24
1 Basi Balaamu alipoona imempendeza Bwana kubariki Israeli, hakuendelea tena kutafuta uchawi kama nyakati nyingine, bali aligeuza uso wake kuelekea nyikani.
2 Balaamu alipotazama nje na kuona Israeli amepiga kambi kabila kwa kabila, Roho wa Mungu akawa juu yake,
3 naye akatoa ujumbe wake:
“Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori,
ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri;
4 ujumbe wake yeye ambaye husikia maneno ya Mungu,
ambaye huona maono kutoka kwa Mwenyezi,
ambaye huanguka kifudifudi, na ambaye macho yake yamefunguka:
5 “Tazama jinsi yalivyo mazuri mahema yako, ee Yakobo,
maskani yako, ee Israeli!
6 “Kama mabonde, yanaenea,
kama bustani kando ya mto,
kama miti ya udi iliyopandwa na Bwana,
kama mierezi kando ya maji.
7 Maji yatatiririka kutoka ndoo zake;
mbegu yake itakuwa na maji tele.
“Mfalme wake atakuwa mkuu kuliko Mfalme Agagi;
ufalme wake utatukuka.
8 “Mungu alimleta kutoka Misri;
yeye ana nguvu kama nyati.
Anayararua mataifa yaliyo adui zake,
na kuvunja mifupa yao vipande vipande;
huwachoma kwa mishale yake.
9 Hujikunyata na kuvizia kama simba,
kama simba jike; nani anayethubutu kumwamsha?
“Abarikiwe kila akubarikiye,
na alaaniwe kila akulaaniye!”
10 Ndipo hasira ya Balaki ikawaka dhidi ya Balaamu. Akapiga mikono yake pamoja, akamwambia Balaamu, “Nilikuita uje kuwalaani adui zangu, lakini umewabariki mara hizi tatu.
11 Sasa ondoka upesi uende nyumbani! Mimi nilisema nitakuzawadia vizuri sana, lakini Bwana amekuzuia usizawadiwe.”
12 Balaamu akamwambia Balaki, “Je, hukumbuki jinsi nilivyowaambia wajumbe uliowatuma kwangu? Niliwaambia hivi,
13 ‘Hata ikiwa Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, nisingeweza kufanya kitu chochote kwa matakwa yangu, kikiwa kizuri au kibaya, kwenda kinyume na agizo la Bwana, nami imenipasa kusema tu kile Bwana atakachosema’?
14 Sasa ninarudi kwa watu wangu. Lakini njoo, nikuonye kuhusu kile watu hawa watakachowatenda watu wako siku zijazo.”
Ujumbe Wa Nne Wa Balaamu
15 Kisha Balaamu akatoa ujumbe wake:
“Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori,
ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri;
16 ujumbe wake yeye ambaye husikia maneno ya Mungu,
ambaye ana maarifa kutoka kwa Aliye Juu Sana,
huona maono kutoka Mwenyezi,
ambaye huanguka kifudifudi
na ambaye macho yake yamefunguka:
17 “Namwona yeye, lakini si sasa;
namtazama yeye, lakini si karibu.
Nyota itatoka kwa Yakobo,
fimbo ya ufalme itainuka kutoka kwa Israeli.
Atawaponda Wamoabu vipaji vya nyuso
na mafuvu yote ya wana wa Shethi.
18 Edomu itamilikiwa,
Seiri, adui wake, itamilikiwa,
lakini Israeli atakuwa na nguvu.
19 Mtawala atakuja kutoka kwa Yakobo
na kuangamiza walionusurika katika mji.”
Ujumbe Wa Mwisho Wa Balaamu
20 Kisha Balaamu akawaona watu wa Amaleki, na kutoa ujumbe wake:
“Amaleki ilikuwa ya kwanza miongoni mwa mataifa,
lakini mwisho wake itaangamizwa milele.”
21 Kisha akawaona Wakeni, akatoa ujumbe wake:
“Makao yenu ni salama,
kiota chenu kiko kwenye mwamba.
22 Hata hivyo ninyi Wakeni mtaangamizwa
Ashuru atakapowachukua mateka.”
23 Ndipo akatoa ujumbe wake:
“Lo, ni nani atakayeweza kuishi wakati Mungu atakapofanya hili?
24 Meli zitakuja kutoka pwani za Kitimu,
zitaitiisha Ashuru na Eberi,
lakini nao pia wataangamizwa.”
25 Kisha Balaamu akainuka na kurudi nyumbani kwake, naye Balaki akashika njia yake.