21
Moyo wa mfalme uko katika mkono wa Bwana;
huuongoza kama mkondo wa maji, popote apendapo.
 
Njia zote za mwanadamu huonekana sawa kwake,
bali Bwana huupima moyo.
 
Kufanya yaliyo sawa na haki inakubalika
zaidi kwa Bwana kuliko dhabihu.
 
Macho ya kudharau na moyo wa kiburi,
ambavyo ni taa ya waovu, vyote ni dhambi!
 
Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida,
kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini.
 
Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo
ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha.
 
Jeuri ya waovu itawaburuta mbali,
kwa kuwa wanakataa kufanya yaliyo sawa.
 
Njia ya mwenye hatia ni ya upotovu,
bali tabia ya mtu asiye na hatia ni nyofu.
 
Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba,
kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.
 
10 Mtu mwovu hutamani sana ubaya,
jirani yake hapati huruma kutoka kwake.
 
11 Wakati mwenye mzaha ameadhibiwa,
mjinga hupata hekima;
wakati mtu mwenye hekima afundishwapo,
hupata maarifa.
 
12 Mwenye Haki huyajua yanayotendeka katika nyumba za waovu,
naye atawaangamiza waovu.
 
13 Mtu akiziba masikio asisikie kilio cha maskini,
yeye pia atalia, wala hatajibiwa.
 
14 Zawadi itolewayo kwa siri hutuliza hasira
na rushwa iliyofichwa kwenye nguo hutuliza ghadhabu kali.
 
15 Wakati haki imetendeka, huleta furaha kwa wenye haki,
bali kitisho kwa watenda mabaya.
 
16 Mtu anayepotea kutoka mapito ya ufahamu,
hupumzika katika kundi la waliokufa.
 
17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini,
yeyote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri.
 
18 Waovu huwa fidia kwa ajili ya wenye haki,
nao wasio waaminifu kwa ajili ya wanyofu.
 
19 Ni afadhali kuishi jangwani
kuliko kuishi na mke mgomvi na mkorofi.
 
20 Katika nyumba ya mwenye hekima
kuna akiba ya vyakula vizuri na mafuta,
lakini mtu mpumbavu
hutafuna vyote alivyo navyo.
 
21 Yeye afuatiaye haki na upendo
hupata uzima, mafanikio na heshima.
 
22 Mtu mwenye hekima huushambulia mji wa wenye nguvu,
na kuangusha ngome wanazozitegemea.
 
23 Yeye alindaye kinywa chake na ulimi wake
hujilinda na maafa.
 
24 Mtu mwenye kiburi na majivuno, “Mdhihaki” ndilo jina lake;
hutenda mambo kwa kiburi kilichozidi.
 
25 Kutamani sana kwa mvivu kutakuwa kifo chake,
kwa sababu mikono yake haitaki kufanya kazi.
 
26 Mchana kutwa hutamani zaidi,
lakini mnyofu hutoa pasipo kuzuia.
 
27 Dhabihu ya mtu mwovu ni chukizo,
si zaidi sana itolewapo kwa nia mbaya!
 
28 Shahidi wa uongo ataangamia,
bali maneno ya mwenye kusikia yatadumu.
 
29 Mtu mwovu ana uso wa ushupavu,
bali mtu mnyofu huzifikiria njia zake.
 
30 Hakuna hekima, wala akili, wala mpango
unaoweza kufaulu dhidi ya Bwana.
 
31 Farasi huandaliwa kwa ajili ya siku ya vita,
bali ushindi huwa kwa Bwana.