31
Sehemu Za Ibada Za Kipagani Zaondolewa
1 Baada ya mambo haya yote kumalizika, Waisraeli ambao walikuwako huko wakaenda kwenye miji ya Yuda, wakayavunja yale mawe ya kuabudia na kuzikatakata zile nguzo za Ashera. Wakabomoa mahali pa juu pa kuabudia miungu pamoja na madhabahu zake kila mahali katika Yuda na Benyamini na katika Efraimu na Manase. Baada ya kuviharibu hivi vyote, Waisraeli wakarudi katika miji yao wenyewe na kwenye milki zao.
2 Hezekia akawapanga makuhani na Walawi katika migawanyo, kila mgawanyo kulingana na wajibu wao, kama ni makuhani au Walawi, ili kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, kuhudumu, kushukuru na kuimba sifa katika malango ya makao ya Bwana.
3 Mfalme akatoa matoleo kutoka mali zake mwenyewe kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na za jioni na sadaka za kuteketezwa kwa siku za Sabato, kwa Sikukuu za Mwezi Mwandamo na kwa ajili ya sikukuu zilizoamriwa kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana.
4 Akawaagiza watu wanaoishi Yerusalemu watoe sehemu iliyo haki ya makuhani na Walawi ili waweze kujitoa kikamilifu kutimiza wajibu wao katika Sheria ya Bwana.
5 Mara tu baada ya kutolewa tangazo hilo, Waisraeli wakatoa kwa ukarimu malimbuko ya nafaka zao, divai mpya, mafuta na asali pamoja na vyote vilivyotoka mashambani. Wakaleta kiasi kikubwa cha fungu la kumi la kila kitu.
6 Watu wa Israeli na Yuda walioishi katika miji ya Yuda wakaleta pia fungu la kumi la makundi yao ya ngʼombe na makundi ya kondoo na mbuzi pia na fungu la kumi la vitu vitakatifu vilivyowekwa wakfu kwa ajili ya Bwana Mungu wao na kuvikusanya katika malundo.
7 Wakaanza kufanya haya katika mwezi wa tatu na kumaliza katika mwezi wa saba.
8 Wakati Hezekia na maafisa wake walipokuja na kuona yale malundo, wakamsifu Bwana na kuwabariki watu wake Israeli.
9 Hezekia akawauliza makuhani na Walawi kuhusu yale malundo,
10 naye Azaria aliyekuwa kuhani mkuu, kutoka jamaa ya Sadoki, akajibu, “Tangu watu walipoanza kuleta sadaka zao katika Hekalu la Bwana tumekuwa na chakula cha kutosha na vingi vya kuweka akiba kwa sababu Bwana amewabariki watu wake, hivyo tumekuwa na kiasi kingi kilichobaki.”
Kutambuliwa Kwa Makuhani Na Walawi
11 Hezekia akatoa agizo la kutengeneza vyumba vya ghala katika Hekalu la Bwana nalo hili likafanyika.
12 Kisha kwa uaminifu wakaleta sadaka zao, mafungu yao ya kumi na vitu vilivyowekwa wakfu. Konania Mlawi, ndiye alikuwa msimamizi wa vitu hivi na Shimei ndugu yake ndiye alikuwa msaidizi wake.
13 Yehieli, Azazia, Nahathi, Asaheli, Yeremothi, Yozabadi, Elieli, Ismakia, Mahathi na Benaya walikuwa waangalizi chini ya Konania na Shimei ndugu yake, waliokuwa wamewekwa na Mfalme Hezekia na Azaria, afisa msimamizi wa Hekalu la Mungu.
14 Kore mwana wa Imna, Mlawi, bawabu wa Lango la Mashariki, alikuwa msimamizi wa sadaka za hiari zilizotolewa kwa Mungu, akiyagawanya hayo matoleo yaliyotolewa kwa Bwana na pia zile sadaka zilizowekwa wakfu.
15 Edeni, Miniamini, Yeshua, Shemaya, Amaria na Shekania walimsaidia kwa uaminifu katika miji ya makuhani, wakiwagawia makuhani wenzao kufuatana na migawanyo yao, wazee kwa vijana sawasawa.
16 Zaidi ya hao wakawagawia wanaume wenye umri wa miaka mitatu au zaidi ambao majina yao yalikuwa kwenye orodha ya vizazi, wale wote ambao wangeingia katika Hekalu la Bwana ili kufanya kazi zao mbalimbali za kila siku kulingana na wajibu katika mgawanyo wao.
17 Kuandikishwa kwa makuhani kulikuwa kwa kufuata chimbuko la nyumba za baba zao na Walawi kuanzia umri wa miaka ishirini au zaidi ilikuwa kufuatana na huduma zao, kwa migawanyo yao.
18 Makuhani waliandikishwa pamoja na watoto wao wadogo, wake zao, watoto wao wa kiume na wa kike, jamii yote iliandikishwa kwa kufuata orodha ya vizazi vyao. Kwa kuwa walikuwa waaminifu katika kujitakasa.
19 Kuhusu makuhani, wazao wa Aroni walioishi kwenye mashamba yaliyozunguka miji yao au katika miji mingine yoyote, watu walitajwa majina ili kumgawia kila mwanaume miongoni mwao na kwa wote waliokuwa katika orodha ya vizazi vya Walawi.
20 Hivi ndivyo Hezekia alivyofanya katika Yuda yote, akifanya lile lililo jema, sawa na la uaminifu mbele za Bwana Mungu wake.
21 Naye katika kila kitu alichofanya katika huduma kwenye Hekalu la Mungu na katika utii kwa sheria na amri, alimtafuta Mungu wake na kufanya kazi kwa moyo wake wote. Naye hivyo akafanikiwa.