4
Ukumbusho Wa Kuvuka Mto Yordani
Wakati taifa lote lilipokwisha kuvuka Mto Yordani, Bwana akamwambia Yoshua, “Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa watu, kila kabila mtu mmoja, nawe uwaambie wachukue mawe kumi na mawili katikati ya Mto Yordani, palepale makuhani waliposimama, wayachukue na kuyaweka mahali mtakapokaa usiku huu wa leo.”
Basi Yoshua akawaita watu kumi na wawili ambao alikuwa amewachagua kutoka miongoni mwa Waisraeli, mtu mmoja kutoka kila kabila, naye akawaambia, “Mtangulie mbele ya Sanduku la Bwana Mungu wenu, mwende katikati ya Mto Yordani. Kila mmoja wenu atainua jiwe begani mwake, kufuatana na hesabu ya makabila ya Waisraeli, kuwa kama ishara katikati yenu. Siku zijazo, wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Ni nini maana ya mawe haya?’ waambieni kwamba maji ya Mto Yordani yaliyokuwa yakitiririka yalitindika mbele ya Sanduku la Agano la Bwana. Wakati lilipovuka Yordani, maji ya Yordani yalitindika. Mawe haya yatakuwa kumbukumbu kwa watu wa Israeli milele.”
Hivyo Waisraeli wakafanya kama Yoshua alivyowaagiza. Wakachukua mawe kumi na mawili kutoka katikati ya Mto Yordani, kulingana na hesabu ya kabila za Waisraeli kama Bwana alivyomwambia Yoshua, nao wakayabeba hadi kambini mwao, mahali walipoyatua chini. Yoshua akayasimamisha yale mawe kumi na mawili ambayo yalikuwa katikati ya Mto Yordani, mahali pale ambapo miguu ya makuhani waliobeba Sanduku la Agano iliposimama. Nayo yako huko mpaka leo.
10 Makuhani waliobeba lile Sanduku walibakia wakiwa wamesimama katikati ya Mto Yordani mpaka kila kitu Bwana alichomwamuru Yoshua kilipokuwa kimefanywa na watu, sawasawa na vile Mose alivyokuwa amemwamuru Yoshua. Watu wakafanya haraka kuvuka, 11 na mara tu watu wote walipokwisha kuvuka, Sanduku la Bwana na makuhani wakavuka watu wakiwa wanatazama. 12 Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakavuka mbele ya Waisraeli, wakiwa wamevaa silaha, kama Mose alivyowaamuru. 13 Kiasi cha watu 40,000 waliojiandaa kwa vita walivuka mbele za Bwana hadi nchi tambarare za Yeriko kwa ajili ya vita.
14 Siku ile Bwana akamtukuza Yoshua mbele ya Israeli yote, nao wakamheshimu siku zote za maisha yake, kama vile walivyomheshimu Mose.
15 Basi Bwana akamwambia Yoshua, 16 “Waamuru hao makuhani wanaolibeba Sanduku la Ushuhuda, wapande kutoka ndani ya Mto Yordani.”
17 Kwa hiyo Yoshua akawaamuru hao makuhani akisema, “Pandeni kutoka ndani ya Mto Yordani.”
18 Nao makuhani wakapanda kutoka ndani ya Mto Yordani wakilibeba hilo Sanduku la Agano la Bwana. Mara tu walipoiweka miguu yao penye kingo, nje ya mto, maji ya Yordani yakarudi kufurika kama ilivyokuwa kabla.
19 Siku ya kumi ya mwezi wa kwanza watu walipanda kutoka Yordani na kupiga kambi huko Gilgali, kwenye mpaka wa mashariki ya Yeriko. 20 Naye Yoshua akayasimamisha huko Gilgali yale mawe kumi na mawili ambayo walikuwa wameyachukua katikati ya Mto Yordani. 21 Akawaambia Waisraeli, “Wazao wenu watakapowauliza baba zao siku zijazo wakisema, ‘Mawe haya maana yake ni nini?’ 22 Basi waambieni, ‘Israeli ilivukia mahali pakavu katika Mto Yordani.’ 23 Kwa maana Bwana Mungu wenu alikausha maji ya Yordani mbele yenu, hadi mlipomaliza kuvuka. Bwana Mungu wenu alifanya haya kwa Mto Yordani sawasawa na kile alichoifanyia Bahari ya Shamu wakati alipoikausha mbele yetu hadi tulipomaliza kuvuka. 24 Alifanya hivi ili kwamba mataifa yote ya dunia yapate kujua kuwa mkono wa Bwana ni wenye nguvu, na ili kwamba kila wakati mpate kumcha Bwana Mungu wenu.”