13
Tubu, La Sivyo Utaangamia
1 Wakati huo huo, kulikuwa na watu waliomwambia Yesu habari za Wagalilaya ambao Pilato aliwaua, na damu ya hao watu akaichanganya na dhabihu yao waliyokuwa wanatoa.
2 Yesu akawauliza, “Mnadhani kwamba hawa Wagalilaya ambao walikufa kifo cha namna hiyo walikuwa na dhambi kuwazidi Wagalilaya wengine wote?
3 La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo.
4 Au wale watu kumi na wanane waliokufa walipoangukiwa na mnara huko Siloamu: mnadhani wao walikuwa waovu kuliko watu wote waliokuwa wanaishi Yerusalemu?
5 Nawaambia, la hasha! Ninyi nanyi msipotubu, wote mtaangamia vivyo hivyo.”
Mfano Wa Mti Usiozaa Matunda
6 Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini uliopandwa katika shamba lake la mizabibu, akaja ili kutafuta tini kwenye mti huo, lakini hakupata hata moja.
7 Hivyo akamwambia mtunza shamba: ‘Tazama, kwa muda wa miaka mitatu sasa nimekuwa nikija kutafuta matunda kwenye mtini huu, nami sikupata hata moja. Ukate! Kwa nini uendelee kuharibu ardhi?’
8 “Yule mtunza shamba akamjibu, ‘Bwana, uache tena kwa mwaka mmoja zaidi, nami nitaupalilia na kuuwekea mbolea.
9 Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vyema, la sivyo uukate.’ ”
Yesu Amponya Mwanamke Kilema Siku Ya Sabato
10 Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato.
11 Wakati huo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyooka wima.
12 Yesu alipomwona, akamwita, akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.”
13 Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu.
14 Lakini kiongozi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Akaambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi. Katika siku hizo, njooni mponywe, lakini si katika siku ya Sabato.”
15 Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ngʼombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato?
16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?”
17 Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.
Mfano Wa Punje Ya Haradali
(Mathayo 13:31-32; Marko 4:30-32)
18 Kisha Yesu akauliza, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaufananisha na nini?
19 Umefanana na punje ya haradali ambayo mtu aliichukua na kuipanda katika shamba lake. Nayo ikakua, ikawa mti nao ndege wa angani wakatengeneza viota vyao kwenye matawi yake.”
Mfano Wa Chachu
(Mathayo 13:33)
20 Yesu akauliza tena, “Nitaufananisha Ufalme wa Mungu na nini?
21 Unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga mpaka wote ukaumuka.”
Mlango Mwembamba
(Mathayo 7:13-14, 21-23)
22 Yesu akapita katika miji na vijiji, akifundisha wakati alisafiri kwenda Yerusalemu.
23 Mtu mmoja akamuuliza, “Bwana, ni watu wachache tu watakaookolewa?”
24 Yesu akawaambia, “Jitahidini sana kuingia kupitia mlango mwembamba, kwa maana nawaambia wengi watajaribu kuingia, lakini hawataweza.
25 Wakati mwenye nyumba atakapoondoka na kufunga mlango, mtasimama nje mkibisha mlango na kusema, ‘Bwana! Tufungulie mlango!’
“Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako.’
26 “Ndipo mtamjibu, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe, tena ulifundisha katika mitaa yetu.’
27 “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’
28 “Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapowaona Abrahamu, Isaki, Yakobo na manabii wote wakiwa katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje.
29 Watu watatoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini, nao wataketi kwenye sehemu walizoandaliwa karamuni katika Ufalme wa Mungu.
30 Tazama, kunao walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, nao wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”
Yesu Aomboleza Kwa Ajili Ya Yerusalemu
(Mathayo 23:37-39)
31 Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakamwendea Yesu na kumwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine kwa maana Herode anataka kukuua.”
32 Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Ninafukuza pepo wachafu na kuponya wagonjwa leo na kesho, nami siku ya tatu nitaikamilisha kazi yangu.’
33 Sina budi kuendelea na safari yangu leo, kesho na kesho kutwa: kwa maana haiwezekani nabii kufa mahali pengine isipokuwa Yerusalemu.
34 “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka!
35 Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana.’ ”