20
Maji Kutoka Kwenye Mwamba
(Kutoka 17:1-7)
1 Katika mwezi wa kwanza jumuiya yote ya Kiisraeli ilifika kwenye Jangwa la Sini, nao wakakaa Kadeshi. Miriamu akafa huko na kuzikwa.
2 Mahali hapo hapakuwa na maji kwa ajili ya jumuiya hiyo, nao wakakusanyika ili kumpinga Mose na Aroni.
3 Watu wakagombana na Mose, na kusema, “Laiti tungelikufa wakati ndugu zetu walipoanguka na kufa mbele za Bwana!
4 Kwa nini mmeileta jumuiya ya Bwana kwenye jangwa hili, ili tufe humu, sisi na mifugo yetu?
5 Kwa nini mmetupandisha kutoka Misri mpaka mahali hapa pa kutisha? Hapa hakuna nafaka wala tini, zabibu au makomamanga. Wala hapa hakuna maji ya kunywa!”
6 Mose na Aroni wakaondoka pale kwenye kusanyiko mpaka kwenye mlango wa Hema la Kukutania na kuanguka kifudifudi, nao utukufu wa Bwana ukawatokea.
7 Bwana akamwambia Mose,
8 “Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Aroni mkusanye kusanyiko pamoja. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.”
9 Kwa hiyo Mose akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele za Bwana kama alivyomwagiza.
10 Mose na Aroni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Mose akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?”
11 Ndipo Mose akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa.
12 Lakini Bwana akamwambia Mose na Aroni, “Kwa sababu hamkuniamini mimi kiasi cha kuniheshimu kama mtakatifu machoni pa Waisraeli, hamtaiingiza jumuiya hii katika nchi ninayowapa.”
13 Haya yalikuwa maji ya Meriba, mahali pale ambapo Waisraeli waligombana na Bwana, naye akajionyesha mwenyewe huko kuwa mtakatifu katikati yao.
Edomu Wakatalia Israeli Kupita
14 Mose akawatuma wajumbe kutoka Kadeshi kwenda kwa mfalme wa Edomu, akisema:
“Hili ndilo ndugu yako Israeli asemalo: Wewe unafahamu juu ya taabu zote ambazo zimetupata.
15 Baba zetu walishuka Misri, nasi tumeishi huko miaka mingi. Wamisri walitutesa sisi na baba zetu,
16 lakini tulipomlilia Bwana, alisikia kilio chetu na akamtuma malaika akatutoa Misri.
“Sasa tupo hapa Kadeshi, mji ulio mpakani mwa nchi yako.
17 Tafadhali turuhusu tupite katika nchi yako. Hatutapita katika shamba lolote, wala shamba la mizabibu, au kunywa maji kutoka kwenye kisima chochote. Tutasafiri kufuata njia kuu ya mfalme, na hatutageuka kulia wala kushoto mpaka tuwe tumeshapita nchi yako.”
18 Lakini mfalme wa Edomu akajibu:
“Hamtapita hapa; kama mkijaribu kupita, tutatoka na kuwashambulia kwa upanga.”
19 Waisraeli wakajibu:
“Sisi tutafuata njia kuu; tena ikiwa sisi au mifugo yetu tutakunywa tone la maji yenu, tutalilipia. Sisi tunataka tu kupita kwa miguu, wala si kitu kingine chochote.”
20 Watu wa Edomu wakajibu tena:
“Hamwezi kupita hapa.”
Ndipo watu wa Edomu wakatoka dhidi ya Waisraeli, jeshi kubwa lenye nguvu.
21 Kwa kuwa Waedomu waliwakatalia Waisraeli kupita katika nchi yao, Israeli wakageuka, wakawaacha.
Kifo Cha Aroni
22 Jumuiya yote ya Kiisraeli ikaondoka kutoka Kadeshi, wakafika kwenye Mlima Hori.
23 Kwenye Mlima Hori, karibu na mpaka wa Edomu, Bwana akamwambia Mose na Aroni,
24 “Aroni atakusanywa pamoja na watu wake. Hataingia katika nchi ninayowapa Waisraeli, kwa sababu ninyi wawili mliasi dhidi ya agizo langu kwenye maji ya Meriba.
25 Watwae Aroni na Eleazari mwanawe, na uwapandishe juu katika Mlima wa Hori.
26 Mvue Aroni mavazi yake, na umvike Eleazari mwanawe, kwa maana Aroni atakusanywa pamoja na watu wake; atakufa huko.”
27 Mose akafanya kama Bwana alivyomwagiza: Wakapanda Mlima Hori mbele ya macho ya jumuiya yote ya Kiisraeli.
28 Mose akamvua Aroni mavazi yake na kumvika mwanawe Eleazari mavazi hayo. Naye Aroni akafia pale juu ya mlima. Kisha Mose na Eleazari wakateremka kutoka mlimani.
29 Jumuiya yote ilipofahamu kwamba Aroni amekufa, jamaa yote ya Kiisraeli wakamwomboleza kwa siku thelathini.