi hicho kikapu?”
11 Akanijibu, “Wanakipeleka katika nchi ya Babeli na kujenga nyumba kwa ajili yake. Itakapokuwa tayari, kikapu kitawekwa pale mahali pake.”
* 5:2 Dhiraa 20 ni sawa na mita 9. 5:2 Dhiraa 10 ni sawa mita 4.5.