9
Bwana Anamtokea Solomoni
(2 Nyakati 7:11-22)
Solomoni alipomaliza kujenga Hekalu la Bwana na jumba la kifalme, alipokwisha kufanya yote aliyotaka kufanya, Bwana akamtokea mara ya pili, kama alivyokuwa amemtokea huko Gibeoni. Bwana akamwambia:
“Nimesikia dua na maombi uliyofanya mbele zangu, nimeliweka wakfu Hekalu hili ambalo umelijenga, kwa kuweka Jina langu humo milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwa humo siku zote.
“Kukuhusu wewe, kama ukienenda kwa unyofu wa moyo na uadilifu, kama baba yako Daudi alivyofanya na kutenda yote ninayoyaagiza kwa kutunza maagizo yangu na sheria, nitakiimarisha kiti chako cha enzi juu ya Israeli milele kama nilivyomwahidi Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe kuwa na mtu kwenye kiti cha enzi cha Israeli.’
“Lakini kama ninyi au wana wenu mkigeukia mbali nami na kuziacha amri na maagizo yangu niliyowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, basi nitakatilia mbali Israeli kutoka nchi niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Ndipo Israeli itakuwa kitu cha kudharauliwa na watu na kuwa kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote. Ingawa hekalu hili linavutia sasa, wote watakaolipita watashangaa na kudhihaki wakisema, ‘Kwa nini Bwana amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’ Watu watajibu, ‘Kwa sababu wamemwacha Bwana Mungu wao, aliyewatoa baba zao Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu Bwana ameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”
Shughuli Nyingine Za Solomoni
(2 Nyakati 8)
10 Miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Solomoni alijenga majengo haya mawili, yaani Hekalu la Bwana na jumba la kifalme, 11 Mfalme Solomoni akampa Hiramu mfalme wa Tiro miji ishirini katika Galilaya, kwa sababu Hiramu alikuwa amempatia mierezi yote, misunobari na dhahabu yote aliyohitaji. 12 Lakini Hiramu alipotoka Tiro kwenda kuiona ile miji ambayo Solomoni alikuwa amempa, hakupendezwa nayo. 13 Hiramu akauliza, “Hii ni miji ya namna gani uliyonipa, ndugu yangu?”
Naye akaiita nchi ya Kabul,* jina lililoko hadi leo. 14 Basi Hiramu alikuwa amempelekea mfalme talanta 120 za dhahabu.
15 Haya ni maelezo kuhusu kazi za kulazimishwa ambazo Mfalme Solomoni, alivyowafanyiza watu ili kulijenga hekalu la Bwana, na jumba lake la kifalme, na Milo, ukuta wa Yerusalemu, Hazori, Megido na Gezeri. 16 (Farao mfalme wa Misri alikuwa ameushambulia na kuuteka mji wa Gezeri. Alikuwa ameuchoma moto. Akawaua Wakanaani waliokuwa wakikaa humo na kisha kuutoa kwa binti yake, yaani mkewe Solomoni, kama zawadi ya arusi. 17 Solomoni akaujenga tena Gezeri.) Akajenga Beth-Horoni ya Chini, 18 akajenga Baalathi na Tamari kwenye jangwa katika eneo la nchi yake, 19 vilevile miji ya ghala na miji kwa ajili ya magari yake na kwa ajili ya farasi wake: chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, katika Lebanoni, na katika eneo yote aliyotawala.
20 Watu wote waliosalia kutoka kwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi (mataifa haya hayakuwa Waisraeli), 21 yaani, wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawangeweza kuwaangamiza kabisa: hawa Solomoni akawalazimisha kuwa watumwa katika shokoa, kama ilivyo hadi leo. 22 Lakini Solomoni hakumfanya yeyote wa Waisraeli kuwa mtumwa; wao ndio waliokuwa wapiganaji wake, maafisa wake wa serikali, maafisa wake, wakuu wake, majemadari wa jeshi wa magari yake ya vita na wapanda farasi. 23 Pia walikuwa maafisa wakuu wasimamizi wa miradi ya Solomoni: maafisa 550 waliwasimamia watu waliofanya kazi.
24 Baada ya binti Farao kuja kutoka Mji wa Daudi na kuingia jumba la kifalme ambalo Solomoni alikuwa amemjengea, akajenga Milo.
25 Solomoni akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani mara tatu kwa mwaka, juu ya madhabahu aliyokuwa amejengea kwa ajili ya Bwana, akifukiza uvumba mbele za Bwana pamoja na dhabihu hizo, hivyo kutimiza kanuni za hekalu.
26 Mfalme Solomoni pia akatengeneza pia meli huko Esion-Geberi, ambayo iko karibu na Elathi katika Edomu, kwenye ukingo wa Bahari ya Shamu.§ 27 Naye Hiramu akawatuma watu wake; mabaharia walioijua bahari, kuhudumu katika hizo meli pamoja na watu wa Solomoni. 28 Wakasafiri kwa bahari mpaka Ofiri na kurudi na talanta 420* za dhahabu, ambazo walimkabidhi Mfalme Solomoni.
* 9:13 Kabul maana yake isiyofaa kitu. 9:14 Talanta 120 za dhahabu ni sawa na tani 4.5. 9:15 Milo maana yake Boma la Ngome, pia 9:24. § 9:26 Yaani Bahari Nyekundu au Bahari ya Mafunjo. * 9:28 Talanta 420 za dhahabu ni sawa na tani 14.