9
Abimeleki Ajaribu Kuanzisha Ufalme
Siku moja Abimeleki mwana wa Yerub-Baali akaenda kwa ndugu ya mama yake huko Shekemu na kuwaambia yeye na ukoo wote wa mama yake, “Waulizeni watu wote wa Shekemu, ‘Lipi lililo bora kwenu: Kutawaliwa na wana wote sabini wa Yerub-Baali, au mtu mmoja peke yake?’ Kumbukeni kwamba, mimi ni mfupa wenu nyama yenu hasa.”
Ndugu za mama yake walipowaeleza watu wote wa Shekemu, wakaelekea kumkubali Abimeleki, kwa kuwa walisema, “Yeye ni ndugu yetu.” Wakampa shekeli sabini* za fedha kutoka hekalu la Baal-Berithi, naye Abimeleki akaitumia kuajiri watu ovyo wasiojali, wakawa ndio wafuasi wake. Akaenda nyumbani kwa baba yake huko Ofra, na juu ya jiwe moja wakawaua ndugu zake sabini, ambao ni wana wa Yerub-Baali. Lakini Yothamu, mwana mdogo wa wote wa Yerub-Baali, akaokoka kwa kujificha. Ndipo watu wote wa Shekemu na Beth-Milo wakakusanyika pamoja chini ya mti mkubwa wa mwaloni penye nguzo iliyoko Shekemu wakamvika Abimeleki taji kuwa mfalme.
Yothamu alipoambiwa hayo, akapanda juu ya kilele cha mlima Gerizimu, akawapazia sauti yake akawaambia, “Nisikilizeni enyi watu wa Shekemu, ili Mungu naye apate kuwasikiliza ninyi. Siku moja miti ilitoka ili kwenda kujitawazia mfalme. Ikauambia mzeituni, ‘Wewe uwe mfalme wetu.’
“Lakini mzeituni ukaijibu, ‘Je, niache kutoa mafuta yangu ambayo kwake miungu na wanadamu huheshimiwa, ili nikawe juu ya miti?’
10 “Kisha miti ikauambia mtini, ‘Njoo na uwe mfalme wetu!’
11 “Lakini mtini ukaijibu, ‘Je, niache kutoa matunda yangu mazuri na matamu, ili niende nikawe juu ya miti?’
12 “Ndipo miti ikauambia mzabibu, ‘Njoo na uwe mfalme wetu.’
13 “Lakini mzabibu ukaijibu, ‘Je, niache kutoa divai yangu inayofurahisha miungu na wanadamu ili nikawe juu ya miti?’
14 “Mwishoni miti yote ikauambia mti wa miiba, ‘Njoo na uwe mfalme wetu.’
15 “Nao mti wa miiba ukaijibu, ‘Kama kweli mnataka niwe mfalme wenu, basi njooni mpate kupumzika chini ya kivuli changu. Lakini kama sivyo, moto na utoke kwenye mti wa miiba ukateketeze mierezi ya Lebanoni!’
16 “Basi ikiwa mmetenda kwa uaminifu na heshima kumfanya Abimeleki kuwa mfalme, na kama mmetendea vyema Yerub-Baali na jamaa yake kama ilivyostahili: 17 kwa kuwa baba yangu aliwapigania ninyi na kuhatarisha nafsi yake na kuwaokoa ninyi kutoka mikononi mwa Wamidiani 18 (lakini leo mmeasi dhidi ya jamaa ya baba yangu, na kuwaua wanawe sabini juu ya jiwe moja, nanyi mkamfanya Abimeleki mwana wa mwanamke mtumwa kuwa mfalme juu ya Shekemu, kwa kuwa yeye ni ndugu yenu), 19 nanyi kama basi mmemtendea Yerub-Baali na jamaa yake kwa heshima na uaminifu, basi Abimeleki na awe furaha yenu, nanyi mwe furaha yake pia! 20 Lakini kama sivyo, moto na utoke kwa Abimeleki na uwateketeze, ninyi watu wa Shekemu na Beth-Milo, nao moto utoke kwenu, watu wa Shekemu na Beth-Milo umteketeze Abimeleki!”
21 Ndipo Yothamu akakimbia, akatoroka akaenda Beeri, akaishi huko, kwa sababu alimwogopa ndugu yake Abimeleki.
22 Baada ya Abimeleki kutawala Israeli kwa muda wa miaka mitatu, 23 Mungu akaruhusu roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu, nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa hila. 24 Hili lilitokea ili ule ukatili waliotendewa hao wana sabini wa Yerub-Baali upatilizwe, na damu yao iwe juu ya Abimeleki ndugu yao aliyewaua, na pia iwe juu ya watu wa Shekemu, ambao walimsaidia kuua ndugu zake. 25 Hivyo, kutokana na uadui juu yake watu wa Shekemu wakaweka watu wa kumvizia katika vilele vya milima. Wakawanyangʼanya watu wote waliopita karibu nao, nayo haya yakaarifiwa kwa Abimeleki.
26 Basi Gaali mwana wa Ebedi akaenda pamoja na ndugu zake wakaingia Shekemu, nao watu wa huko wakamtumainia yeye. 27 Wakaenda mashambani mwao kuvuna zabibu na kuzisindika hizo zabibu, wakafanya sikukuu katika hekalu la mungu wao. Wakati wakila na kunywa, wakamlaani Abimeleki. 28 Gaali mwana wa Ebedi akasema, “Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tumtumikie? Je, yeye si mwana wa Yerub-Baali? Naye Zebuli si ndiye msaidizi wake? Basi watumikieni watu wa Hamori, babaye Shekemu. Kwa nini tumtumikie Abimeleki? 29 Laiti watu hawa wangekuwa chini ya amri yangu! Basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ondoa jeshi lako lote.’ ”
30 Zebuli aliyekuwa mtawala wa mji aliposikia aliyosema Gaali mwana wa Ebedi, akakasirika sana. 31 Akatuma ujumbe uende kwa Abimeleki kwa siri na kusema, “Gaali mwana wa Ebedi na ndugu zake wamekuja Shekemu, na wanauchochea mji huu kinyume chako. 32 Sasa, basi, usiku huu wewe uondoke na watu wako ili mje kuwavizia mashambani. 33 Kisha asubuhi wakati wa kuchomoza jua, amka mapema na ujipange dhidi ya huo mji. Wakati yeye na jeshi lililo pamoja naye watakapotoka kukabiliana nanyi, mwaweza kuwatendea kwa kadiri mnavyoweza.”
34 Kwa hiyo Abimeleki pamoja na jeshi lake lote wakaondoka usiku na kujificha karibu na Shekemu wakiwa vikosi vinne. 35 Basi Gaali mwana wa Ebedi alikuwa ametoka nje akawa amesimama katika ingilio la mji wakati ule ule ambao Abimeleki na watu wake walipokuwa wanatoka sehemu zao za maficho.
36 Gaali alipowaona, akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka kwenye vilele vya milima!”
Zebuli akajibu, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.”
37 Lakini Gaali akasema tena, “Tazama, watu wanashuka kutoka katikati ya nchi na kikosi kimoja kinakuja kutoka Tabur-Ezeri na kikosi kingine kutoka upande wa Elon-Meonenimu.”
38 Ndipo Zebuli akamwambia, “Kuko wapi kujivuna kwako sasa, wewe uliyesema, ‘Huyo Abimeleki ni nani hata tumtumikie?’ Hawa si wale watu uliowadharau? Toka nje sasa ukapigane nao!”
39 Basi Gaali akatoka akawaongoza watu wa Shekemu kupigana na Abimeleki. 40 Abimeleki akamfukuza, watu wengi wakajeruhiwa katika kukimbia huko, njia nzima hadi kwenye ingilio la lango. 41 Abimeleki akakaa Aruma, naye Zebuli akawafukuza Gaali na ndugu zake watoke Shekemu.
42 Kesho yake watu wa Shekemu wakatoka wakaenda mashambani, Abimeleki akaambiwa juu ya jambo hili. 43 Hivyo akawachukua watu wake, akawagawanya katika vikosi vitatu na kuwaweka waviziao huko mashambani. Alipowaona watu wanatoka kwenda nje ya mji, akainuka dhidi yao na kuwashambulia. 44 Abimeleki pamoja na vile vikosi wakaharakisha kwenda mbele kwenye nafasi, mahali pa ingilio la lango la mji. Vile vikosi viwili vikawawahi wale waliokuwa mashambani na kuwaua. 45 Siku hiyo nzima Abimeleki akazidisha mashambulizi yake dhidi ya mji hadi akawa ameuteka na kuwaua watu wa huo mji. Kisha akauangamiza mji na kusambaza chumvi juu yake.
46 Kwa kusikia jambo hili watu wote katika mnara wa Shekemu, wakaingia kwenye ngome ya hekalu la El-Berithi. 47 Abimeleki aliposikia kuwa wamekusanyika huko, 48 yeye na watu wake wote wakakwea kwenye Mlima Salmoni. Abimeleki akachukua shoka, akakata baadhi ya matawi, ambayo aliyachukua mabegani. Akawaagiza wale watu waliokuwa pamoja naye kuwa, “Fanyeni kile mlichoona mimi nikifanya!” 49 Basi watu wote wakakata matawi na kumfuata Abimeleki. Wakayakusanya hayo matawi juu ya ngome na kuitia moto ili kuwachoma wale watu wote waliokuwa ndani yake. Hivyo watu wote katika mnara wa Shekemu, karibia watu 1,000 waume kwa wake, pia wakafa.
50 Baadaye Abimeleki akaenda Thebesi na kuuzingira kwa jeshi na kuuteka. 51 Hata hivyo, ndani ya huo mji kulikuwa na mnara imara, ambako watu wote wa mji wanaume na wanawake, watu wote wa mji, walikimbilia ndani yake. Wakajifungia ndani yake na kupanda juu ya paa la mnara. 52 Abimeleki akaja kwenye ule mnara na kuushambulia, lakini alipokaribia kwenye ingilio la mnara ili kuuchoma kwa moto, 53 mwanamke mmoja akaangusha sehemu ya juu ya jiwe la kusagia juu ya kichwa cha Abimeleki, likapasua fuvu la kichwa chake.
54 Akamwita kwa haraka kijana yule aliyechukua silaha zake, na kumwambia, “Chukua upanga wako na uniue, watu wasije wakasema kwamba, ‘Mwanamke amemuua.’ ” Basi yule kijana akamchoma upanga, naye akafa. 55 Waisraeli walipoona kuwa Abimeleki amekufa, kila mtu akaenda nyumbani kwake.
56 Hivyo ndivyo Mungu alivyolipiza uovu ule ambao Abimeleki alikuwa ameutenda kwa baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini. 57 Mungu akawapatiliza watu wa Shekemu uovu wao juu ya vichwa vyao, na juu yao ikaja laana ya Yothamu mwana wa Yerub-Baali.
* 9:4 Shekeli 70 za fedha ni sawa na gramu 800.