3
1 Tazameni ni pendo kuu namna gani alilotupa Baba, kwamba sisi tuitwe wana wa Mungu! Na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.
2 Wapendwa, sasa tu wana wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua ya kwamba yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo.
3 Kila mmoja mwenye matumaini haya ndani yake hujitakasa, kama vile yeye alivyo mtakatifu.
4 Kila mtu atendaye dhambi afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi.
5 Lakini mwajua ya kuwa yeye alidhihirishwa ili aziondoe dhambi, wala ndani yake hamna dhambi.
6 Kila mtu akaaye ndani yake hatendi dhambi. Kila mtu atendaye dhambi hakumwona yeye wala hakumtambua.
7 Watoto wapendwa, mtu yeyote asiwadanganye. Kila mtu atendaye haki ana haki, kama yeye alivyo na haki.
8 Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi.
9 Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu.
10 Kwa jinsi hii tunaweza kujua dhahiri watoto wa Mungu na pia watoto wa ibilisi. Yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.
Mpendane Ninyi Kwa Ninyi
11 Hili ndilo neno mlilolisikia tangu mwanzo: Kwamba imetupasa tupendane sisi kwa sisi.
12 Msiwe kama Kaini aliyekuwa wa yule mwovu akamuua ndugu yake. Basi kwa nini alimuua? Ni kwa sababu matendo yake Kaini yalikuwa mabaya na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.
13 Ndugu zangu, ninyi msistaajabu kama ulimwengu ukiwachukia.
14 Sisi tunajua ya kwamba tumepita mautini kuingia uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Kila asiyempenda ndugu yake akaa mautini.
15 Yeyote amchukiaye ndugu yake ni muuaji, nanyi mwajua ya kwamba muuaji hana uzima wa milele ndani yake.
16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu.
17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo?
18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.
19 Basi hivi ndivyo tutakavyoweza kujua ya kuwa sisi tu wa kweli na hivyo twaithibitisha mioyo yetu mbele za Mungu
20 kila mara mioyo yetu inapotuhukumu. Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu, naye anajua kila kitu.
21 Wapendwa, kama mioyo yetu haituhukumu, tunao ujasiri mbele za Mungu,
22 lolote tuombalo, twalipokea kutoka kwake, kwa sababu tumezitii amri zake na kutenda yale yanayompendeza.
23 Hii ndiyo amri yake: kwamba tuliamini Jina la Mwanawe, Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi kama yeye alivyotuamuru.
24 Wale wote wanaozishika amri zake hukaa ndani yake na yeye ndani yao. Hivi ndivyo tunavyojua kwamba anakaa ndani yetu. Nasi twajua hili kwa njia ya Roho yule aliyetupa.