3
Mtu Aliyepooza Mkono Aponywa
(Mathayo 12:9-14; Luka 6:6-11)
Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi, na huko palikuwa na mtu aliyepooza mkono. Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki. Yesu akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele ya watu wote.”
Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza kimya.
Yesu akawatazama pande zote kwa hasira, akahuzunika sana kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa kabisa! Kisha Mafarisayo wakatoka nje, nao wakaanza kufanya shauri la kumuua Yesu wakiwa na Maherode.
Umati Wa Watu Wamfuata Yesu
Yesu pamoja na wanafunzi wake wakaondoka huko wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya ukamfuata. Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, umati mkubwa wa watu ukamjia kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumaya, na ngʼambo ya Yordani, pamoja na wale wa sehemu za karibu na Tiro na Sidoni. Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake waweke tayari mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga. 10 Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa. 11 Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.” 12 Lakini aliwaonya wasimseme yeye ni nani.
Yesu Achagua Mitume Kumi Na Wawili
(Mathayo 10:1-4; Luka 6:12-16)
13 Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia. 14 Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye, na awatume kwenda kuhubiri 15 na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu. 16 Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro); 17 Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo); 18 Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo, 19 na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.
Yesu Na Beelzebuli
(Mathayo 12:22-32; Luka 11:14-23; 12:10)
20 Kisha Yesu aliporudi nyumbani, umati wa watu ukakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula. 21 Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”
22 Walimu wa sheria walioteremka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli!* Anatoa pepo wachafu kwa kutumia mkuu wa pepo wachafu!”
23 Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani? 24  Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama. 25  Nayo nyumba kama ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama. 26  Naye Shetani kama akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama bali mwisho wake umewadia. 27  Hakuna mtu yeyote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu. Ndipo ataweza kuteka nyara mali zake. 28  Amin, nawaambia, dhambi zote na makufuru yote ya wanadamu watasamehewa. 29  Lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”
30 Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”
Mama Na Ndugu Zake Yesu
(Mathayo 12:46-50; Luka 8:19-21)
31 Kisha wakaja ndugu zake Yesu pamoja na mama yake. Wakasimama nje, wakamtuma mtu kumwita. 32 Umati wa watu ulikuwa umeketi kumzunguka, nao wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”
33 Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”
34 Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu. 35  Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”
* 3:22 Beelzebuli kwa Kiyunani ni Beelzebubu, yaani mkuu wa pepo wachafu.