5
Imani Katika Mwana Wa Mungu Huushinda Ulimwengu
1 Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ndiye Kristo amezaliwa na Mungu, na yeyote ampendaye Baba humpenda pia mtoto aliyezaliwa naye.
2 Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu, kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake.
3 Huku ndiko kumpenda Mungu, yaani, kuzitii amri zake. Nazo amri zake si nzito.
4 Kwa maana kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, yaani, hiyo imani yetu.
5 Ni nani yule aushindaye ulimwengu? Ni yule tu aaminiye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.
Ushuhuda Kuhusu Mwana Wa Mungu
6 Huyu ndiye alikuja kwa maji na damu, yaani, Yesu Kristo. Hakuja kwa maji peke yake, bali kwa maji na damu. Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli.
7 Kwa maana wako watatu washuhudiao[ mbinguni: hao ni Baba, Neno na Roho Mtakatifu. Hawa watatu ni umoja.
8 Pia wako mashahidi watatu duniani]: Roho, Maji na Damu; hawa watatu wanakubaliana katika umoja.
9 Kama tunaukubali ushuhuda wa wanadamu, basi ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi, kwa kuwa huu ndio ushuhuda wa Mungu kwamba amemshuhudia Mwanawe.
10 Kila mtu amwaminiye Mwana wa Mungu anao huu ushuhuda moyoni mwake. Kila mtu asiyemwamini Mungu amemfanya yeye kuwa mwongo, kwa sababu hakuamini ushuhuda Mungu alioutoa kuhusu Mwanawe.
11 Huu ndio ushuhuda: kwamba Mungu ametupa uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe.
12 Aliye naye Mwana wa Mungu anao uzima, yeye asiye na Mwana wa Mungu hana uzima.
Maneno Ya Mwisho
13 Nawaandikia mambo haya ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu ili mpate kujua ya kuwa mnao uzima wa milele.
14 Huu ndio ujasiri tulio nao tunapomkaribia Mungu, kwamba kama tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.
15 Nasi kama tunajua atusikia, lolote tuombalo, tunajua ya kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba.
16 Kama mtu akimwona ndugu yake akitenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo. Ninamaanisha wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo.
17 Jambo lolote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti.
18 Tunajua ya kuwa yeye aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, bali aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hawezi kumdhuru.
19 Sisi twajua kuwa tu watoto wa Mungu na ya kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu.
20 Nasi pia twajua ya kwamba Mwana wa Mungu amekuja, naye ametupa sisi ufahamu ili tupate kumjua yeye aliye Kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye Kweli, yaani, ndani ya Yesu Kristo Mwanawe. Yeye ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele.
21 Watoto wapendwa, jilindeni nafsi zenu kutokana na sanamu. Amen.