6
Gideoni
1 Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele za Bwana, naye kwa miaka saba Bwana akawatia mikononi mwa Wamidiani.
2 Mkono wa Midiani ukawa na nguvu dhidi ya Israeli na kwa ajili ya Wamidiani, Waisraeli wakajitengenezea mahali pa kujificha milimani, kwenye mapango na ngome.
3 Kila wakati Waisraeli walipopanda mazao mashambani, Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki walivamia nchi yao.
4 Wakapiga kambi katika mashamba yao na kuharibu mazao ya nchi yote hadi kufikia Gaza, wala hawakuacha kiumbe chochote kilicho hai kwa Waisraeli, iwe kondoo au ngʼombe au punda.
5 Walipanda na mifugo yao na mahema yao, mfano wa makundi ya nzige. Ilikuwa haiwezekani kuwahesabu watu na ngamia zao; wakavamia nchi ili kuiharibu.
6 Waisraeli wakafanywa kuwa maskini sana na Wamidiani, hata Israeli wakamlilia Bwana kuomba msaada.
7 Waisraeli walipomlilia Bwana kwa sababu ya Wamidiani,
8 Bwana akawapelekea nabii, ambaye aliwaambia, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: Niliwapandisha mtoke Misri, toka nchi ya utumwa.
9 Nikawanyakua kutoka mikononi mwa Wamisri na kutoka mikononi mwa watesi wenu wote. Nikawafukuza watoke mbele yenu nami nikawapa ninyi nchi yao.
10 Nikawaambia, ‘Mimi ndimi Bwana Mungu wenu; msiiabudu miungu ya Waamori, ambayo mnakaa katika nchi yao!’ Lakini ninyi hamkuitii sauti yangu.”
11 Malaika wa Bwana akaja akaketi chini ya mti wa mwaloni huko Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi, Mwabiezeri, ambako Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione.
12 Malaika wa Bwana alipomtokea Gideoni, akamwambia, “Bwana yu pamoja nawe, Ewe shujaa mwenye nguvu.”
13 Gideoni akajibu, “Ee Bwana wangu, kama Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi basi yale matendo yake makuu baba zetu waliyotusimulia juu yake waliposema, ‘Je, Bwana hakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasa Bwana ametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.”
14 Bwana akamgeukia na kusema “Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?”
15 Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.”
16 Bwana akamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.”
17 Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonyesha kweli kwamba ni wewe unayesema nami.
18 Tafadhali ninakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea sadaka yangu na kuiweka mbele yako.”
Naye Bwana akamwambia, “Nitangoja mpaka utakaporudi.”
19 Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa moja ya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mti wa mwaloni na kumpa.
20 Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo.
21 Malaika wa Bwana akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa Bwana akatoweka kutoka machoni pake.
22 Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa Bwana, akapiga kelele kwa mshangao, akasema, “Ole wangu, Bwana Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa Bwana uso kwa uso!”
23 Lakini Bwana akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.”
24 Hivyo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu mahali pale na kupaita, Yehova-Shalom. Mpaka leo ingalipo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri.
25 Usiku ule ule Bwana akamwambia, “Mchukue ngʼombe dume wa baba yako, yaani, yule wa pili mwenye miaka saba, na ubomoe madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako, na ukaikate Ashera iliyo karibu nayo.
26 Kisha mjengee Bwana Mungu wako, madhabahu halisi, kwa taratibu zake, juu ya huu mwamba. Kwa kutumia kuni za hiyo nguzo ya Ashera uliyoikatakata, mtoe sadaka huyo dume wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa.”
27 Basi Gideoni akawachukua watumishi wake kumi na kufanya kama Bwana alivyomwambia. Lakini kwa kuwa aliwaogopa jamaa yake na watu wa mji, akafanya haya usiku badala ya mchana.
28 Watu wa mji walipoamka asubuhi, tazama madhabahu ya Baali imebomolewa na nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwakatwa na yule ngʼombe wa pili ametolewa sadaka juu ya madhabahu yaliyojengwa upya!
29 Wakaulizana, “Ni nani aliyetenda mambo haya?”
Walipochunguza kwa makini, wakaambiwa, “Ni Gideoni mwana wa Yoashi, ndiye alitenda hivi.”
30 Watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mlete mwanao hapa. Ni lazima afe, kwa sababu amebomoa madhabahu ya Baali na kukatakata nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”
31 Lakini Yoashi akauambia ule umati uliokuwa umezunguka ukiwa kinyume naye, “Je, ninyi mtamtetea Baali? Mnajaribu kumwokoa? Yeyote mwenye kumpigania atauawa kufikia kesho asubuhi! Kama Baali ni mungu kweli, anaweza kujitetea mwenyewe wakati mtu anapobomoa madhabahu yake.”
32 Basi siku ile wakamwita Gideoni “Yerub-Baali,” yaani, “Baali na ashindane naye,” kwa sababu alibomoa madhabahu yake.
33 Basi Wamidiani wote, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki wakaunganisha majeshi yao, wakavuka ngʼambo ya Yordani na kupiga kambi katika Bonde la Yezreeli.
34 Ndipo Roho wa Bwana akamjia Gideoni, akapiga tarumbeta, akiwaita Waabiezeri ili wamfuate.
35 Akatuma wajumbe waende katika Manase yote, akiwataka wachukue silaha na pia katika Asheri, Zabuloni na Naftali, nao wakakwea ili kukutana nao.
36 Gideoni akamwambia Mungu, “Kama utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu, kama ulivyoahidi:
37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo kwenye kiwanja cha kupuria nafaka, na kama utakuwepo umande juu ya ngozi tu, nayo ardhi yote ikiwa kavu, ndipo nitakapojua kuwa utaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.”
38 Hivyo ndivyo ilivyotokea. Gideoni akaamka asubuhi na mapema kesho yake, akaikamua ile ngozi, umande ukatoka, maji ya kujaa bakuli.
39 Kisha Gideoni akamwambia Bwana, “Usinikasirikie. Ninaomba nifanye ombi moja lingine. Niruhusu nifanye jaribio jingine moja kwa ngozi hii. Wakati huu uifanye ngozi hii kavu na ardhi yote ifunikwe na umande.”
40 Usiku ule Mungu akafanya hivyo. Ngozi ile ilikuwa kavu, nayo ardhi yote ikafunikwa na umande.