21
Miji Kwa Walawi
Basi viongozi wa jamaa ya Walawi, wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa nyingine za makabila ya Israeli huko Shilo katika Kanaani na kuwaambia, “Bwana aliamuru kupitia Mose kuwa mtupe miji ya kuishi yenye sehemu za malisho kwa mifugo yetu.” Hivyo kama vile Bwana alivyoamuru, Waisraeli wakawapa Walawi miji ifuatayo pamoja na sehemu zake za malisho kutoka urithi wao wenyewe.
Kura ya kwanza ikaangukia Wakohathi, ukoo kwa ukoo. Walawi waliokuwa wazao wa kuhani Aroni walipewa miji kumi na mitatu kutoka makabila ya Yuda, Simeoni na Benyamini. Wazao wengine waliobaki wa Wakohathi walipewa miji kumi kutoka koo za makabila ya Efraimu, Dani na nusu ya Manase.
Wazao wa Gershoni walipewa miji kumi na mitatu kutoka koo za makabila ya Isakari, Asheri, Naftali na nusu ya Manase huko Bashani.
Wazao wa Merari, ukoo kwa ukoo, walipewa miji kumi na miwili kutoka makabila ya Reubeni, Gadi na Zabuloni.
Kwa hiyo Waisraeli wakawapa Walawi miji hii pamoja na sehemu zake za malisho, kama vile Bwana alivyokuwa ameamuru kupitia kwa Mose.
 
Kutoka makabila ya Yuda na Simeoni waligawa miji ifuatayo kwa majina 10 (miji hii walipewa wazao wa Aroni ambao walitokana na koo za Wakohathi wa Walawi, kwa sababu kura ya kwanza iliwaangukia):
11 Waliwapa Kiriath-Arba (yaani Hebroni), pamoja na sehemu zake za malisho zilizoizunguka, katika nchi ya vilima ya Yuda. (Arba alikuwa baba wa Anaki.) 12 Lakini mashamba na vijiji vilivyozunguka mji mkubwa walikuwa wamempa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake.
13 Kwa hiyo wazao wa kuhani Aroni wakapewa Hebroni (mji mkuu wa makimbilio kwa ajili ya yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji), Libna, 14 Yatiri, Eshtemoa, 15 Holoni, Debiri, 16 Aini, Yuta na Beth-Shemeshi, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji tisa kutoka kwa makabila haya mawili.
17 Kutoka kabila la Benyamini wakawapa Gibeoni, Geba, 18 Anathothi na Almoni, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne.
19 Miji yote waliyopewa makuhani, wazao wa Aroni, ilikuwa kumi na mitatu, pamoja na sehemu zake za malisho.
 
20 Koo nyingine za Wakohathi, ambao pia ni Walawi, walipewa miji kutoka kabila la Efraimu:
21 Katika nchi ya vilima ya Efraimu walipewa Shekemu (mji mkubwa wa makimbilio kwa yeyote anayeshtakiwa kwa mauaji) na Gezeri, 22 Kibsaimu na Beth-Horoni, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne.
23 Pia kutoka kabila la Dani wakapokea Elteke, Gibethoni, 24 Aiyaloni na Gath-Rimoni pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne
25 Kutoka nusu ya kabila la Manase, wakapokea Taanaki na Gath-Rimoni pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji miwili.
26 Miji yote hii kumi pamoja na sehemu zake za malisho ilipewa koo za Wakohathi zilizobaki.
 
27 Koo za Walawi za Wagershoni walipewa:
kutoka nusu ya kabila la Manase,
Golani katika Bashani (mji mkuu wa makimbilio kwa yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji) na Beeshtera, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji miwili;
28 kutoka kabila la Isakari walipewa,
Kishioni, Daberathi, 29 Yarmuthi na En-Ganimu, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne
30 kutoka kabila la Asheri walipewa,
Mishali, Abdoni, 31 Helkathi na Rehobu, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne.
32 Kutoka kabila la Naftali walipewa,
Kedeshi katika Galilaya (mji wa makimbilio kwa ajili ya yeyote anayeshtakiwa kwa mauaji), Hamoth-Dori na Kartani, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji mitano.
33 Miji yote ya koo za Wagershoni ilikuwa kumi na mitatu, pamoja na sehemu zake za malisho.
 
34 Koo za Wamerari (Walawi waliobaki) walipewa:
kutoka kabila la Zabuloni,
Yokneamu, Karta, 35 Dimna na Nahalali, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne;
36 kutoka kabila la Reubeni walipewa
Bezeri, Yahasa, 37 Kedemothi na Mefaathi, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne;
38 kutoka kabila la Gadi walipewa,
Ramothi katika Gileadi (mji wa makimbilio kwa ajili ya yeyote anayeshtakiwa kwa ajili ya mauaji), Mahanaimu, 39 Heshboni na Yazeri, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne.
40 Miji yote waliyopewa koo za Wamerari, waliokuwa mabaki ya Walawi, ilikuwa ni kumi na miwili.
41 Miji yote ya Walawi katika eneo lililoshikwa na Waisraeli lilikuwa arobaini na minane, pamoja na sehemu zake za malisho. 42 Kila mmoja wa miji hii ulikuwa na sehemu ya malisho kuuzunguka; ndivyo ilivyokuwa kwa miji hii yote.
 
43 Kwa hiyo Bwana akawapa Israeli nchi yote aliyokuwa ameapa kuwapa baba zao, nao wakaimiliki na kukaa humo. 44  Bwana akawapa pumziko kila upande, kama vile alivyokuwa amewaapia baba zao, hakuna hata mmoja wa adui zao aliyeweza kusimama mbele yao, Bwana akawatia adui zao wote mikononi mwao. 45 Hakuna hata mojawapo ya ahadi nzuri ya Bwana kwa nyumba ya Israeli ambayo haikutimia; kila moja ilitimia.